Kama huna furaha kwenye maisha yako, kama hufurahii jinsi maisha yako yanavyokwenda, hilo ni jukumu lako, pokea jukumu hilo, chukua hatua na songa mbele.

Kama kuna matokeo ya tofauti uliyoyapata kwenye maisha yako, matokeo ambayo siyo uliyotegemea, hilo ni jukumu lako, pokea matokeo hayo, chukua hatua sahihi na songa mbele.

Kama hufurahii kipato unachopata sasa, ambacho ni kidogo na hakitoshelezi, hilo ni jukumu lako, lipokee na chukua hatua sahihi ili kuweza kuongeza kipato chako.

Kama kuna watu huwapendi kwenye maisha yako, hilo ni jukumu lako, chukua hatua kwenye yale mambo yanayokufanya usiwapende wengine na uweze kuwa bora zaidi. Kwa sababu yeyote unayemchukia tatizo siyo lake, tatizo ni wewe mwenye chuki.

Kama hupendi pale ulipo sasa, kama ungependa kupiga hatua zaidi na kwenda mbele zaidi, hilo ni jukumu lako, chukua hatua kuelekea unakotaka kufika.

Kama umejaribu ukashindwa, kama umekutana na changamoto kubwa kwenye maisha yako na unakaribia kukata tamaa, hilo ni jukumu lako, chukua hatua sahihi ili uweze kuvuka changamoto hiyo na maisha yaendelee.

Hatua ya kwanza ya kwenda kwenye mafanikio makubwa, hatua ya kwanza ya kupata kile unachotaka kwenye maisha yako, ni kukubali kila kinachotokea kwenye maisha yako kama jukumu lako na kuanza kuchukua hatua ili kufika unakotaka kufika.

Hapa inabidi usahau kabisa nini watu wengine wamekufanyia, nini serikali imefanya au haijafanya, nini wazazi wamefanya au hawakufanya, nini wengine wamefanya au hawakufanya.

Unahitaji kubeba jukumu la maisha yako wewe, na kisha kuchukua hatua za kurekebisha yale ambayo huyataki kwenye maisha yako. Hii ndiyo njia pekee ya kuondoka pale ulipo sasa na kufika mbali zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha