Watu wengi wamekuwa wanakwama kwenye kuanza.
Na kikubwa ambacho wengi wanasema kinawakwamisha ni kukosa kila wanachohitaji ili waweze kuanza.
Watu wengi wanafikiri hawawezi kuanza mpaka wawe na kila wanachokitaka.
Kitu ambacho hakiwezi kutokea kwa hali yoyote ile.
Ni vigumu sana kupata kila unachotaka, hasa mwanzoni.
Hivyo njia pekee ya kuanza, ni kutumia chochote ulichonacho wakati unapotaka kuanza.
Na uzuri ni kwamba, una kila unachotaka ili kuanza.
Iwe ni biashara, kazi, kujifunza, mahusiano au chochote, tayari una vitu vingi unavyoweza kuanza navyo.
Hapo ulipo, una watu, vitu na hata mazingira ambayo ukiweza kuyatumia vizuri, unaweza kuanza chochote unachotaka.
Na kadiri utakavyoendelea, ndivyo utakavyojifunza na hata kupata hamasa ya kuendelea zaidi.
Kitu kingine kizuri ni kwamba zama tunazoishi sasa, zimerahisisha sana kuanza chochote.
Kama unataka kuwa mwandishi, simu uliyonayo ni kifaa tosha kabisa kwenye kuandika chochote unachotaka kuandika. Kwa kuwa na blogu, au kutumia mitandao ya kijamii, unaweza kumfikia yeyote unayetaka kumfikia na ujumbe wako.
Kadhalika kwenye kuanza biashara, huhitaji kusubiri mpaka uwe na eneo la kufanyia biashara hiyo. Badala yake unaweza kuwa na huduma au bidhaa, kisha ukatumia mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii kama soko lako. Na hata bidhaa haihitaji kuwa yako, unaweza kuchukua bidhaa ya mtu mwingine na ukaiuza kwa faida. Hivyo unaweza kuingia kwenye biashara ukiwa huna eneo la biashara wala huna bidhaa yako mwenyewe.
Usikwame kwa kisingizio kwamba huna pa kuanzia au huna cha kuanza nacho. Anzia hapo ulipo na tumia kila ulichonacho kuweza kuanza. Ukishaanza, utajifunza mengi sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,