Rafiki yangu mpendwa,

Leo nataka nikupe sifa ya nguo moja, ambayo kwa wengi inaweza kuwa inavutia sana, lakini wewe kama rafiki yangu, sitakushauri uikimbilie nguo hii, kwa sababu ambazo nitazitoa baadaye.

Ipo nguo moja ambayo inawatosha watu wote, kila mtu anaweza kuivaa nguo hiyo na asiwe na shida yoyote. Ni nguo yenye rangi moja, na yenye ukubwa mmoja unaomwenea kila mtu. Pia nguo hii bei yake ni rahisi sana, hivyo yeyote anayeitaka anaipata kwa urahisi sana.

Nguo ya aina hii inashawishi sana kuinunua, kwa sababu kwanza ni rahisi, pili inamtosha kila mtu. Hivyo unaweza kununua moja na mkashirikiana wengi kuivaa.

Lakini unapokuja kuangalia upande wa pili wa nguo ya aina hiyo, ndiyo unastuka kwamba faida unazofikiria ni za juu juu sana. Kwanza ukubwa wa nguo hautaendana na kila mtu, kuna ambao itakuwa kubwa kwao, na kuna ambayo itakuwa ndogo kwao. Rangi pia haitaendana na kila mtu, kuna ambao itawafaa na kuna ambao haitawafaa. Na hata mtindo wa nguo hiyo, hautamfaa kila mtu, kuna watu utaendana nao, na wengine wengi hawataendana na mtindo huo.

KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO

Hivyo wazo lako zuri na la furaha, kwamba ukipata nguo hiyo moja inayowatosha watu wote linakosa mashiko. Ni mpaka pale unapokimbilia kupata nguo hiyo ndiyo unagundua kwamba haikufai, na hata kama ilikuwa bei rahisi, bado unakua umepoteza fedha ulizolipia kupata nguo hiyo, hata kama fedha zilikuwa kidogo.

Mambo mengi sana tunayofanya kwenye maisha yetu, yanafanana sana na mfano huu wa nguo niliokushirikisha.

Tunapoamua ni kazi au biashara gani tufanye, tunaangalia wengine wengi wanafanya nini, na kujiaminisha kwa kuwa wengi wanafanya basi kitakuwa kitu sahihi kwetu kufanya. Tunaingia na kufanya, na tunagundua ni kitu ambacho hakiendani na sisi kabisa, lakini sasa unakuwa umeshaweka nguvu na muda sana kwenye kuingia kwenye kitu hicho kiasi kwamba unaogopa kuondoka.

Tunapotafuta ushauri kwa ajili ya vitu tunavyotaka kufanya, huwa tunakimbilia kupata ushauri unaomfaa kila mtu, ule ushauri kwamba kama hali ipo hivi, fanya hivi. Lakini sasa wewe una vitu vya nyuma huko, ambavyo vimechangia sana pale ulipo sasa, ushauri huo rahisi unaopata hauwezi kukusaidia kabisa, tena wakati mwingine utazidi kukupoteza zaidi.

Rafiki, ninachotaka kukuambia hapa ni kwamba, hakuna kitu kimoja kinachowafaa wengine kinakufaa na wewe pia kama kilivyo. Kila kitu kinapaswa kubadilika kulingana na mtu na mtu.

Na hapa nitapenda niingie kwa undani zaidi kwenye eneo la ushauri.

Nimeona watu wengi sana wanalalamika kufanyia kazi ushauri ambao walipewa na ukawa madhara makubwa zaidi kwao. Lakini ukichunguza kwa undani kuhusu ushauri huo, unagundua kwamba ushauri waliofanyia kazi haukuwa ushauri ulioandaliwa kwa ajili yao binafsi. Bali ulikuwa ushauri ambao unatolewa kwa wengi, kwa jina jingine unaitwa ushauri wa bure.

SOMA; Mambo Matatu (3) Ya Kuzingatia Ili Kupata Ushauri Bora Utakaokuwezesha Kufikia Mafanikio Makubwa.

Ule ushauri ambao watu wanajitolea kukupa, wanaona kitu kwa nje, wanakupa ushauri na wewe unakimbilia kuchukua hatua. Haijalishi mtu ni mwerevu kiasi gani, haijalishi mtu ana mafanikio makubwa kiasi gani, kama amekuangalia tu kwa nje na kukupa ushauri, ukiufanyia kazi kuna nafasi kubwa ya kuumia zaidi.

Kama unataka kupata ushauri mzuri, lazima umweleze mtu kwa kina yale yaliyopo ndani yako. Hata kama ameshaona nje, anahitaji kujua ndani nini kinaendelea. Anahitaji kujua vitu gani vya ndani yako ambavyo vinakukwamisha, ili anapokushauri, ushauri huo uhusishe vya nje na vya ndani.

Na hapa ndipo panapokuwa na umuhimu mkubwa wa kuwa na KOCHA au MENTA ambaye anakufuatilia kwa karibu. Mtu huyu anakuwa anajua zaidi kuhusu wewe, na ushauri au mwongozo anaokupa, unakuwa unaendana na hali yako na siyo ushauri unaoendana na yale wengine wanafanya.

Unapokuwa na kocha au menta mzuri, anaweza kukushauri ufanye kitu ambacho ni tofauti na anachowashauri wengine wafanye. Kwa sababu anakuwa ameshaisoma hali yako na kujua kwamba njia pekee kwako ni kufanya kile ambacho hashauri wengine wafanye.

Kwenye maisha yako, epuka sana vitu vinavyomfaa kila mtu, epuka sana vitu ambavyo kila mtu anaweza kufanya, na pia epuka vitu ambavyo ni rahisi au bure.

Na inapokuja kwenye ushauri, ipo kauli kwamba gharama ya ushauri wa bure utaanza kuilipa pale utakapofanyia kazi ushauri huo.

Chagua kuwa na kocha au menta ambaye atakujua wewe kwa undani, ambaye hutamficha kitu chochote na ambaye atakupa ushauri au mwongozo kulingana na hali unayopitia wewe, na siyo kulingana na yale wanayofanya wengine.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu

Usomaji