Rafiki, nimewahi kukuandikia kwamba, kama kuna kitu kikubwa unachotaka kufanya kwenye maisha yako, kitu ambacho hujawahi kufanya na wala wengine hawajawahi kufanya, dunia haitakuruhusu kabisa ukifanye. Hivyo kama utaomba kwanza ruhusa, ukubali mpaka uruhusiwe ndiyo ufanye, hutapata ruhusa unayotaka, na hivyo hutaweza kufanya unachotaka.
Badala yake, nilikuambia usiombe ruhusa, badala yake fanya, kisha omba msamaha baadaye. Chochote unachotaka kufanya, ambacho ni kikubwa, na ni kitu sahihi kwako kufanya, na hakiendi kinyume na sheria, unahitaji kukifanya, na kama kuna mambo yataenda tofauti na ulivyotegemea, basi unayo nafasi ya kuomba msamaha.
Lakini mara nyingi, kama unachotaka kufanya kitafanikiwa, hutakuwa na haja ya kuomba msamaha, kwa sababu matokeo mazuri yatajieleza yenyewe, na watu wanapenda matokeo mazuri, bila ya kujali yamepatikanaje.
Lakini pale matokeo yanapokuja tofauti, ndiyo kila mtu atakuwa na cha kukuambia, watakuambia usingeweza, walijua utashindwa na watakuonesha ni kwa jinsi gani umewaumiza au kuwaangusha. Na hapa ndipo unapohitaji kuomba msamaha ili maisha yaendelee.
Hapa ndipo panawapa watu wengi hofu, wengi wanafikiria kwamba kama matokeo yatakuja tofauti, wakiomba msamaha hawatakubaliwa au hautapokelewa vizuri. Lakini ukweli ni kwamba, kama ukikosea msamaha hautapokelewa, basi jua kwa namna yoyote ile hakuna atakayekupa ruhusa. Hivyo hilo linakuacha na kitu kimoja pekee, kufanya.
Kwa sababu kama utafikiria ruhusa hupewi, na msamaha pia hutapewa, hutaweza kupiga hatua yoyote kubwa kwenye maisha yako. Wewe fanya na kama matokeo yatakuwa mazuri hutakuwa na haja ya kuongea, kwa sababu yatajieleza yenyewe. Na kama matokeo yatakuwa mabaya, utahitaji kuomba msamaha, na kama hautapokelewa basi shukuru kwamba umejaribu na unajua njia ipi haifanyi kazi na ipi sahihi kwako kutumia.
Nenda kafanye leo kile unachojua ni muhimu kwako kufanya, lakini unahofia kufanya kwa sababu hakuna anayekuruhusu kufanya. Jua dunia haitakuruhusu ufanye chochote cha tofauti. Hivyo kama ni kitu sahihi, fanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,