Rafiki yangu mpendwa,

Tunaishi kwenye zama bora sana kuwahi kutokea hapa duniani. Ni zama ambazo ukomo umeondolewa kwenye vitu vingi. Mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii imefanya vitu vingi kuwa rahisi kwa watu wengi.

Kwa mfano mtu sasa hivi anaweza kuanzisha biashara ambayo ataiendesha kupitia mtandao wa intaneti na akafanikiwa sana. Uzuri ni kwamba biashara hiyo inaweza kuendeshwa moja kwa moja kwenye mtandao wa intaneti na hivyo mtu akaepuka gharama nyingi ambazo mtu anaingia kwenye kuendesha biashara kwa njia ya kawaida.

Mtu anapofanya biashara kwa njia ya mtandao wa intaneti, anaweza asihitaji kuwa na eneo la biashara, hivyo anaepuka gharama za kukodi eneo la biashara. Lakini pia hahitaji kuingia gharama kubwa kutangaza biashara yako, maana mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii imefanya kutangaza biashara kuwe rahisi sana. Kitu kikubwa sana kinachohitajika kwenye kufanya biashara kwa njia ya intaneti ni kuwepo kwa uaminifu baina ya mfanyabiashara na mteja.

KIPATO KWA BLOG

Zipo hatua sita muhimu sana kwa mtu kufuata ili kuweza kuanzisha biashara na kutengeneza kipato kupitia mtandao wa intaneti.

Hatua ya kwanza; amua ni bidhaa au huduma gani utakayotoa.

Hatua ya kwanza kabisa ni mtu kuamua ni bidhaa au huduma gani unategemea kutoa kwa wateja wako kwenye biashara yako ya mtandaoni.

Hapa unahitaji kuangalia ni kitu gani unaweza kukitoa vizuri sana kwa wateja wako na kuyafanya maisha yao kuwa bora.

Kama unapenda biashara yako iwe ya mtandaoni moja kwa moja, yaani haihusishi kukutana moja kwa moja na wateja, biashara ya huduma ni nzuri kuliko ya bidhaa. Kwa sababu bidhaa zina changamoto ya kuwekeza kwenye kuziandaa na pia kumfikishia mteja.

Lakini biashara ya huduma, kazi ipo mwanzoni kwenye kuandaa huduma, baada ya hapo unaendelea kunufaika na huduma uliyoiandaa mara moja.

Hatua ya pili; tengeneza tovuti au blogu yako.

Unapofanya biashara kwa kutumia mtandao wa intaneti, unahitaji kuwa na maskani yako huko mtandaoni. Lazima uwe na sehemu ambayo watu wakija wanakutana na taarifa zako na biashara yako pia. Tovuti au blogu yako ndiyo inaweza kuwa duka lako, ambapo watu wanatembelea na kuchagua ni kipi wanataka kununua kwako.

Zipo njia rahisi sana za kupata tovuti au blog bila ya kuingia gharama kubwa. Ingia www.wordpress.com au www.blogger.com na utaweza kutengeneza tovuti yako mwenyewe na kuanza. Kama unaweza kufungua email, basi pia unaweza kutengezeza tovuti au blogu kupitia mitandao hiyo miwili.

Hatua ya tatu; andaa ofa yako.

Chochote utakachotaka kuuza kupitia mtandao wa intaneti, unapaswa kujua kwamba kuna wengine wengi ambao wanauza pia. Hivyo unahitaji kuwa na kitu cha kuwavutia wateja kuja kwako.

Na hapa ndipo unapohitaji kuwa na ofa nzuri kwa wateja wako. Ninaposema ofa simaanishi kupunguza bei au kutoa bure, badala yake kuweka bidhaa au huduma zako kwa namba ambayo mteja atanufaika zaidi akinunua kwako na siyo kwa wengine.

Weka pamoja bidhaa au huduma unazotoa kwa namna ambayo mteja akinunua atanufaika zaidi. Jinsi unavyopakia bidhaa na jinsi unavyopangilia huduma zako kulingana na mahitaji ya wateja wako, ni muhimu sana kwa mafanikio ya biashara yako.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; The Million-Dollar, One-Person Business (Jinsi Ya Kuendesha Biashara Yenye Thamani Ya Zaidi Ya Dola Milioni Moja Ukiwa Mwenyewe).

Hatua ya nne; chagua njia ya kulipwa.

Kwa kuwa biashara yako itakuwa mtandaoni, na kwa sehemu kubwa hutakutana ana kwa ana na wateja wako, unapaswa kuwa na njia ya kuweza kulipwa.

Kwa sasa zipo njia nyingi za kuweza kulipwa na wateja hata kama hampo ana kwa ana. Unaweza kulipwa kwa njia ya benki na pia unaweza kulipwa kwa njia ya huduma za kifedha za mitandao ya simu, kama MPESA, TIGO PESA na kadhalika.

Pia zipo kampuni ambazo zinatoa huduma za malipo mtandaoni. Kupitia kampuni hizi, wateja wako wanaweza kukulipa kwa urahisi kupitia njia yoyote ambayo ni rahisi kwao. Mfano wa kampuni hizi ni DIRECT PAY, PESAPAL na nyinginezo.

Chagua njia utakayolipwa nayo na hakikisha ni rahisi kwa wateja wako kutumia. Njia ya mitandao ya simu ni rahisi kuliko nyingine zote, hivyo unaweza kuanza na hiyo.

Hatua ya tano; itangaze ofa yako kwa dunia.

Baada ya kuwa na ofa nzuri kwa wateja wako, na ukawa na njia bora ya wateja kuweza kukulipa, sasa unachohitaji kufanya ni kuhakikisha dunia inafahamu kuhusu wewe, kuhusu biashara yako na kuhusu ofa unayotoa kwa wateja wako.

Hapa sasa ndipo kazi ya tovuti au blog yako inapoonekana na pia ndipo mitandao ya kijamii inapopata kazi. Unahitaji kuandaa matangazo ya mtandaoni na kuyarusha, unahitaji kuandaa makala za mafunzo zinazoendana na ofa yako na kuwashirikisha watu mtandaoni. Ukikutana na wenye uhitaji, wakijifunza na kuona una kitu cha tofauti unatoa, watakuwa tayari kununua.

Hata uwe na bidhaa au huduma bora kiasi gani, hata kama ofa yako ni nzuri sana, kama watu hawajui uwepo wako hawatanunua. Na kwa dunia ya sasa, dunia yenye kila aina ya kelele, unapaswa kuwa na njia bora ya kuwasiliana na wateja wako na hata dunia kwa ujumla.

Hatua ya sita; jifunze kupitia hatua ya kwanza mpaka ya tano, kisha rudia.

Kwenye hatua ya kwanza mpaka ya tano utajifunza mengi sana pale unapoanza kutekeleza. Kwa kusoma hivi ni rahisi na utajiambia unaweza kufanya. Ukishaanza kufanya ndiyo utakutana na changamoto mbalimbali, hapa ndipo unapaswa kujifunza na kuchukua hatua ili kuwa bora zaidi.

Rekebisha yale unayokosea na imarisha yale unayofanya vizuri na hili litakuwezesha wewe kufanikiwa sana kwenye biashara yako unayofanya kwa kutumia mtandao wa intaneti.

Rafiki yangu, fuata hatua hizo sita na itaweza kuanzisha biashara na kutengeneza kipato kupitia mtandao wa intaneti. Unaweza kujifunza mengi zaidi kuhusu kutengeneza kipato mtandaoni kwa kusoma kitabu nilichoandika; JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG. Kitabu ni softcopy na kinatumwa kwa njia ya email. Kimeeleza kwa kina na kwa picha jinsi mtu unavyoweza kutengeneza blogu yako mwenyewe. Gharama ya kitabu ni tsh elfu 10. Kukipata tuma fedha kwa namba 0755 953 887 au 0717 396 253 kisha tuma ujumbe wenye email yako na jina la kitabu kisha utatumiwa kitabu. Karibu sana upate maarifa haya yatakayokuwezesha kujiajiri kupitia mtandao wa intaneti.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL

Usomaji