Wafanyabiashara ndiyo tunaoharibu biashara zetu wenyewe, kwa sababu tunashindwa kutengeneza uaminifu kwenye biashara zetu.

Mtu akija kwenye biashara yako, atauliza punguzo la bei, kwa sababu anajua na wewe utakuwa umeweka bei ya juu ili ukiulizwa punguzo uuze kwa bei unayotaka kuuza.

Sasa hii ni njia ya hovyo sana ya kuendesha biashara, ni njia ya kudanganyana, njia ya kuviziana na njia ambayo huwezi kutengeneza imani ya wateja kwako.

Ukishakuwa mtu wa kuongeza na kupunguza bei kwa sababu mteja anataka hivyo, nao wateja wanajifunza kwamba kwako hakuna bei maalumu. Hivyo hata akija kununua na ukampunguzia, ataondoka akiamini angekomaa zaidi ungepunguza tena.

Kama umewahi kufanya manunuzi kwenye maduka makubwa (supermarkets) bei umewekewa kwenye kitu na ukichukua maana yake umekubaliana na bei, hakuna nipunguzie hapa kidogo. Kama umewahi kupata huduma kwenye hoteli kubwa, bei zipo juu na unalipa, huanzi kuomba punguzo. Kwenye maeneo hayo huombi punguzo kwa sababu unajua hizo ndiyo bei zilizopangwa, na utapata huduma bora kwa kulipa bei hizo.

Hii ndiyo imani unayopaswa kuijenga kwenye biashara yako kwenye upande wa bei. Pale mteja anapotaka punguzo, na kukupa sababu kwamba wengine wote wanapunguza, mweleze kwamba wewe unatoa bei moja, na unatoa huduma ambazo hataweza kuzipata huko kwingine. Na kama atakuwa tayari kunufaika na huduma zako, awe tayari kulipia.

Ukiendesha biashara yako kwa viwango hivyo na uwazi huo, wapo wateja ambao watafurahia sana kununua kwako hata kama wanalipa zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha