“We must all wage an intense, lifelong battle against the constant downward pull. If we relax, the bugs and weeds of negativity will move into the garden and take away everything of value.” —Jim Rohn
AMKA Mwanamafanikio,
AMKA kwenye siku hii nyingine nzuri sana ya leo,
Siku ambayo tumepata nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari NGUVU INAYOKUVUTA CHINI…
Popote ulipo, ipo nguvu inayokuvuta chini, ipo nguvu inayohakikisha huendi mbele zaidi, ipo nguvu inayohakikisha unaanguka kabisa.
Bila ya kuweka juhudi mara zote kuivuka nguvu hiyo, huwezi kupiga hatua yoyote kwenye maisha yako.
Na hii ni kanuni ya asili kabisa,
Rusha kitu chochote kwenda juu, baada ya muda utakiona kinarudi chini, maana dunia ina nguvu ya mvutano, ya kutaka vitu vyote vizuri chini.
Bila ya kuwepo kwa nguvu inayofanya kitu kiendelee kwenda juu, inayozidi nguvu ya mvutano ya dunia, kitu hakitaenda mbali.
Lima shamba lako vizuri, liwe safi kabisa na panda mazao yako.
Baada ya muda utakuta magugu yameota sana.
Magugu haya yanarudisha mazao uliyopanda chini, yanahakikisha mazao hayakui ipaswavyo.
Ni lazima uendelee kuweka juhudi kupalilia mazao uliyopanda ili kuzuia magugu yasiyarudishe chini.
Kwenye maisha yako ya kila siku, kuna nguvu kubwa sana inayokuvuta chini, nguvu inayohakikisha hupigi hatua kubwa kwenye maisha yako.
Kuna wale wanaokuzunguka, wale wanaokuambia huwezi na utashindwa,
Kuna changamoto kwenye kila unachofanya,
Kuna uvivu binafsi wa kutokutaka kuumia sana na kazi,
Kuna hali ya kukosa hamasa na kukata tamaa,
Kuna wengine wanaoshindwa na kukukatisha tamaa,
Kuna mafanikio madogo yanayokufanya uridhike na uache kuweka juhudi za mwanzom na hapo unaanguka.
Unaona ni kwa jinsi gani nguvu zinazokuvuta chini zilivyo nyingi na kubwa.
Hii ina maana kwamba kama kila wakati huweki juhudi kuvuka nguvu hizo, huwezi kufanya makubwa na kupiga hatua kwenye maisha yako.
Utaendelea kuwa chini, hata ukipanda kidogo utaanguka tena.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuweka juhudi ili kuzivuka nguvu zinazokuvuta chini.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha