Leo fanya zoezi hili rahisi sana kwenye biashara yako,

Mkumbuke mteja mmoja ambaye amewahi kununua kwako siku za nyuma, lakini siku za karibuni hujamwona akinunua tena.

Ingia kwenye mawasiliano ya wateja wako, na chukua mteja mmoja, au wachache ambao hujawaona wakinunua mara kwa mara kisha fanya nao mawasiliano.

Na mawasiliano hayahitaji kuwa ya kuwauliza kwa nini hawanunui, au kuwaambia waje kununua.

Bali yanakuwa mawasiliano ya kutaka kujua wanaendeleaje na maisha yao, na pia kujua kile walichonunua kiliwasaidiaje. Kingine unahitaji kujua ni kama wana changamoto zozote zinazohusiana na ile biashara unayofanya wewe.

Mwisho kabisa, baada ya kujua kinachoendelea kwenye maisha yake, mkaribishe kwenye biashara yako, kwa kumweleza huduma bora zaidi unazotoa sasa. Kama tangu anunue kuna vitu umeboresha, mweleze uboreshaji uliofanyika na jinsi unavyoweza kumsaidia yeye zaidi.

Fanya hivi kwa wateja wachache kila siku, kwa muda ambao huna wateja kwenye biashara yako, au huna cha kufanya, chagua kuwasiliana na wateja wachache wa zamani. Unaweza kuona ni hatua ndogo, lakini baada ya muda utajikuta unawarudisha wateja wengi sana kwenye biashara yako.

Tengeneza ratiba ya kuwasiliana na wateja 10 kila siku, au kama huwezi basi wasiliana na wateja watano. Ndani ya mwezi mmoja, utajikuta na wateja zaidi ya 100 wanakuja kwenye biashara yako. Na hapo unakuwa hujatumia gharama za ziada.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha