Msongo wa mawazo ni tatizo linalowasumbua wengi. Na kwa dunia ya sasa, dunia inayokwenda kwa kasi na hakuna mwenye muda, msongo wa mawazo unaongezeka kila siku na kwa wengi.
Lakini upo mfumo wa maisha ambao unachochea sana msongo wa mawazo kwa wengi.
Mfumo huo ni kutokuwa na taarifa sahihi juu ya vitu, mazingira na wewe mwenyewe.
Kama hujui kitu fulani, mwanzoni utapata shida sana, kila utakachotaka kufanya na kitu hicho kitakupa msongo wa mawazo, kwa sababu hujui utafanyaje. Fikiria mara ya kwanza kwako kufanya kitu ambacho hujawahi kufanya, labda kuendesha gari, au baiskeli au pikipiki, ulikuwa na msongo wa mawazo kila ulipofikiria kuendesha. Lakini baadaye ulizoea na msongo ukaondoka.
Kama hujui pale ulipo, yaani huyaelewi mazingira, utasumbuka sana na msongo wa mawazo. Pata picha kwa mara ya kwanza unaenda eneo ambalo hulijui, ni kwa namna gani unapata msongo wa mawazo kufikiria kufika kule unakotaka kufika.
Kadhalika, kama hujijui vizuri wewe mwenyewe, kama hujui ni vitu gani unaweza kukamilisha, kila wakati utakuwa na msongo wa mawazo. Kila unapokutana na magumu utajiambia ndiyo mwisho wako, lakini baadaye utagundua magumu hayo umeweza kuyavuka vizuri.
Rafiki, ninachotaka kukuambia hapa ni kitu kimoja, kila unapojikuta kwenye msongo wa mawazo, jiulize ni nini ambacho hujui. Ni kitu gani hujui, mazingira gani huyajui na nini usichojua kuhusu wewe binafsi. Kwa kuangalia maeneo hayo, utaweza kupata utatuzi wa msongo wa mawazo.
Kadiri unavyojua, ndivyo msongo wa mawazo unavyozidi kupungua.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,