Kinachowazuia watu wengi kupata kile wanachotaka, kupata mafanikio makubwa, ni muda uliopo kati ya wazo, kuamua na kuchukua hatua.

Watu wengi wanapata wazo, lakini inawachukua muda sana mpaka kufikia maamuzi na hata wakishafikia maamuzi, inawachukua muda sana mpaka kuanza kuchukua hatua.

Kadiri muda kati ya wazo na maamuzi unavyokuwa mrefu, ndivyo uwezekano wa kitu kutokufanyika unazidi kuwa mkubwa.

Kadiri muda kati ya maamuzi na kuchukua hatua unavyokuwa mkubwa, ndivyo inavyokuwa rahisi kugundua wengine wameshaanza kufanya.

Kuna mambo mengi sana kwenye maisha yako ambayo umekwama siyo kwa sababu unayojiambia, ila kwa sababu tu hutaki kufanya maamuzi au hutaki kuchukua hatua.

Kwenye mambo mengi unayojiambia umekwama, unachojiambia ni kwamba unahitaji muda zaidi. Lakini ukweli ni kwamba, huhitaji muda zaidi, unahitaji kufanya maamuzi sasa na kuchukua hatua.

Leo hii hebu pitia mambo yote ambayo una mawazo mazuri kisha jiulize kwa nini hujafanya. Utakachogundua ni kwamba hujafanya maamuzi, au umeshayafanya lakini hujaanza kutekeleza.

Fanya maamuzi leo na kama tayari ulishafanya maamuzi basi anza utekelezaji.

Chochote unachojiambia unasubiri unajidanganya, kwa sababu kama unajiambia unasubiri uwe na uhakika na usikosee, hakuna chochote unachoweza kuwa na uhakika nacho kwenye maisha yako, na mambo mengi mno utakosea.

Hivyo fanya maamuzi sasa na chukua hatua, na kama itakuwa umekosea, basi utafanya marekebisho, ambayo yanakuwa rahisi ukiwa umeshaanza.

Huhitaji muda zaidi, unahitaji kufanya maamuzi sasa na kuchukua hatua sasa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha