Rafiki yangu mpendwa,

Nimekuwa nakuambia kitu kimoja muhimu sana, kinachokuzuia usipate kile unachotaka, ni kile ambacho unacho kwa sasa.

Ndiyo, namaanisha kinachokuzuia usipate kazi unayotaka, ni kazi uliyonayo sasa. Na kinachokuzuia usifikie biashara unayotaka, ni biashara au kile unachofanya sasa.

Na hata kwenye fedha, kinachokuzuia usipate fedha unazotaka, ni zile fedha ulizonazo au unazopata sasa.

Kwa kifupi ni kwamba, chochote ulichonacho sasa au unachopata sasa ndiyo kinachokuzuia wewe usipate kile unachotaka zaidi.

Na hii ni kwa sababu sisi binadamu tuna tabia ya kuwa na mapenzi na vitu ambavyo tayari tunavyo, na hivyo hatupendi kuvipoteza, tunaendelea kuving’ang’ania hata pale ambapo havina tena msaada kwetu.

Hali hii ndiyo kikwazo kikubwa sana cha mafanikio kwa wengi, wanashindwa kupiga hatua zaidi kwa sababu ya hatua ambayo tayari wameshapiga.

KIPATO KWA BLOG

Leo nakwenda kukushirikisha falsafa muhimu sana unayohitaji kuitumia ili kuweza kufanya maamuzi magumu kwa mafanikio yako. Falsafa hii inaitwa KUKATA MGUU ILI KUOKOA MAISHA.

Ukweli ni kwamba kila kiungo ambacho kipo kwenye mwili wako ni muhimu sana kwa maisha yako. Una macho mawili, mikono miwili, miguu miwili, vyote vina umuhimu. Japo vitu vingi vipo viwili, kimoja kikiondoka, maisha lazima yatabadilika sana, hayatabaki kama yalivyokuwa mwanzo. Na ndiyo maana tunapenda sana viungo vyetu.

Lakini inafika wakati kwamba kiungo ambacho tunacho, kinakuwa na matatizo ambayo kama kisipoondolewa, basi mwili mzima utaathirika. Mfano mguu umepata kidonda kisichopona na sehemu ya kidonda hicho imeshaoza, na kidonda kinaendelea kupanda na mguu. Kama mguu huo hautaondolewa, sumu ya kidonda itasambaa mwili mzima na utaishia kufa. Je katika hali kama hii utang’ang’ana kubaki na mguu wako kwa sababu hutaki kuishi na mguu mmoja?

Utakapopewa ushahidi na wataalamu kwamba kuendelea kuwepo kwa mguu wa aina hiyo ni hatari kwako, hutakataa kuhusiana na kuondolewa kwa mguu huo. Utakuwa tayari kukata mguu ili kuokoa maisha.

Lakini inapokuja kwenye mafanikio, inapokuja kwenye kufanya maamuzi muhimu sana kwako, huwa unaogopa kukata mguu kuokoa maisha. Huwa unang’ang’ana na mguu wako mbovu na mwishowe maisha yanaangamia kabisa.

Kuna vitu kwenye maisha yako unahitaji kuvipoteza kabisa ili kuweza kupata kile unachotaka, kuweza kupiga hatua zaidi kuelekea unakotaka kufika. Kuna vitu hata kama unavipenda kiasi gani, hutaweza kufanikiwa kama hutaondokana navyo au hutavibadili.

Ndiyo maana ni muhimu sana kujua falsafa hii na wakati wa kuitumia, kukata mguu ili kuokoa maisha.

SOMA; Kitu Kimoja Kinachowatofautisha Waliofanikiwa Na Walioshindwa.

Kuna baadhi ya maeneo ambayo watu wanaogopa sana kutumia falsafa hii na wanapata madhara makubwa, mfano;

  1. Kushindwa kuachana na tabia ambayo mtu umeshaizoea na hivyo kushindwa kubadili maisha.
  2. Kushindwa kumfukuza mfanyakazi ambaye ameshaonesha dalili za kukosa uaminifu au kutokujituma na mwishowe biashara inakufa.
  3. Kushindwa kuvunja mahusiano ambayo yanakuweka kwenye misukosuko kila siku na mwishowe maisha yako yanakuwa hovyo.
  4. Kushindwa kuacha kazi ambayo inakulipa kidogo na kwenda kwenye kujiajiri au kufanya biashara ambayo umekuwa unafikiria kuifanya kwa muda mrefu.
  5. Kushindwa kuacha biashara moja unayoipenda na kwenda kwenye nyingine ambayo itakuwezesha kupiga hatua zaidi.
  6. Kushindwa kujinyima kile unachotamani sana kwa sasa, ili kuweza kupata kile unachohitaji zaidi kwa baadaye.
  7. Kushindwa kusema hapana kwenye vitu vizuri unavyoshirikishwa, ili uweze kuweka nguvu na muda wako kwa vile ambavyo ni muhimu zaidi kwako.

Kwenye kila eneo la maisha yako, kuna maeneo ambayo hutaki kukata mguu ili kuokoa maisha, unakazana kubaki na mguu wako na maisha yako, kitu ambacho hakiwezekani.

Mafanikio kwenye maisha ni mchezo wa kulipa gharama, kila unachotaka, utakipata kama tu utakuwa tayari kulipa gharama. Kadiri unavyotaka makubwa, ndivyo unavyohitaji kulipa gharama kubwa zaidi.

Pia mafanikio ni mchezo unaohitaji kujitoa kafara, unahitaji kutoa vile vitu ambavyo unavipenda sana, kuachana navyo ili uweze kufanikiwa. Kwa sababu vile vitu unavyovipenda ndiyo vimeshikilia hisia zako na hivyo huwezi kufikiri kwa umakini. Lakini unapoachana na vitu hivyo, hisia zako zinakuwa huru, unaweza kufikiri kwa umakini na ukaona vitu kama vilivyo.

Kuwa tayari kukata mguu ili kuokoa maisha, usikimbie wala kukwepa kufanya maamuzi magumu ambayo yatakuwezesha kufanikiwa sana kwenye maisha yako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL