Kila kitu tunachofanya kwenye maisha yetu, kinaacha alama fulani kwetu na kwa wengine pia.

Hakuna chochote unachofanya ambacho kitafutika kabisa kwenye maisha yako. Wapo watakaoona kile unachofanya, na kuendelea kuwa na kumbukumbu yetu kupitia kile tunachofanya.

Sasa unapohitaji kujenga ukuu, unapohitaji kujenga umaarufu au sifa yako kwa wengine, kazana kufanya yale ambayo ni muhimu sana kwako, kile ambacho unakijali sana.

Hii ina maana kwamba, usikimbilie kufanya kila kitu ili uonekane na wewe upo, usikimbilie kuwaiga wengine ili uonekane upo kama wao.

Badala yake unahitaji kuchagua kufanya yale ambayo ni muhimu, yale ambayo kama unachofanya kitatangazwa moja kwa moja na vyombo vyote vya habari, basi utajivunia sana kwa unachofanya.

Lakini kama unachofanya hakipo kwenye hatua hiyo, hatua ya kuwa tayari kila mtu aone unachofanya, basi unapoteza muda wako. Na pia unatengeneza picha ambayo watu watashindwa kujua wakuaminije. Kwa sababu kuna wakati wanakuona unafanya vitu vizuri, wakati mwingine unafanya vitu vya hovyo.

Weka muda na nguvu zako kwenye kufanya yale ambayo unajali zaidi, yale ambayo unataka kila mtu ajue unafanya. Sasa watu watajua unafanya kwa wewe kufanya, na siyo kusema unafanya au kuigiza unafanya.

Kwa kifupi, jua vipaji vyako, jua uwezo wako, na jua kile unachotaka, kisha yatengeneze maisha yako kwenye nguzo hizo muhimu. Itakuchukua muda lakini utatengeneza sifa ambayo itakusaidia zaidi kuliko kuhangaika na vitu ambavyo haviendani na wewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha