Mwandishi George Bernard Shaw amewahi kuandika; mtu wa kawaida anaenda kama dunia inavyotaka. Mtu asiye wa kawaida, anaifanya dunia iende kama anavyotaka yeye. Hivyo maendeleo yote duniani yanategemea mtu asiye wa kawaida.
Kauli hii ina ukweli mkubwa sana, kwa sababu ni kweli maendeleo yote tunayofurahia duniani leo, yameletwa na watu ambao hawakukubali kuipokea dunia kama ilivyo.
Angalia kuanzia utengenezaji wa magari, treni, ndege, ujio wa teknolojia za kompyuta, intaneti na hata mitandao ya kijamii. Kabla ya kuja kwa vitu hivi, watu walikuwa wamesharidhika na njia za zamani za kuendesha maisha yao. Na walijua hakuna namna wanaweza kubadili hilo.
Lakini wakaja watu ambao walikataa hilo, watu waliojua wanaweza kufanya tofauti na ilivyozoeleka. Lakini watu hao hawakuenda salama, hawakuachwa wafanye kile wanachotaka. Bali walipingwa, kukatishwa tamaa na hata kuzuiwa, kwa sababu wengi waliamini watu hao wamechanganyikiwa au akili zao hazifanyi kazi sawasawa.
Ni ung’ang’anizi wa watu ambao walionekana siyo wa kawaida ndiyo umeifikisha dunia hapa tulipofika sasa. Hii ina maana kwamba, ili dunia itoke hapa ilipo na kwenda mbele zaidi, lazima kati yetu pawe na watu wasio wa kawaida, watu wanaotaka kuifanya dunia iwe kama wanavyotaka wao.
Je wewe umechagua upande upi, upande wa kuendelea kufanya kile ambacho tayari kinajulikana na hakuna wa kukusumbua, au upande wa kufanya vitu vipya, ambavyo havijazoeleka na watu watakuchukulia kama mtu usiye wa kawaida?
Sikia rafiki, usiogope kuonekana siyo wa kawaida, kwa sababu maendeleo ya dunia yanategemea watu wasio wa kawaida. Hivyo jitoe kuwa mmoja wa wale watakaoifanya dunia kuwa bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,