Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari MUDA TAYARI UNAO…
Kama kuna kitu unataka kufanya kwenye maisha yako, lakini unajiambia huwezi kukifanya kwa sababu huna muda, unajaribu kujidanganya wewe au wengine.

Muda tayari unao, kwa sababu kila mmoja wetu ana masaa 24 pekee kwenye siku yake.
Hakuna anayeweza kuongeza haya dakika moja kwenye siku yake.
Hivyo unaposema huna muda unaweza kuwa unamaanisha nini? Kwamba wewe siku yako ina masaa 20 badala ya 24?

Rafiki, muda tayari unao, hautaongezeka wala kupungua.
Kitu chochote unachotaka kufanya kwenye maisha yako, tayari unao muda wa kukifanya, unachohitaji ni kuchagua kuacha kufanya vitu vingine ambavyo kwa sasa vinachukua muda wako na kufanya kile ambacho ni muhimu kwako.

Hivyo kama unataka kuwa mkweli, usiseme huna muda wa kufanya kitu, bali sema kulingana na mipango yako na vipaumbele vyako, muda wako ni muhimu zaidi kuliko kile unachotaka kufanya.

Kwa mfano kama unataka kusoma vitabu kila siku lakini unajiambia huna muda, kauli sahihi unayopaswa kujiambia ni ungependa kusoma vitabu, lakini kwa mipango na vipaumbele vyako, kusoma vitabu siyo muhimu sana kwako. Kufuatilia habari au maisha ya wengine ni muhimu zaidi kwako kuliko kusoma vitabu. Unaona jinsi inavyokuwa vizuri ukijiambia ukweli?

Au kama inabidi uanzishe biashara ya pembeni huku ukiendelea ma ajira yako lakini unajiambia huna muda, kauli sahihi ya kujiambia ni kwa mipango na vipaumbele vyako, ni muhimu zaidi kwako kifanya vitu vingine vinavyoendelea kukufanya ukose fedha, kuliko kufanya kitu ambacho kitakuongezea kipato chako.

Jambo linapokuwa muhimu sana kwako, muda wa kulifanya unapatikana. Na jambo lisipokuwa muhimu, utafanya chochote ili tu usiwe na muda wa kulifanya.
Muda tayari unao, ni wewe kuchagua unafanya nini na muda ulionao.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujiambia ukweli kuhusu matumizi yako ya muda.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha