Karibu kila falsafa na imani ya kidini inaeleza umuhimu wa kuishi wakati uliopo, umuhimu wa mtu kuishi sasa, kuwa pale alipo, kwa wakati aliopo.

Lakini sisi binadamu tuna uwezo mkubwa sana wa kuyaharibu maisha yetu bila ya kufanya chochote, bali kujitengenezea hofu ya vitu visivyokuwepo na ambavyo hatuwezi kuviathiri kwa wakati uliopo.

Huwa tunapenda kutumia muda wetu mwingi kufikiria mambo yaliyopita, ambayo hatuwezi tena kuyabadili na kuishia kuwa na majuto.

Pia tumekuwa tunapoteza muda mwingi kwa kufikiria kesho, ambayo bado haijafika na tunajitengenezea hofu kubwa kuhusu kesho hiyo.

Rafiki, hakuna kiwango chochote cha hofu unachoweza kuwa nacho leo ambacho kitakuwezesha wewe kutatua tatizo la kesho. Unaweza kuwa na hofu utakavyo, lakini jua kesho itakuwa pale pale, na tatizo la kesho utakutana nalo.

Hivyo kuhofia kuhusu kesho yako, ni kuipoteza leo, na kuiharibu zaidi kesho yako.

Kwa sababu maandalizi bora kabisa kwa kesho yako, ni kuishi vizuri leo. Kama leo utaishi vizuri, kama utafanya yale uliyopanga kufanya bila ya kuahirisha, kama utazingatia afya yako, malengo yako na mahusiano yako, kesho yako inakwenda kuwa bora sana.

Na kuhusu jana, yaliyopita huwezi kuyabadili, jifunze kisha songa mbele, usiendelee kurudia kila kilichopita kwa sababu utaishia kujiumiza na majuto na wakati huna namna ya kubadili chochote kilichopita.

Ishi leo, ishi kwenye wakati ulionao, ishi kwa ubora leo na kesho itakuwa bora kama ambavyo umeweza kuifanya leo kuwa bora.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha