Nikiwa nasoma kitabu, mwandishi alitoa kauli hii, napenda sana kulala, hivyo kitu pekee kinachokatisha usingizi wangu inabidi kiwe kinalipa fedha ya kutosha.

Kwa asili sisi binadamu ni wavivu, na uvivu wetu ndiyo uliotuwezesha sisi binadamu kuweza kudumu mpaka sasa.

Uvivu ni njia ya akili kutunza nguvu zetu kwa kutukatisha tamaa tusifanye mambo ambayo siyo muhimu zaidi kwetu, ili nguvu hizo ziweze kutumika pale jambo muhimu sana linapotokea.

Chukua mfano upo msituni na unatumia nguvu zako kurusha mawe na kukimbia kimbia bila maana, baadaye unachoka. Ukiwa umejipumzisha, mara anatokea simba, inabidi ukimbie, lakini huwezi, hivyo unaliwa na simba. Hivyo watangulizi wetu, walijifunza kwa kadiri wanavyotumia nguvu zao kwa kiasi kidogo, kwenye kupata chakula na kuzaliana, nguvu nyingi ziliweza kutumika kujilinda na kujiokoa kutoka kwenye hatari.

Wote tunajua ya kwamba kwa sasa hakuna hatari kama kipindi hicho cha kuishi msituni, lakini bado akili zetu zinaishi kwa msingi huo.

Hivyo unaweza kutumia uvivu wako kufanikiwa sana kwenye maisha yako. Unachofanya ni kuchagua yale mambo ambayo ni muhimu zaidi kwako, yale ambayo yanakupeleka kwenye mafanikio unayotaka. Kisha kuyapa hayo kipaumbele pekee. Hivyo nguvu zako unapeleka kwenye mambo hayo tu, na muda mwingine unautumia kufanya kile unachopenda, ambacho hakihusiani na kazi.

Kwa mfano kama unapenda kulala kama anavyosema mwandishi niliyekushirikisha awali, basi weka kitu pekee kitakachokatisha usingizi wako kiwe kinachangia kuelekea kwenye malengo yako makubwa, la sivyo jibu linakuwa hapana.

Najua siyo vitu vyote unavyopenda vinaweza kutumika kupimia kazi zako, lakini kama kuna kitu cha kivivu, kisichokuwa na madhara kwa afya yako unapenda kufanya, kitumie hicho kama njia pekee ya kupima uzito wa kazi unayotaka kwenda kufanya.

Kuna kauli moja nilijifunza kwa bilionea Mark Cuban kuhusu vikao, anasema hahudhurii kikao chochote, labda kama kuna mtu anamlipa, nimekuwa natumia kauli hiyo na vikao vingi vinakosa sifa ya malipo na inanisaidia kuokoa muda sana.

Angalia kipi unapenda kufanya na kipe kipaumbele katika kuchagua nini unafanya na muda wako, na uvuvi wako utakusaidia sana kufanikiwa, maana utatumia nguvu zako kwa yale ambayo ni muhimu zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha