Kwenye uchumi kuna sheria inaitwa kupungua kwa marejesho, au kwa kiingereza law of diminishing return.

Sheria hii inasema kwamba kuna wakati marejesho ya kitu fulani yanapungua licha ya juhudi zinazowekwa zinavyozidi kuwa kubwa. Yaani juhudi zinaongezwa, lakini matokeo yanazidi kuwa madogo.

Wapo watu ambao wameanzisha biashara, zikawa zinafanya vizuri sana mwanzoni na wakajua wameshaigundua siri ya mafanikio kwenye biashara. Lakini baadaye biashara inaanza kushuka na kila juhudi wanazochukua biashara inazidi kushuka.

Wengi wanakuwa hawaamini kama biashara waliyonayo inaelekea kufa, hivyo wanakazana na kila kitu na mwishowe biashara inakuwa na wanabaki hawana kitu.

Unapaswa kujua sheria hii ya kupungua kwa marejesho, ili uweze kuchukua hatua kabla mambo hayajawa mabaya zaidi. Na ili kuitumia sheria hii, lazima uwe unaipima biashara yako kwa usahihi, lazima uwe unajua kila kinachoendelea kwenye biashara yako.

Wakati mwingine kupungua kwa marejesho kunaweza kusiwe kwa biashara nzima, badala yake kunakuwa kwa huduma au bidhaa fulani unayokuwa unatoa.

Kwa mfano umekuja na huduma au bidhaa ambayo mwanzoni wateja walikuwa wengi, lakini baadaye ukawa umeshauzia sehemu kubwa ya soko na hakuna tena wateja wapya, hata ukazane kiasi gani, mauzo yanazidi kupungua kadiri muda unavyokwenda.

Katika hali kama hiyo, lazima ufanye mabadiliko labda ya bidhaa au huduma yako au kuwafanya wateja ambao walishanunua tayari wanunue tena.

Unafikiri kwa nini makampuni ya simu yanatoa matoleo mengi ya simu, ambayo hayana tofauti kubwa? Kwa sababu makampuni haya yanajua hata juhudi ziwe kubwa kiasi gani, kuna wakati toleo litafika kwenye kilele na mauzo hayataongezeka tena. Hivyo wanakuja na toleo jipya na mauzo yanaanza tena.

Using’ang’ane na biashara au bidhaa ambayo imeshafikia ukomo wa ukuaji, jua wakati gani unapata marejesho yanayopungua na uchukue hatua sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha