Fikiria umeenda kwenye biashara, una shida ya kitu fulani, umeoneshwa kile pale, bei yake kiasi fulani. Unataka kujua zaidi kama kitakusaidia, muuzaji anakuambia hebu usinisumbue, kama unataka chukua kama hutaki acha. Utajisikiaje?

Najua utajisikia vibaya sana, na kwa kuwa sasa hivi wauzaji wa chochote unachotaka ni wengi, basi utaenda kwa wengine na utamsema mfanyabiashara huyo kwa kila unayemjua, kwa jinsi asivyojali.

Najua pia kama wewe ni mfanyabiashara, hutaweza kutoa kauli kama hizo kwa wateja wako. Kwa sababu unajua ni kauli mbaya ambazo zitakupotezea wateja wako.

Sasa japo husemi kauli hizo, lakini matendo yako unapokuwa na mteja wako, yanasema waziwazi kauli hizo, kwamba wewe siyo muhimu, hatujakuita hapa, utajua mwenyewe, acha kunipotezea muda n.k.

Kwa mfano pale mteja anapokuuliza kitu na wewe ukawa bize kwenye simu, hii ni kauli rahisi sana kwa mteja wako kwamba huku kwenye simu nina kitu muhimu zaidi kuliko wewe, hivyo subiri au kama huwezi ondoka.

Au mteja anapotaka kupata ufafanuzi fulani na unampa majibu ya mkato, majibu ambayo hayampi taarifa za kutosha, hapo unamwambia wazi kwamba huna muda wa kumwelezea kila kitu, hivyo kama atapata sehemu nyingine ya kuelezewa, aende.

Au pale mteja anaporudi akiwa na shida ya kile alichonunua, labda hakifanyi kazi vizuri au hakimfai na wewe ukamwambia nimeshakuuzia sihusiki tena, hapo unamwambia wazi kwamba ukinunua kwangu tusizoeane tena, ondoka na usirudi tena.

Vitendo vyetu vinaongea zaidi kuliko maneno yetu. Hivyo kuwa makini na kila unachofanya unapokuwa na mteja wa biashara yako. Mpe huduma bora, mpe umakini wa kutosha, msikilize, tatua tatizo lake na mkaribishe tena na tena kwenye biashara yako. Ni kitu rahisi kufanya lakini wengi hawapendi, kwa sababu hawataki kazi zaidi, wanataka mteja aje, anunue aondoke na wao waendelee kupoteza muda kwenye mambo mengine yasiyo hata muhimu kwao au kwa biashara zao.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha