Siku mpya,
Siku nzuri,
Na siku tuliyokuwa tunaisubiri sana imewadia.
Ni ile siku ambayo tulijiambia kesho tutafanya hivi.
Kesho ndiyo imeshafika na sasa ni wajibu kwetu kwenda kufanya kile tulichojiahidi kufanya.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari JIWEKEE UKOMO…
Tunaishi kwenye zama ambazo moja ya vitu ambavyo tunajivunia ni kutokuwa na ukomo.
Tuna nafasi ya kufanya kila tunachotaka bila ya kuzuiwa na yeyote.
Hatuna ukomo kwenye matumizi ya muda, tunafanya tu kila tunachotaka kufanya na muda wetu.
Hatuna ukomo kwenye matumizi ya fedha, tunatumia mpaka zinaisha na tunakopa kwa kadiri tunavyoweza.
Hatuna ukomo kwenye nini tunaweza kukubali na kukataa, tunasema ndiyo kwenye kila kitu mpaka tunashindwa kujua kipi cha kufanya.
Mtu mmoja amewahi kusema kwamba ukiingia kwenye casino, hakuna saa na wala huoni nje, hivyo huwezi kujua ni saa ngapi mpaka kunakucha.
Sasa angalia ufanano wa casino na mitandao ya kijamii, ukiingia kwenye mitandao ya kijamii, kila unapopangusa unakitana na kitu kizuri, na kinakuja kizuri zaidi, hakuna mwisho wa vitu vizuri.
Unajiambia unaingia mara moja, unakuja kustuka ni masaa unaendelea kugusa tu.
Rafiki, bila ya kujiwekea ukomo, hutaweza kufanua makubwa hapa duniani.
Utahangaika sana na kila kitu, utachoka na mwisho wa siku hutaona kipi umefanya.
Unahitaji kuwa na ukomo kwenye vitu gani pekee utafanya na vipi utapuuza.
Unahitaji kuwa na ukomo kwenye muda wako, kwa kutenga muda kwa kitu fulani na ukiisha unaacha, hata kama umefikia pazuri kiasi gani.
Unahitaji kuwa na ukomo kwenye fedha zako, kwa kutenga fungu kwa ajili ya kitu fulani, likiisha ndiyo basi, hakuna fedha nyingine.
Jiwekee ukomo, ndiyo njia pekee ya kuweza kufanya yale muhimu na kufanikiwa.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujiwekea ukomo kwenye muda wako, nguvu zako na fedha zako.
#JiwekeeUkomo #Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha