Rafiki yangu mpendwa sana,

Kama kuna kipengele cha makala nyingi ninazoandika kila juma ambacho huwa nakisubiri kwa hamu, basi ni kipengele hiki cha #TANO ZA JUMA, kwa sababu ni makala ambazo nakupa mambo mengi kwa wakati mmoja, na yote yanakuwa na msaada mkubwa kwako kama utayafanyia kazi.

Nakushirikisha sindano tano muhimu sana ambazo ukizifanyia kazi kwenye juma linalofuata, utajishukuru sana baadaye, kuliko kulianza juma ukiwa huna mpango wote mkubwa.

Karibu kwenye TANO ZA JUMA LA 38 kwa mwaka huu 2018, kama kuna watu bado hawajastuka, nikukumbushe tu, zimebaki siku 99 ili mwaka huu 2018 uishe. Ndiyo, tulianza mwaka huu tukiwa na siku 365, lakini sasa zimebaki chini ya mia moja. Lakini usitaharuki kwa kuona mwaka unaisha na hujafanya chochote, bali chukua hatua sasa.

Na kama ambavyo nimekuwa nakusisitiza, mwaka ni kipimo cha muda cha kuangalia umepiga hatua kiasi gani. Lakini kipimo cha muda cha kuchukua hatua ni juma, siku saba ni nzuri kupangilia na kujipima kadiri unavyokwenda. Hivyo kwa majuma 14 yaliyosalia kwa mwaka huu 2018 unaweza kufanya makubwa kuliko uliyofanya kwa majuma 38 yaliyopita. Chukua hatua sasa na weka juhudi.

MASAA MAWILI YA ZIADA
Kama changamoto yako mpaka sasa ni muda, pata na usome kitabu hiki, kitakuwezesha kupangilia na kutumia muda wako vizuri.

Nikukaribishe kwenye tano za juma, ujifunze na kuchukua hatua, ili maisha yako yaweze kuwa bora sana.

#1 KITABU NILICHOSOMA; JINSI YA KUENDESHA NCHI.

Jinsi ya kuendesha nchi ni kitu ambacho kila mtu anaweza kusema na kushauri, lakini unapokuwa kiongozi, kuna mambo mengi sana unayohitaji kuyazingatia ili kuendesha nchi vizuri.

Changamoto za uongozi hazijaanza leo, zimeanza zaidi ya miaka 300 iliyopita, tangu enzi za utawala wa Roma, ambao ulipitia misukosuko mingi sana kiuongozi. Uongozi bora ndiyo ulioikuza Roma na kuifanya kuwa moja ya jamii zilizostaarabika mapema. Lakini pia uongozi mbovu ndiyo ulioiangusha Roma na kuipoteza kabisa.

Makosa ambayo yalifanywa na viongozi wa enzi hizo na kupelekea mataifa yao kuanguka, yamekuwa yanarudiwa mpaka zama hizi, na yamewaangusha viongozi wengi. Unaweza kujiuliza je ni kwamba viongozi wengi hawasomi historia au kujifunza? Lakini unapata jibu kwamba mtu kabla hajawa na madaraka na baada ya kuwa na madaraka ni watu wawili tofauti kabisa. Mtu mmoja aliwahi kuandika, madaraka yanawalevya watu. Na mwingine akasema huwezi kumjua mtu mpaka utakapompa madaraka makubwa.

Juma hili nilipata nafasi ya kusoma kitabu kifupi sana kinachoitwa HOW TO RUN A COUNTRY, mwongozo wa uongozi kutoka kwenye kazi za aliyekuwa kiongozi na mwanasiasa wa enzi za utawala wa Roma Marcus Tullius Cicero. Cicero alipata nafasi ya kuwa kiongozi wa juu kwenye serikali ya Roma, na baadaye kubaki kuwa mwanasiasa, ambaye alipinga sana utawala wa mabavu, kitu ambacho kilipelekea ahukumiwe kifo.

Na hata wakati anahukumiwa kifo, alisema wazi kwamba yupo tayari kufa kusimamia kile alichoamini, ambacho ni serikali ya watu na siyo serikali ya mtu mmoja au kikundi cha watu. Kwa sababu Cicero anasema, hakuna serikali hatari kama ile inayoongozwa na maamuzi ya mtu mmoja au kikundi kidogo cha watu, hata iwe na nia njema kiasi gani, baadaye hubadilika na kuwa udhalimu mkubwa.

Cicero anatuambia kuna serikali za aina tatu,

Ya kwanza ni serikali ya kifalme, ambapo mtu mmoja anatawala nchi.

Ya pili ni serikali ya kitabaka, ambapo kunakuwa na tabaka linalotawala na tabaka linalotawaliwa.

Ya tatu ni serikali ya kidemokrasia ambapo watu wote wanashiriki kwenye maamuzi ya uongozi.

Cicero anatuambia, katika aina hizi za serikali, hakuna hata moja iliyo bora, maana zote zinaweza kubadilika na kuwa kitu kibaya sana.

Anasema ufalme unaweza kugeuka na kuwa udikteta,

Tabaka linalotawala linaweza kubadilika na kuwa tabaka la unyonyaji

Na demokrasia inaweza kugeuka kuwa machafuko pale kikundi fulani cha watu kinapotaka maamuzi yao yafanyiwe kazi.

Hivyo Cicero alipigania sana uwepo wa serikali ambayo itajumuisha aina hizo tatu za serikali, ambayo ni Jamhuri, ikiwa na maana kwamba ni mali ya wananchi. Hapo kunakuwa na kiongozi mkuu, ambaye anasaidiana na viongozi wengine, na wananchi ndiyo wanaochagua uongozi na kudhibiti uongozi huo.

MAMBO KUMI YA KUZINGATIA ILI KUENDESHA NCHI VIZURI.

Kupitia kazi za Cicero, tunapata mambo kumi ambayo anashauri viongozi wazingatie ili kuendesha nchi zao vizuri.

Kabla hujasema wewe siyo kiongozi wa nchi, nikuambie tu, wewe ni kiongozi wako binafsi, ni kiongozi wa familia yako, ni kiongozi wa biashara zako na pia ni kiongozi kwenye eneo lako la kazi. Hivyo mambo haya kumi yatakusaidia sana kwenye maisha yako, hata kama siyo kiongozi wa nchi.

Karibu tujifunze mambo haya kumi na jinsi ya kuyatumia kwenye maisha yetu ili tuweze kuwa na maisha bora na mahusiano mazuri na wengine pia.

Moja; Fuata sheria za asili.

Cicero anatuambia zipo sheria za asili ambazo zinaongoza maisha ya kila kiumbe hapa duniani. Kiongozi yeyote anayetaka kuongoza vizuri, lazima aweze kufuata sheria hizo za asili.

Sehemu ya sheria hizo za asili ni kwamba watu wote ni sawa, kila mtu anastahili kupata haki, kila mtu ana uhuru wa kuishi na kufanya maamuzi yake, na pia kila mtu anayo haki ya kuwa na furaha kwenye maisha yake.

Kama kiongozi, lazima uhakikishe watu wako wana uhuru huo wa maisha, tofauti na hapo uongozi utakuwa mgumu.

Mbili; Kuwa na mgawanyo wa madaraka.

Kila serikali inapaswa kuwa na mgawanyo wa madaraka, na pia kiongozi kuwa na njia ya kuhojiwa na kudhibitiwa asije kugeuka na kuwa kiongozi mbaya.

Cicero aliona jinsi ambavyo viongozi wengi wanaanza na nia nzuri, na watu wanawaamini sana, wanaacha kuwahoji na kuwadhibiti, na kinachotokea viongozi au wanabadilika na kuwa madikteta na watawala wabaya sana.

Lazima iwepo njia ya kukufanya wewe kama kiongozi uweze kuhijiwa na kudhibitiwa, ili kuepuka madhaifu yako ya kibinadamu kuharibu uongozi wako,

Tatu; Kuwa na tabia njema na uadilifu wa hali ya juu sana.

Cicero anatuambia kitu pekee kitakachomwezesha kiongozi kuwa bora ni tabia njema, na kitakachomwezesha kuendelea kuwa kiongozi bora ni uadilifu wa hali ya juu sana.

Anatuambia kama kiongozi, maslahi ya nchi yako yanapaswa kuwa juu ya maslahi binafsi. Pale kiongozi anapoanza kujali maslahi yake kwanza, ndipo ufisadi unapoanzia na uongozi kuwa mbaya sana.

Cicero anasema kama kiongozi, hupaswi hata kutiliwa shaka juu ya tabia zako au uadilifu wako. Watu watakuamini zaidi pale unapokuwa na tabia njema na uadilifu wa hali ya juu.

Nne; waweke marafiki karibu, na maadui karibu zaidi.

Cicero anatuambia moja ya udhaifu wa kiuongozi ni watu kuwachukulia poa marafiki zao, na kuwapuuza maadui wao. Unahitaji kuwaangalia kwa karibu sana marafiki zako, maana hao ndiyo wanaoweza kuwa wabaya sana kwa uongozi wako, hasa pale wanapokosa walichotegemea.

Pia anatuambia tuwe makini na maadui zetu, tujue kila wanachofanya ili lisitokee lolote la kutushangaza.

Cicero anasisitiza pia umuhimu wa kushirikiana na wale ambao wanapingana na uongozi wetu, kwa sababu kupitia wao tunajifunza njia za kuwa bora zaidi.

Tano; Akili na ujuzi

Cicero anasema wale wanaoongoza, wanapaswa kuwa na akili sana. Anasema lazima kiongozi awe mjuzi wa mambo, na kadiri kiongozi anavyojua, ndivyo watu wanamwamini na kumheshimu.

Cicero anasema kiongozi asiyekuwa na ujuzi wa kutosha kwenye chochote anachoongelea, hotuba zao zinakuwa za maneno matupu na matendo yao yanakuwa hatari sana.

Sita; Maelewano ni njia ya kuweza kufikia muafaka.

Cicero anasema kwenye uongozi, kuna wakati utahitaji kukubaliana na yale usiyokubaliana nayo ili tu kufikia muafaka. Anasema kama kiongozi hupaswi kuwa na misimamo isiyoyumba, kwa kufanya hivyo utasababisha matatizo hata kwenye mambo madogo.

Cicero anasema kama kiongozi usibadili maono yako, bali badili njia ya kufika pale. Hivyo kama ipo njia ya kufika pale, ambayo ni sahihi lakini ulijiambia hutaipita, na ndiyo njia pekee iliyopo kwa wakati huo, weka pembeni majigambo yako na fanya kile kinachopaswa kufanywa.

Kama kiongozi kuna wakati utajikuta unalazimika kufanya vitu ambavyo ulijiahidi hutafanya kabisa. Lakini uongozi una changamoto, lazima nyakati nyingine ulegeze msimamo ili mambo yaweze kwenda.

Saba; Usiongeze kodi, labda kama ni lazima sana.

Cicero anasema hakuna kitu kinawachosha wananchi kama kodi. Na serikali nyingi zimekuwa zinapandisha kodi kila mara kwa sababu serikali zinakuwa kubwa na njia pekee ya serikali kupata fedha ni kukusanya kodi.

Cicero anashauri kama kiongozi, usipandishe kodi kila wakati, labda kama ni muhimu mno na wananchi wajue hivyo.

Pia Cicero anasema jukumu la serikali ni kuwawezesha wananchi wake kujipatia mali kadiri wawezavyo kisheria, na fikra za viongozi kwamba wachache wenye mali wanapaswa kunyang’anywa na kugaiwa wale wasiojiweza ni fikra inayorudisha maendeleo ya wengi nyuma. Kama wapo watu wanaoweza kujikusanyia mali kwa njia halali, kazi ya serikali ni kuwahakikishia mali zao hizo zinakuwa salama, na siyo kuchukua na kuwapa wasiokuwa nacho.

Nane; Uhamiaji unaifanya nchi kuwa imara.

Cicero anasisitiza umuhimu wa nchi kupokea wahamiaji kutoka maeneo mengine. Wahamiaji wanakuja na ujuzi mpya, uzoefu wa tofauti na hata utamaduni wa tofauti. Ukiangalia nchi nyingi zilizoendelea, ni zile zilizoruhusu wahamiaji kuingia. Na hata ndani ya nchi moja, kila eneo, utakuta wahamiaji kutoka mkoa mwingine wana mafanikio makubwa kuliko waliozaliwa eneo lile.

Tisa; Usianzishe vita isiyo na umuhimu.

Cicero anasema zipo sababu mbili pekee za nchi kuingia kwenye vita;

Moja ni kujitetea pale nchi inapokuwa imevamiwa, lazima nchi ipigane kuondoa uvamizi.

Mbili ni kulinda heshima ya nchi, pale ambapo nchi inakuwa inachezewa na watu wengine, inaweza kuingia kwenye vita kulinda heshima yake.

Sababu nyingine yoyote ya nchi kuingia kwenye vita siyo sahihi na italeta madhara kwenye uongozi na nchi kwa ujumla.

Kumi; Rushwa inaangamiza taifa.

Cicero anasema taifa lolote linaloanguka, anguko huwa linaanzia ndani na siyo nje. Na anguko linaanzia ndani pale viongozi wanapokuwa na tamaa, rushwa na udanganyifu. Anasema vitu hivyo vikishakuwa ndani ya serikali, inakuwa dhaifu kwa nje na rahisi kuangamia.

Kama kiongozi unapaswa kuhakikisha uongozi unakuwa wa uaminifu na uadilifu wa hali ya juu, na rushwa, tamaa, udanganyifu havipo kabisa katika uongozi. Wananchi wanakuwa na imani pale wanapogundua viongozi wao ni wasafi na waadilifu.

Rafiki, hayo ndiyo mambo kumi ya kuzingatia kwenye uongozi wowote unaoubeba, iwe ni wako binafsi, wa familia, wa kazi, wa biashara na hata wa nchi. Fanyia kazi mambo hayo kumi ili kuwa kiongozi bora kabisa na kufikia maono yako makubwa.

#2 MAKALA YA JUMA; AINA MBILI ZA AKAUNTI YA KIFEDHA KWAKO.

Watu wengi wamekuwa wanashangazwa na kitu kimoja, wakiwa na fedha wanakuwa na mipango mizuri sana, lakini wanapopata fedha nyingi, akili zao ni kama zinaacha kufanya kazi, na fedha zikiisha ndiyo akili zinawarudia.

Wengi wamekuwa hawaelewi hili kwa sababu hawajui kwamba kila mmoja wetu ana aina mbili za akaunti ya kifedha. Kuna akaunti ya benki na akaunti ya kisaikolojia. Sasa kama akaunti yako ya kisaikolojia haijakaa sawa, akaunti yako ya benki haitatulia kabisa.

Nimeeleza vizuri sana na kwa kina aina hizi mbili za akaunti kwenye makala ya juma hili, kama hukupata nafasi ya kuisoma unaweza kuisoma hapa; Aina Mbili Za Akaunti Za Kifedha Kwenye Maisha Yako Na Moja Inayokuzuia Usifikie Utajiri Mkubwa.

Pia juma hili nilieleza sifa za watu ambao hawapaswi kwa namna yoyote ile kukosa SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, kama bado hujafanya maamuzi ya ushiriki au usishiriki, soma hapa; Hawa Ndiyo Walengwa Wakuu Wa SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, Kama Ni Mmoja Wao Chukua Hatua Sasa.

Rafiki, kila siku kuna makala zinaenda hewani kwenye www.amkamtanzania.com na www.kisimachamaarifa.co.tz namaanisha kila siku, bila kuacha siku hata moja. Ninachotaka kwako rafiki yangu, uwe unaianza siku na kitu kizuri cha kufanyia kazi kupitia mitandao hiyo. Hivyo tenga ratiba yako kwamba kila unapoamka, cha kwanza ni kuingia kwenye AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA ili kujifunza.

#3 TUONGEE PESA; JILAZIMISHE KUISHIWA.

Kilio cha wengi kwenye fedha ni kwamba, wakipata fedha haikai na hata wakiweka akiba, haikai. Yaani wakipata fedha au wakiwa na akiba, matatizo ndiyo yanazaliwa, watu ndiyo wanapata shida na mahitaji ndiyo yanaongezeka. Ni mpaka fedha walizonazo ziishe ndiyo matatizo nayo yanatulia.

Nikuambie kitu kimoja rafiki, kama unapitia changamoto hiyo, kuna suluhisho moja ambalo ni zuri sana kwako. Suluhisho hilo ni kujilazimisha kuishiwa.

Iko hivi, ukiwa na fedha, akili yako inajua una fedha, hivyo ukikutana na chochote, hutaweza kuvumilia kama unayo fedha, utaitumia tu. Sasa unachohitaji, ni akili yako ijue kwamba huna fedha, hivyo unapokutana na tatizo, unalazimika kufikiria njia ya kulitatua na siyo kutumia fedha ulizonazo.

Katika kutumia dhana hii ya kujilazimisha kuishiwa, kwanza kuwa na bajeti yako ya kuendesha maisha. Kisha tenga kipato kinachokidhi bajeti hiyo. Kiasi kingine chote cha fedha kiweke kwenye akaunti maalumu ambayo huwezi kuondoa fedha hizo.

Pia kila fedha ya ziada unayopata, ambayo hukuwa nayo kwenye ratiba, usitoe hata senti, yote weka kwenye akaunti hiyo muhimu.

Hii itakusaidia uwe huna fedha kwa muda mwingi, na inapotokea changamoto inayokuhitaji uwe na fedha, itabidi utafute njia nyingine za kupata fedha hiyo na siyo kutoa zile ulizoweka akiba, kwa sababu umeweka sehemu ambayo huwezi kutoa.

Jilazimishe kuishiwa na utaweza kuweka akiba, kuwekeza na kukuza kipato chako zaidi.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; JE UMESHAANZA KULIPA ADA YA KUSHIRIKI SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018?

Rafiki yangu mpendwa, zimebaki siku 38, ambazo ni sawa na wiki tano ili kufikia tarehe ya mwisho ya kulipia ada ya kushiriki semina ya KISIMA CHA MAARIFA 2018. Mwisho wa kulipia semina hii ni tarehe 31/10/2018 na semina itafanyika tarehe 03/11/2018 jijini dar es salaam.

Nachukua nafasi hii kukukumbusha kwamba kama hujaanza kulipia semina hii, unapaswa kufanya hivyo kwa sababu siku zinakaribia sana. nilikupa taarifa hii kwa mara ya kwanza tukiw ana zaidi ya siku 120, sasa zimebaki chini ya siku 40.

Kumbuka nilikupa nafasi ya kulipa kidogo kidogo ili mpaka kufikia tarehe 31/10/2018 uwe umeshalipa ada ya kushiriki ambayo ni tsh 100,000/=

Lakini pia kama utalipa yote kwa pamoja, kumbuka kufanya hivyo mapema kabla ya muda kuisha.

Namba za kufanya malipo ni 0755 953 887 au 0717 396 253 majina ya namba hizo ni Amani Makirita.

Kama ndiyo kwa mara ya kwanza unapata taarifa hizi za semina, unaweza kupata maelezo zaidi ya semina hii hapa; Karibu Kwenye Semina Ya KISIMA CHA MAARIFA 2018; Mafanikio, Biashara Na Uhuru Wa Kifedha.

Rafiki yangu mpendwa, SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA ni tukio ambalo huwa linatokea mara moja tu kwa mwaka, ambapo tunakutana kwa pamoja na kujijengea msingi imara wa mafanikio tunaokwenda kuuishi mwaka mzima.

Siyo tukio la kukosa, kwa yeyote aliyejitoa maisha yake kwa ajili ya mafanikio makubwa, kwa yule anayejua anaweza kufanya zaidi ya pale alipo sasa. Karibu sana tuwe pamoja kwenye semina ya mwaka huu 2018, fanya malipo yako ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki semina hii.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; JINSI UNAVYOWEZA KUPATA CHOCHOTE UNACHOTAKA.

“You can have anything you want, if you want it badly enough. You can be anything you want to be, do anything you set out to accomplish if you hold to that desire with singleness of purpose.” – Abraham Lincoln

Dhana kwamba mtu yeyote anaweza kufanya chochote anachotaka kufanya, kupata chochote anachotaka na kufika popote anapotaka, imekuwa inaonekana ni kauli ya hamasa tu na isiyofanya kazi.

Lakini shahidi za wale waliotoka chini kabisa na kufika mafanikio ya juu, zinatuhakikishia kwamba dhana hii inafanya kazi vizuri sana.

Lakini itafanya kazi pale tu wewe utakapofanya kazi.

Na kazi unayohitaji kufanya ni moja; SHIKILIA HITAJI LAKO KWENYE KUSUDI LAKO KUBWA KWENYE MAISHA. Lazima uwe na kusudi kubwa kwenye maisha yako, kusudi ambalo umejitoa kulifikia kwa namna yoyote ile. Kisha shikilia hitaji lako kwenye kusudi hilo. Pasiwepo na chochote cha kukuyumbisha kuhusu kupata kile unachotaka. Na ukishaweka msimamo huo, dunia itakupisha upate unachotaka.

Lakini nikutahadharishe, haitakuwa rahisi, hutajisemea tu unaweza kupata chochote halafu ukaendesha maisha yako kama wengine wanavyoendesha ukitegemea kupata matokeo makubwa. Utakuwa unajidanganya wewe mwenyewe na utaishia kukata tamaa.

Unapojitoa kweli kupata unachotaka, lazima uwe tayari kuumia, lazima uwe tayari kuteseka, kutengwa, kuchekwa na kudharauliwa, lakini mwisho wa siku, utasimama kama mshindi.

Rafiki, nenda kalianze juma la 39 ukiwa na maamuzi ya nini unataka kukamilisha, na usikubali chochote kikuyumbishe kwenye kukamilisha ulichopanga. Pia nenda ukawe kiongozi bora zaidi na usisahau kulipa ada ili uweze kushiriki semina ya KISIMA CHA MAARIFA 2018.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu

Usomaji
Kama unapata changamoto kwenye usomaji wa vitabu, karibu ujiunge na kundi la KURASA KUMI ZA KITABU, uweze kujijengea nidhamu ya kusoma vitabu.