Changamoto kubwa kwenye biashara ni pale ushindani unapowekwa kwenye bei. Pale wenzako wanapopunguza bei ili kupata wateja zaidi.
Ni rahisi kukimbilia na wewe kupunguza bei, lakini hiyo siyo mbinu ambayo itakuwezesha kufanikiwa kwenye biashara.
Kwa sababu unapopunguza bei, unapunguza faida na kadiri faidia inavyokuwa ndogo ndivyo huduma unazotoa zinavyokuwa za hovyo.
Hivyo basi, pale washindani wako wa kibiashara wanapopunguza bei, wewe ongeza thamani. Mwanzoni anayepunguza bei atapata wateja wengi, lakini mpango huo hautaweza kudumu. Kwa sababu kwa bei ndogo, huduma zitakuwa mbovu na wateja watachoka.
Wewe unapoongeza thamani, mwanzoni wateja hawatakuwa wengi, lakini wale wachache utakaowapata, wataamini na pia wataleta wateja wengi zaidi. Utaweza kutoa huduma bora kwa wateja wachache wanaojali na utaweza kutengeneza faida nzuri.
Usikimbilie kupungua bei, kwa sababu bei rahisi itakupoteza kabisa kutoka sokoni. Mara zote ongeza thamani na itakulipa zaidi na zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,