Rafiki yangu mpendwa,

Watu wengi wanapenda kupiga hatua kwenye maisha yao, lakini ni wachache sana wanaopiga hatua hasa na kufanikiwa.

Wengi hubaki na matamanio ya kufanikiwa lakini wasifanikiwe. Na sababu huwa ni visingizio ambavyo wengi wanavyo.

Watu wengi wana visingizio vingi kwa nini hawafanikiwi au kupiga hatua. Wana kila sababu kwa nini watashindwa na hivyo hawajaribu kabisa.

Na sababu kubwa inayotumiwa na wengi, ni kukosa mtaji au kuwa na mtaji kidogo. Wengi wametumia sababu hii kushindwa kupiga hatua kubwa na kufanikiwa.

Kwenye makala ya leo ya ushauri, nakwenda kukuonesha jinsi gani unaweza kutengeneza mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuanza na mtaji mdogo kabisa.

Na hivi ndivyo msomaji mwenzetu alivyotuandikia akiomba mtaji kwenye hili;

“Mimi nina mtaji mdogo tu ni kama laki mbili hivi je nianzie wapi ili nifikie malengo yangu.” – Brandi J. G.

Mtaji mdogo wa shilingi laki mbili siyo mdogo sana kiasi cha kushindwa kuutumia kufanya makubwa, na pia siyo mkubwa kiasi cha kuweza kuamua nini ufanye.

Shilingi laki mbili ni kiasi ambacho unaweza kuanza nacho na baada ya muda ukaweza kupiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako.

Lakini unapoanza biashara yoyote kwa mtaji kidogo, unapaswa ujue kwamba mtaji mkubwa utakuwa wewe mwenyewe. Hivyo muda wako, nguvu zako na maarifa yako yatajazia kwenye ule mtaji ambao unakosekana kwenye fedha.

Hivyo basi, matumizi sahihi ya mtaji mdogo unaoanza nao, yanapaswa kuwa kujijenga wewe binafsi. Kwa sababu kama wewe hautakuwa vizuri, chochote utakachoanzisha kitashindwa, na hapo ndipo wengi walipoangukia.

Hivyo ushauri ambao nautoa kwa mtu yeyote mwenye mtaji kidogo, kwanza wekeza ndani yako.

Ninaposema wekeza ndani yako, namaanisha ujiongeze kwa upande wa maarifa, utumie mtaji mdogo ulionao kujifunza kwa kina kuhusu chochote unachotaka kufanya.

Kulingana na kiasi cha fedha ulichonacho, chagua njia itakayokufaa ya wewe kujifunza kwa kina kuhusiana na unachotaka kufanya.

Unaweza kununua vitabu vinavyoeleza vizuri kuhusiana na unachofanya, kisha kuvisoma kwa umakini na kuchagua hatua unazokwenda kufanyia kazi.

Kama unapanga kuingia kwenye biashara, nunua vitabu vya biashara, mafanikio na hata ufanisi. Soma vitabu hivyo kwa kina, andika yale uliyojifunza na unayokwenda kufanyia kazi, kisha anza kufanyia kazi mara moja.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Jifunze kila unachopaswa kuhusu biashara, kuanzia kuja na jina la biashara, kupata mtaji au kuanza biashara bila ya mtaji, masoko, mauzo, mzunguko wa fedha na hata mbinu za ukuzaji wa biashara.

Pia jifunze vitu kama uongozi na kujenga mahusiano mazuri na watu wengine. Kwa sababu hivyo pia ni muhimu kwa mafanikio yako kibiashara.

Rafiki, utaona kwa mtaji kidogo ulionao sijakushauri sana kuhusu biashara gani ufanye, bali nimekushauri kuanza kuwekeza ndani yako mwenyewe. Hii ni kwa sababu wengi wanaingia kwenye biashara wakiwa hawana uelewa wa kutosha, na wanachoishia kupata ni kupoteza fedha zao.

Utaumia sana pale utakapopoteza fedha kidogo uliyodunduliza na usione chochote ulichopata. Weka kipaumbele kwenye kuwekeza ndani yako kwanza, jifunze na chukua hatua kwenye yale unayojifunza, utaweza kupiga hatua zaidi.

Ukishakuwa na maarifa sahihi kuhusu biashara, unaweza kuanza biashara yoyote unayotaka, hata kama hutakuwa na mtaji kabisa. Pia utajifunza njia za kutumia fedha za watu wengine katika kuanzisha na kukuza biashara yako, huku ukinufaika wewe na wao wakinufaika pia.

Kitu kingine muhimu sana utakachojifunza kwenye kuwekeza kwako binafsi, ni uvumilivu. Unapoanza biashara kwa mtaji kidogo au bila ya mtaji kabisa, muda unahitajika, hivyo lazima uwe mvumilivu.

Anza na uwekezaji wa ndani yako binafsi, na kama utahitaji kujua baadhi ya biashara unazoweza kuanza kwa mtaji kidogo ulionao, unaweza kujifunza hapa; USHAURI; Biashara Unazoweza Kuanza Kwa Mtaji Wa Tsh Laki Mbili Na Kuweza Kufanikiwa.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog