Najua hili limekuwa linatokea kwenye biashara yako mara nyingi.

Kuna mteja ambaye amekuwa hanunui kwako, anakupita na kwenda kununua kwa muuzaji mwingine, japo na wewe unauza kile anachokwenda kununua kule.

Sasa inatokea siku moja, mteja huyo anaenda kule anakoenda kununua, anakosa kitu hicho, halafu anarudi kwako. Unachukua hatua gani kwenye hali kama hii.

Nimewahi kuona wafanyabiashara wanakataa kuwauzia wateja wa aina hii, au wengine wanawasema kwamba wamezoea kule sasa leo wamekosa. Yote hayo ni ujinga, kupoteza muda wako na kupoteza nafasi ya kutengeneza mteja ambaye atakuwa mwaminifu kwa biashara yako.

Adhabu ya mteja asiyenunua kwako mara kwa mara ni kumpa huduma bora sana siku ambayo amekuja kununua. Hakikisha unampa huduma ambayo haipati kule anakokwenda kununua mara kwa mara, na hapo utakuwa umejipa nafasi ya kumshawishi aendelee kuja kwako.

Kila mteja uliyenaye sasa, kuna mahali alikuwa ananunua kabla hajaja kwako, na kila mteja anayenunua kwako, anaweza kupata sehemu nzuri zaidi ya kununua. Usipoteze muda na nguvu kuwakasirikia wateja ambao kwa sababu moja au nyingine hawajanunua kwako.

Peleka muda na nguvu hizo kwenye kutoa huduma bora kabisa kwa wale wateja wanaokuja kwenye bishara yako, mfanye mteja awe na shauku ya kurudi tena kwenye biashara yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha