Rafiki yangu mpendwa,

Juma jingine zuri sana kuwahi kutokea kwenye maisha yetu, juma la 37 kwa mwaka huu 2018 linatuaga. Japo juma hili linaisha, alama tulizoweka kwenye maisha yetu na ya wale wanaotuzunguka zitadumu na sisi milele.

Na kama kuna uzembe tuliofanya kwenye juma hili, tutaujutia maisha yetu yote, lakini kama tutalifanya juma tunalokwenda kuanza kuwa bora zaidi, basi tutaweza kufuta uzembe tuliofanya juma hili.

Ndiyo maana ni muhimu sana kujifanyia tathmini kila juma, kwa sababu ni rahisi kuchukua hatua haraka pale unapoona mambo hayaendi vizuri. Hivyo unapomaliza kusoma hizi tano za juma, tulia na ufanye tathmini ya juma zima jinsi lilivyokwenda kwako, kisha uweke mipango ya juma linalokwenda kuanza.

Kama ilivyo utamaduni wetu, nakukaribisha kwenye TANO ZA JUMA, ambapo kila mwisho wa juma nakuandalia sindano tano muhimu zitakazotibu maeneo mbalimbali ya maisha yako. Kwa sababu kanuni yetu ni hii; MAARIFA SAHIHI + KUCHUKUA HATUA KUBWA = MAFANIKIO MAKUBWA.

Mimi nakupa maarifa sahihi, ni wajibu wako kuchukua hatua kubwa ili uweze kupata matokeo makubwa. Imani yangu ni unachukua hatua kwa kila unachojifunza, na kama huchukui hatua, sijui nini kitaweza kukusaidia. Rai yangu kwako ni moja, kila unapojifunza kitu, chukua hatua, maisha yako yatakuwa bora sana.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

#1 KITABU NILICHOSOMA; JINSI YA KUNUNUA WATEJA KWENYE BIASHARA YAKO.

Kazi kubwa ya kila biashara ni kununua wateja wa biashara hiyo. Sasa ili biashara iweze kufanikiwa, lazima iweze kununua wateja bora kwa gharama ambazo siyo kubwa. Kitu ambacho wafanyabiashara wengi siyo tu hawakifanyii kazi, ila hata hawakijui.

Inawezekana upo kwenye biashara, lakini hujui kama biashara yako inanunua wateja. Sasa nikuambie tu, kila biashara huwa inatumia fedha kununua wateja, na biashara yako pia inatumia fedha kununua wateja.

Labda nikuulize swali, biashara yako inatumia gharama kiasi gani kununua wateja? Na je gharama ambazo biashara yako inatumia kununua wateja zinarudi? Najua maswali haya yanaweza kukuacha ukiwa umeduwaa kwa sababu hujawahi kufikiria kuhusu kununua wateja.

Sasa kwenye kitabu nilichosoma juma hili; BUYING CUSTOMERS, kilichoandikwa na kocha wa biashara Bradley Sugars, mwandishi ametushirikisha njia sahihi za kununua wateja bora wa biashara zetu na kwa gharama nafuu ambazo biashara inaweza kumudu.

Kwa kuanza, kila biashara huwa inanunua wateja. Kila hatua unayotumia kuwafanya wateja wajue kuhusu uwepo wa biashara yako, ni kununua wateja. Kama umewahi kutangaza biashara yako, umewahi kuandaa vipeperushi, kama umetengeneza bango, au kuuza vitu kwa pamoja kwa bei ya punguzo, kama umewahi kupunguza bei ili mteja anunue, au kutoa zawadi kwa mteja anayenunua. Kama umewahi kutoa usafiri kwa mteja, au kumpelekea alichonunua, au kumwomba mteja wako akuletee wateja zaidi. Zote hizo ni harakati za kununua wateja unazotumia kwenye biashara yako.

Sasa kuna ambazo zinakuletea wateja bora, nyingine hazikuletei wateja wazuri. Nyingine ni za gharama kubwa kwako, nyingine ni za gharama ndogo.

Kupitia kitabu cha BUYING CUSTOMERS, tunakwenda kujifunza jinsi ya kununua wateja bora kwa gharama nafuu kwenye biashara zetu.

NJIA TANO ZA KUTENGENEZA FAIDA KWENYE BIASHARA.

Kabla ya kuingia kwenye kununua wateja, mwandishi anatukumbusha njia tano za kutengeneza faida kwenye biashara yako. Njia hizi zinategemeana na zinaenda kama ngazi, hivyo ili kunufaika lazima uzifanyie kazi kwa pamoja.

Njia ya kwanza ni kuongeza idadi ya watu wanaoijua biashara yako. Na hapa ndipo zoezi zima la kununua wateja linapofanya kazi. Kadiri watu wengi wanavyojua kuhusu biashara yako, ndivyo inakuwa rahisi kwako kuwageuza watu hao kuwa wateja. Kama watu 1000 ndiyo wanaojua kuhusu uwepo wako, ukiongeza watu 100 unakuwa umeenda mbele zaidi.

Njia ya pili ni kuwageuza wanaojua kuhusu biashara yako kuwa wateja halisi. Mtu kujua biashara yako haimaanishi ndiyo mteja wa biashara hiyo. Mteja ni yule ambaye ametoa fedha na kununua kitu kwenye biashara yako. ili kuongeza wateja wa biashara yako, unahitaji kuwashawishi wale wanaojua kuhusu biashara yako wanunue kile unachouza.

Njia ya tatu ni kuwafanya wateja warudi kununua tena na tena. Kama umetumia gharama kumfikisha mteja kwenye biashara yako, jua kabisa akinunua mara moja ni hasara kwako. Unapata faida pale mteja anaponunua tena na tena na tena. Na unachopaswa kujua ni kwamba, ni rahisi kumuuzia mteja ambaye alishanunua kwako kuliko kumuuzia mteja mpya kabisa. Hivyo weka juhudi katika kuwafanya wateja waendelee kununua kwako zaidi na zaidi.

Njia ya nne; kuongeza kiwango cha manunuzi. Kama mteja akija kwako ananunua kitu kimoja, unahitaji kumshawishi anunue kitu kingine ambacho kinaendana na kile alichonunua. Hapo unaongeza mauzo na kuongeza faida pia. Kwa mfano kama unauza vifaa vya ujenzi, akaja mteja kununua rangi, unahitaji kumshawishi anunue na brashi za kupakia rangi na vitu vingine vinavyoendana na hili. Kadhalika kwenye mavazi na hata vifaa vya kielektroniki, mpe mteja wigo wa kununua vitu vinavyoendana na kile anachotaka.

Njia ya tano ni kuongeza bei, hii ndiyo wengi huwa wanaikimbilia, lakini ukitumia hizo nne na hii kwa pamoja, utanufaika sana. kwenye njia ya tano, unaongeza bei ya kitu ili upate faida zaidi. Kama utafanyia kazi hatua hizi tano kwa pamoja, ongezeko dogo, kama la asilimia 10 kwenye kila hatua, litaleta ongezeko la asilimia 61 kwenye faida.

GHARAMA ZA KUPATA WATEJA WA BIASHARA YAKO.

Kuna aina mbili za gharama ya kupata wateja wa biashara yako.

Aina ya kwanza ni GHARAMA ZINAZORUHUSIWA za kupata mteja. Hapa unatumia gharama ambazo mteja akinunua mara moja basi gharama ile inarudi. Chukua mfano umetengeneza tangazo ambalo limekugharimu tsh 100,000/= na tangazo hilo limewafikia watu 1000. Katika hao 1000 ndiyo wamenunua. Na kwa kila unayenunua unapata faida ya shilingi elfu moja. Inamaana kwa watu 100, faida unayopata ni tsh 100,000/= sawa sawa na gharama ulizoingia kutoa tangazo. Hivyo hiyo ni gharama inayoruhusiwa ya kupata mteja. Kama utaandaa tangazo kwa gharama kubwa kuliko faida unayopata, hiyo sasa siyo GHARAMA INAYORUHUSIWA kupata wateja.

Aina ya pili ni GHARAMA UWEKEZAJI KWA WATEJA. Hapa unatumia gharama kubwa, ambayo inakuletea wateja, lakini manunuzi ya mwanzo ya mteja hayalipi gharama hiyo. Lakini kwa kuwa mteja ataendelea kununua, basi huko mbeleni ile gharama inarudi. Hivyo hapa unakuwa umewekeza kwa mteja, ukijua kwamba atafanya biashara na wewe kwa muda mrefu na gharama zako zitarudi.

Kwa biashara ndogo, ni vyema kutumia gharama zinazoruhusiwa, kwa biashara kubwa, ambazo zina rasilimali nyingi, zinaweza kuwekeza kwa wateja na baadaye zikanufaika zaidi. Usikimbilie kununua wateja kabla hujajua ni gharama kiasi gani unaingia na kama zinalipwa na idadi ya wateja watakaonunua.

MAENEO MATATU YA BIASHARA KUWEKA MKAZO.

Ili biashara yako ifanikiwe, inahitaji kuweka mkazo kwenye maeneo haya matatu muhimu sana.

Eneo la kwanza; THAMANI YA MAISHA YA MTEJA. Wafanyabiashara wengi huwa wanamwangalia mteja kwa wakati ule anaokuja kununua tu. Huwa hawaangalii thamani yake ya maisha. Kwa mfano kama mteja akija kununua kwako mara moja, unapata faida ya shilingi elfu moja, ni rahisi kuona elfu moja inakuja. Lakini chukua mfano kwamba mteja huyo ananunua kila wiki, na anaweza kununua kwako kwa miaka mitano ijayo. Hii ina maana kwa mwaka, anakuingizia faida ya 1000 x 52(idadi ya wiki za mwaka) ambayo ni tsh 52,000/= na kwa miaka mitano; 5 x 52,000/= ambayo ni sawa na 260,000/=. Thamani ya maisha ya mteja wako huyo ni shilingi laki mbili na elfu sitini, na siyo ile elfu moja unayoiona anapokuja. Je kwa kujua hilo hutaongeza umakini zaidi kwa mteja huyu ili aendelee kuwa na wewe kwa miaka hiyo mitano na hata zaidi?

Eneo la pili; GHARAMA YA KUMPATA MTEJA. Hapa ndipo gharama za kununua wateja wa biashara yako zinapoingia. Kabla hujachukua hatua yoyote ya kuongeza wateja zaidi kwenye biashara yako, lazima ujiulize gharama unayotumia inaleta wateja wangapi na kama gharama hizo zinarudi kupitia mauzo. Upo usemi kwenye utangazaji wa biashara kwamba nusu ya bajeti ya matangazo huwa inapotea, ila mtu hawezi kujua ni nusu ipi. Hii ina maana kwamba, gharama nyingi watu wanazotumia kutangaza biashara zao zinapotea, hazirudi kabisa kwenye biashara. Lazima ujue gharama zako na zinarudije.

Eneo la tatu; KIWANGO CHA WATEJA WAPYA WANAOPATIKANA. Unapotangaza biashara yako, watu wengi wanajua kuhusu uwepo wako. Lakini watu kujua kuhusu biashara yako hakukunufaishi chochote. Ni mpaka pale watu hao watakapochukua hatua ya kununua ndiyo biashara inanufaika, kama gharama zimepigwa vizuri. Hivyo eneo la kuweka mkazo ni kuongeza kiwango cha wanaojua biashara kuwa wateja wa biashara hiyo. kadiri watu wengi wanaofikiwa na tangazo wanakua wateja, ndivyo gharama za kupata wateja zinakuwa ndogo na faida inakuwa kubwa baadaye.

NJIA ZA KUONGEZA THAMANI YA MAISHA YA WATEJA WAKO.

Tumeshaona kwamba wateja wako wanapokaa na wewe kwa muda mrefu ndivyo unavyonufaika zaidi. Hivyo unahitaji kuweka juhudi kuhakikisha wateja wanabaki na wewe kwa muda mrefu. Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia ili wateja wakae na wewe kwa muda mrefu.

 1. Toa huduma bora sana kwa wateja wako, ambazo hawawezi kuzipata sehemu nyingine yoyote ila kwako tu.
 2. Kutengeneza mahusiano mazuri na wateja wako, wafanye wateja kuwa rafiki kwako na kwa biashara yako, waone siyo tu wanakuja kununua, bali wanakuja kwa rafiki yao, anayewajali na kuwapa kile kilicho sahihi kwao.
 3. Weka mbele maslahi ya wateja wako na siyo faida unayotaka kupata.
 4. Waelimishe wateja wako, washauri vizuri, hata kama utapoteza mauzo, lakini hilo litawajengea imani zaidi na hivyo kuendelea kununua zaidi.
 5. Wafanye wateja wako kuwa mashabiki wa biashara yako.

Zipo hatua saba ambazo wateja wanapitia mpaka kufikia ngazi ya ushabiki.

Hatua ya kwanza ni wapitaji tu, wanaisikia au kiona biashara yako lakini hawajawahi kuuliza chochote.

Hatua ya pili ni wateja tarajiwa, wamesikia na wamefuatilia kutaka kujua zaidi kuhusu biashara yako.

Hatua ya tatu ni wanunuaji, hapa wamejua, wakafuatilia na wakajaribu kununua kile unachouza.

Hatua ya nne ni wateja, hapa mtu amejaribu kununua kwa mara ya kwanza, na amerudi tena kununua. Mtu kununua mara moja haimfanyi kuwa mteja, na wala haikufanyi wewe kuwa mjanja. Ni mpaka mtu atakaporudi tena kununua ndiyo utajua umefanya kazi nzuri.

Hatua ya tano ni mwanachama, hapa mteja anakuwa mnunuaji wa mara kwa mara na unaweza kumpa manufaa ya kadiri anavyonunua. Labda akifika kiwango fulani anapata zawadi, au akinunua mara tano, ya sita anapata bure. Hapa mwanachama anakuwa na kielelezo cha kuonesha idadi ya manunuzi yake.

Hatua ya sita ni mtetezi wa biashara yako, hapa mteja anakuwa tayari kuwaambia watu wengine kuhusu biashara yako, anatoa shuhuda kwa wengine na hasiti kuwaalika wengi waje kununua.

Hatua ya saba ni shabiki kindakindaki, hawa ni wale wateja ambao hawaambiwi chochote kuhusu biashara yako, yaani wao wameshachukulia biashara yako kama sehemu ya maisha yako. Hawa ni wateja ambao wanaiongelea biashara yako muda wote, na wakikutana na mtu ambaye hanunui kwako wanaona anakosa kitu kikubwa sana.

Katika kuboresha thamani ya maisha ya wateja wako, kazana kuwapandisha wateja wako ngazi mpaka wafikie kiwango cha watetezi na mashabiki wa biashara yako.

WATEJA WA KUFUKUZA KWENYE BIASHARA YAKO.

Ili biashara yako ikue vizuri na uweze kupata faida, lazima ufukuze baadhi ya wateja.

Kwanza kabisa unahitaji kuwapanga wateja wako kwenye makundi A, B, C, na D.

Kundi A ni wale wateja ambao wanalipa fedha nyingi na siyo wasumbufu.

Kundi B ni wale wateja ambao wapo tayari kulipia, lakini siyo walipaji wa fedha nyingi, ila ni wateja wenye msimamo, ambao unaweza kwenda nao muda mrefu, na hawana usumbufu mkishakubaliana.

Kundi C ni wale wateja ambao wanataka punguzo kwenye kila kitu, na watakusumbua sana, wanaweza kununua kwa bei ya punguzo na bado wakarudi tena kulalamika kwamba haikuwa sawa kwao.

Kundi D ni wale wateja ambao ni matatizo kwa biashara yako, kwanza hawalipi kwa wakati, na kwenye kila kitu wanatafuta njia ya kubishana au kugombana. Hawa ni wateja ambao wanakuja wakiwa wamejipanga kukusumbua, ili wanufaike zaidi wao.

Ukishawagawa wateja wako kwenye makundi hayo manne, wahudumie vizuri wateja wa kundi A na B, na fukuza wateja wa kundi C na D, kwa sababu hawa ni wateja mabao hawana faida, na pia wanakuzuia usiwahudumie vizuri wateja wa kundi A na B.

Swali ni unawafukuzaje wateja hao?

Zipo njia mbili;

Ya kwanza ni kuwapa utaratibu mpya wa kufanya biashara na wewe, kwamba yale waliyozoea hayapo tena. Bei ni moja na haipungui na malipo ni kwanza na siyo baadaye. Kama hawawezi hilo wanaweza kwenda kwenye biashara nyingine.

Njia ya pili ni kuongeza bei ya bidhaa au huduma unayouza, na moja kwa moja watakimbia wenyewe.

Ukishaachana na wateja hao wasumbufu, nguvu zako peleka kwa wale wateja wazuri wa biashara yako.

Pia unapotangaza biashara yako, hakikisha unatumia lugha inayowavutia wateja wa kundi A na B, badala ya kundi C na D. Kwa mfano kama tangazo lako linasema kuna punguzo la bei au zawadi ya bure, utajikuta unavutia C na D wengi, maana ndiyo wanaopenda rahisi na bure.

NJIA ZA KUONGEA KIWANGO CHA WATEJA WAPYA.

Baada ya kutangaza biashara yako, utakuwa na watu wengi wanaojua kuhusu biashara yako, hawa ni wateja tarajiwa. Sasa unahitaji kuwabadili hawa na kuwa wateja halisi wa biashara yako. Kadiri unavyowageuza wengi kuwa wateja halisi, ndivyo gharama ya kuwapata inakuwa ndogo na ndivyo faida inakuwa kubwa kwako.

Kuongeza kiwango cha wateja wapya, fanya yafuatayo;

 1. Toa uhakika wa kile unachouza, mpe mteja uhakika kwamba kama anachonunua hakitafanya kazi basi anaweza kurudisha na akapata kitu kingine au akarudishiwa fedha zake.
 2. Tumia shuhuda za wateja walionunua kwako siku za nyuma na wakanufaika sana. shuhuda zina nguvu kubwa ya ushawishi.
 3. Kuwa na kitu cha tofauti ambacho kinapatikana kwako tu na mteja hawezi kukipata kwa wafanyabiashara wengine, na mweleze wazi kwamba atakipata kwako tu.
 4. Uza viti vya thamani kubwa, ambavyo upatikanaji wake siyo rahisi.
 5. Tengeneza mwonekano mzuri wa kile unachouza, ikiwa ni pamoja na unavyopakia kile unachouza. Mwonekano mzuri unaongeza mauzo.
 6. Weka majaribio ambapo mteja anaweza kujaribu kitu kabla hajakinunua.

Njia ambazo unapaswa kuziepuka sana kuwashawishi watu kununua ni kupunguza bei au kutoa zawadi zenye thamani kubwa. Kwa kufanya hivi utapunguza faida na pia utavutia wateja ambao baadaye watakuwa wasumbufu sana kwako.

Rafiki, hayo ni machache muhimu kati ya mengi yanayopatikana kwenye kitabu cha BUYING CUSTOMERS. Nimekushirikisha yale ambayo najua wewe rafiki yangu unaweza kuanza kufanyia kazi na biashara yako ikanufaika sana. Nenda kachukue hatua na pia pata muda usome kitabu hiki.

#2 MAKALA YA WIKI; HATUA NANE ZA KUTOKA CHINI MPAKA MAFANIKIO MAKUBWA.

Watu wengi wamekuwa na wasiwasi na hadithi nyingi za mafanikio, hasa pale wanapojaribu kuiga hadithi hizi wakashindwa. Pale mtu mwenye mafanikio anapohojiwa kwenye vyombo vya habari, au kuandika kitabu, na kueleza kwamba alianzia chini kabisa na amefikia mafanikio makubwa, wengi huwa na wasiwasi kwamba anayosema si kweli, kwa sababu wao wakijaribu kutumia njia hizo hizo hawafanikiwi.

Ukweli ni kwamba mafanikio siyo matokeo kama yanavyoshangiliwa na wengi, mafanikio ni mchakato, mchakato ambao unaweza kuwwa mrefu sana.

Juma hili nimekuandikia makala nzuri sana kuhusu mchakato wa mafanikio, ambapo nimekushirikisha hatua nane, ngumu sana za kutoka chini mpaka mafanikio makubwa. Kama unataka kufanikiwa, NI LAZIMA uzijue hatua hizi na uzifanyie kazi. Kama bado hujazijua, soma makala hii hapa; Hizi Ndiyo Hatua Nane (8) Za Kutoka Chini Kabisa Mpaka Kufikia Mafanikio Makubwa. Zijue Hapa Ili Uweze Kufanikiwa.

Pamoja na makala za kila siku, kuna makala nyingine nilikushirikisha juma hili kuhusu kanuni moja muhimu itakayokuwezesha wewe kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako. kama hukuisoma, isome hapa pia; Hii Ndiyo Kanuni Rahisi Itakayokuwezesha Wewe Kupata Chochote Unachotaka.

Kila siku naweka makala kwenye AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA, hivyo nikushauri sana rafiki yangu, kitu cha kwanza kufanya kwenye siku yako ni kuingia kwenye www.amkamtanzania.com ili uanze na mafunzo muhimu sana kwa mafanikio. Pia kwa wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, kila siku asubuhi ingia www.kisimachamaarifa.co.tz kuna makala tatu zinakuwa zinakusubiria wewe ujifunze na kuchukua hatua.

#3 TUONGEE PESA; JINSI YA KUONGEZA KIPATO CHAKO KILA MWEZI.

Rafiki, kwenye eneo la fedha, ukuaji unapimwa kwa ongezeko lako la kipato. Na ongezeko siyo la mwaka, bali la mwezi. Kila mwezi, inabidi kipato chako kiwe kinaongezeka.

Kama kipato chako kinabaki pale pale kila mwezi, kama ilivyo kwa waajiriwa na hata wafanyabiashara wengi, siyo kwamba unabaki pale pale, bali unarudi nyuma kwa upande wa kipato.

Kwa sababu kila siku gharama za maisha zinaongezeka, hivyo kipato kisipoongezeka, unazidi kurudi nyuma.

Njia pekee ya kuongeza kipato chako kila mwezi ni kutoa thamani zaidi kwa wengine. Kama upo kwenye biashara hilo ni rahisi, uzia wateja wengi zaidi kila mwezi, hata kupata mteja mmoja wa ziada kila mwezi ni hatua nzuri. Wauzie wateja ulionao zaidi kila mwezi, na pia ongeza bidhaa na huduma ambazo wateja wako wanahitaji pia.

Kwa walioajiriwa, pia unaweza kuongeza thamani zaidi kwenye kazi yako au nje ya kazi yako na ukaongeza kipato chako. Kama una utaalamu fulani, tumia utaalamu huo nje ya kazi yako kwa kutoa huduma za utaalamu huo. Unaweza kutoa huduma za ushauri kulingana na utaalamu ulionao na watu wakalipia msaada ambao unakuwa umewapatia.

Chochote unachofanya, hakikisha kila mwezi kipato chako kinaongezeka zaidi. Na hivyo ni muhimu kila mwezi ukapiga hesabu za kujua kipato chako ni kiasi gani.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; KWA NINI HUWEZI KUPATA USHAURI WANGU KIRAHISI KAMA UNAVYOTAKA.

Rafiki, kadiri ninavyoweka juhudi kwenye kutoa maarifa zaidi, ndivyo watu wengi zaidi wanavyotaka kupata ushauri kwangu. Kitu ambacho wanakuja kugundua hakiwezekani na mwishowe wananilaumu kwa nini siwapi ushauri.

Rafiki, nikuambie kitu kimoja, umekuwa na tatizo kwa miaka ziadi ya kumi, labda ni ndoa yako haifanyi kazi, au upo kwenye madeni, au biashara haikui, kwa miaka kumi umejitengeneza kufika hapo ulipo sasa. Halafu unataka unielezee tatizo lako kwa dakika tano au kumi, halafu nikupe ushauri ndani ya dakika tano na maisha yako yabadilike mara moja?

Ingekuwa hivyo wala usingefika kwangu, ungekua umeshatatua kila tatizo ulilonalo siku nyingi sana. Siyo rahisi ndiyo maana umetafuta sana kwenye mtandao mpaka ukakutana na mimi. Sasa unapokutana na mimi, sikudanganyi kwamba nina muujiza wa kufuta matatizo yako yote kwa ushauri wa mara moja. Bali nahitaji kukaa na wewe kwa angalau mwaka mmoja, nikikushirikisha maarifa kila siku, ambayo yataanza kubadili mtazamo wako, yatakujengea msingi unaoishi, utajijengea nidhamu na utaanza kuchukua hatua. Ni ndani ya mwaka, kwa kuweka juhudi ndiyo unaanza kuona mabadiliko kwenye maisha yako.

Na hii ndiyo sababu nilianzisha KISIMA CHA MAARIFA, na ada kuwa ya mwaka. Uamue kuingia gharama ya kukaa na mimi kwa mwaka mmoja, ukijifunza, ukipata nafasi ya kuuliza chochote, na mwisho wa mwaka ufanye tathmini, je kwa mwaka huu mmoja maisha yangu yamekuwa tofauti na miaka ya nyuma. Kama yamekuwa tofauti tunafurahia kwa pamoja, kama yamezidi kuwa mabaya basi nakupa ruhusa ya kudai ada yako na unaendelea na maisha yako.

Hivyo rafiki yangu, kama unahitaji ushauri wangu, jua kwanza lazima uwe kwenye KISIMA CHA MAARIFA, nje ya hapo tutapotezeana tu muda, ni bora muda huo nikautumia kuandaa mafunzo bora kwa wale ambao wanajaribu kuchukua hatua wenyewe. Lakini kama utataka mkono wangu uingie kwenye maisha yako, unapaswa kuwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Kwa sababu chochote nitakachokushauri, nitafuatilia kuona kama unakifanyia kazi kweli.

Karibu sana ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA kama bado hujajiunga. Tuma ujumbe kwa wasap namba 0717396253 wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA na nitakutumia maelekezo ya kujiunga.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KAMA HUJISIKII VIZURI NI TATIZO LAKO.

‘Be miserable. Or motivate yourself. Whatever has to be done, it’s always

your choice.’ – Wayne Dyer

kama unajisikia vibaya, hilo ni tatizo lako ninafsi. Wala usitafute mtu wa kumlaumu, hakuna anayeharibu siku yako ila wewe mwenyewe. Hakuna anayeharibu maisha yako ila wewe mwenyewe. Wewe ndiye unayechagua ufikirie nini, usikilize nini, uangalie nini, uambatane na nani na ufanye nini.

Sasa kama unachagua kufikiria vitu vinavyokufanya ujisikie vibaya, unataka kumlaumu nani? Kama umechagua mwenyewe kusikiliza na kuangalia habari hasi, halafu unajisikia kukata tamaa na maisha, unataka kumlaumu nani? Kama umechagua kukaa na watu ambao hawana wanakoelekea, watu waliokata tamaa na maisha yao, na wewe unaanza kuona maisha yako hayana maana, unafikiri nani wa kulaumiwa?

Kama unajisikia vibaya, umekata tamaa na maisha au unakosa hamasa ya kuchukua hatua, anza kuangalia maamuzi uliyofanya kwenye maisha yako, na utaona jinsi yale uliyochagua wewe mwenyewe yanakuweka kwenye hali hiyo.

Na uzuri ni kwamba wewe ndiye unayechagua, hivyo usijaribu kumlaumu yeyote. Kama hupendi pale ulipo sasa badili kitu, wewe siyo mti kwamba lazima uendelee kuwa hapo ulipo sasa.

Rafiki, kama nilivyokuambia mwanzo wa makala hii, pangilia juma linalokuja leo, ili linapoanza uwe na hatua za kuchukua. Nakutakia kila la kheri, uwe na juma bora sana na ukayaweke kwenye vitendo yale niliyokushirikisha kwenye hizi TANO ZA JUMA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu

Usomaji