Kama unajiambia unataka kuingia kwenye biashara lakini hujui biashara gani ufanye, nina ushauri mmoja mzuri sana kwako. Uza kitu ambacho unapata shida ya kukipata.
Najua kwenye maisha yako kuna vitu unatafuta, ambavyo umekuwa hupati au hata ukipata siyo kwa namna ambavyo ulitaka kupata.
Habari njema ni kwamba, siyo wewe mwenyewe mwenye uhitaji wa vitu hivyo, wapo wengine wengi, lakini baada ya kugundua hawawezi kupata, basi wengi wanakuwa wamekata tamaa na kuendelea na maisha yako.
Hii ina maana kwamba, kama wewe utatatua mwenyewe kile unachokosa, na ukaweza kuwashirikisha wengine, utakuwa na wateja wengi wa kile unachofanya au kutoa.
Hivyo anza kuangalia kwenye yale mahitaji yako muhimu, yapi ambayo hupati au huyapati kwa viwango unavyotaka kupata. Kisha ona jinsi gani unaweza kutatua mahitaji hayo kwako binafsi na kuwashirikisha wengine pia.
Uzuri wa kuanza biashara ambayo wewe mwenyewe ndiyo mwenye uhitaji ni kwanza utapata unachotaka, pili utakuwa na ushuhuda mzuri kwa wateja wako na tatu hutakubali kushindwa kabisa kwenye biashara hiyo, kwa sababu biashara inakuwa sehemu ya maisha yako, hivyo hata kama utakutana na ugumu, utaendelea maana wewe mwenyewe una uhitaji mkubwa wa biashara hiyo.
Vitu vingi unavyotafuta, tayari vipo hapo ulipo, tayari unavyo ndani yako, na kimojawapo ni biashara bora kabisa kwako. Anza kuangalia ndani yako sasa na angalia mazingira yanayokuzunguka, una jawabu la biashara gani nzuri kwako kufanya. Anza kujitatulia mwenyewe matatizo yako na utaweza kuwatatulia wengine pia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,