Wapo watu wengi wameingia kwenye biashara wakifikiri ni fursa bora kumbe ni kitu cha msimu, kitu ambacho kinapita.
Wapo wengine ambao wamebadili sana biashara zao wakijua mambo yamebadilika kumbe ni msimu tu wa kupita.
Kabla hujafanya maamuzi muhimu kwenye biashara yako, kwanza angalia kinachokusukuma kufanya maamuzi. Je ni kitu cha kudumu na kisichobadilika au ni kitu cha kupita?
Kwenye biashara, unahitaji kuweka mkazo kwenye vitu visivyobadilika, au kama vinabadilika basi isiwe kwa haraka sana.
Kwa sababu moja ya vitu vitakavyokusaidia kufanikiwa kwenye biashara ni msimamo wako. Wateja wanakuamini na kuja kwako kwa sababu ya msimamo wako. Kwa sababu wanajua wakija kwako watapata kile wanachotaka. Lakini kama hawana uhakika wakija kwako watapata wanachotaka, hawatajisumbua kuja.
Muhimu sana ujijengee msimamo fulani kwa wateja wako kupitia bidhaa na huduma unazouza. Na achana na mambo mengi ya msimu yanayokuja na kupita. Usiwe na tamaa za kupata fedha za haraka, tamaa za aina hii zimewaponza wengi na kujikuta wanaharibu kabisa biashara zao.
Kitu ambacho hakitabadilika kwenye biashara yako, ambacho unapaswa kukiwekea mkazo mkubwa ni matatizo au mahitaji ya mteja wako. Hicho ndiyo kitu unachopaswa kukitumia katika kufanya maamuzi muhimu ya biashara yako.
Kila unapokutana na kitu unachoona kwamba ni fursa bora kwako, jiulize je fursa hiyo inakusaidiaje kuwahudumia wateja wako vizuri, inawasaidiaje wateja wako kuondokana na matatizo yao au kutimiza mahitaji yao? Kama ina msaada itumie, kama haina msaada achana nayo.
Ukitumia msimamo huu, utaepuka na ile hali ya kuhangaika na biashara nyingi kwa wakati mmoja, kitu ambacho kinakuchosha na kukuzuia wewe kukuza biashara yako. Chagua wateja ambao unajua changamoto zao na mahitaji yao, na tengeneza biashara unayotatua matatizo au kutimiza mahitaji hayo. Kinachofuata baada ya hapo ni msimamo wako kwenye kuendesha biashara yako na kuepuka kuvutwa na kila aina ya fursa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,