Rafiki yangu mpendwa,

Mtu mmoja aliwahi kunukuliwa akisema duniani kuna watu wa aina ya tatu,

Aina ya kwanza ni watu ambao wanasababisha vitu kutokea, hawa ni watu wanaozalisha vitu, wanaoleta mabadiliko, ambayo wengi wanayafurahia sana.

Aina ya pili ni watu ambao wanashangaa vitu kutokea, hawa ni walaji wa vile vinavyotengenezwa na wale wanaosababisha vitu kutokea. Ni watu wanaofurahia mabadiliko yanayosababishwa na wengine.

Aina ya tatu ni wale ambao hawajui hata ni nini kimetokea, hawa ni wale ambao hawajui hata nini kinaendelea, wao wanaenda na maisha yao ya mazoea na mabadiliko yanaishia kuwa na madhara kwao, bila hata kujua kwa nini wanapata madhara wanayopata.

Swali ni je wewe upo kwenye aina ipi ya watu? Je ni msababishaji wa mambo, mfurahiaji au usiyejua hata nini kinaendelea?

vitabu softcopy

Rafiki, tunaweza pia kuwagawa watu kwenye makundi mawili,

Kundi la kwanza ni wazalishaji, hawa ndiyo wanaotengeneza vitu, wanaleta mawazo mapya na njia mpya za kufanya vitu, hawa ndiyo wanayafanya maisha kuwa rahisi zaidi kwa wengine.

Kundi la pili ni walaji, hawa ni wale wanaotumia vitu vinavyotengenezwa na wengine, wanaofurahia vitu vipya ambavyo ni bora zaidi.

Swali ni je wewe upo upande upi, wa uzalishaji au ulaji?

Kwa kawaida, kila mtu anapaswa kuwa mlaji na mzalishaji, kwa sababu kila mtu kuna kitu anapaswa kuchangia kwenye hii dunia.

Lakini kwa maisha ya sasa, tumeishia kuwa na walaji wengi kuliko wazalishaji. Watu wengi wanafurahia kupata vitu vya wengine, lakini hawajiulizi ni kipi ambacho wao wamechangia kwenye maisha ya wengine.

Kadiri teknolojia inavyokua na kuja na vitu bora, watu wanavifurahia sana. zikitoka simu mpya kila mtu anakimbilia kupata simu hizo, huo ni ulaji. Ukianzishwa mtandao mpya wa kijamii kila mtu anakimbilia kuwa mwanachama, ulaji. Watu wanaamka asubuhi tayari kwa ulaji, wanaanza na ulaji wa habari mbalimbali, kisha ulaji wa kufuatilia maisha ya wengine kupitia mitandao, halafu ulaji wa kazi za wengine.

SOMA; NYEUSI NA NYEUPE; Kuhusu Kufanya Kazi Kwa Nguvu Na Kufanya Kazi Kwa Akili.

Mtu anaweza kuianza siku mpaka anaimaliza hakuna kikubwa alichozalisha, zaidi ya kula vile vilivyozalishwa na wengine. Sasa siku za aina hii zinapojirudia kwa muda, ndiyo unapata mtu ambaye hana mafanikio yoyote, yupo tu anasukuma maisha.

Rafiki yangu mpendwa, ujumbe wangu kwako leo ni jinsi unavyoweza kuacha alama hapa duniani na kuishi milele hata baada ya kufa. Na njia pekee ya kufanya hivyo ni kuzalisha, na siyo tu kuzalisha, bali kuzalisha vitu ambavyo vinagusa maisha ya wengine.

Unapaswa kuacha kuwa mlaji pekee, unahitaji kuzalisha. Unahitaji kutoa mchango wako kwenye maisha ya wengine, unahitaji kuacha alama kwenye maisha ya wengine, kiasi kwamba siku za mbele huko watayaangalia maisha yao na kusema nilikutana na mtu fulani au kazi yake na imeyafanya maisha yangu kuwa bora sana.

Na huhitaji kua mvumbuzi mkubwa sana ndiyo uweze kuacha alama hapa duniani. Bali unahitaji kuifanya kazi yako vizuri, kwa uzalishaji wa hali ya juu sana, kiasi kwamba kila anayekutana na kazi yako, maisha yake yanakuwa bora kiasi kwamba hawezi kusahau kabisa.

Kama wewe ni mwalimu wafundishe wanafunzi wako vizuri kiasi kwamba kwa maisha yao yote hawatakusahau. Weka kitu kwenye maisha yao ambacho kitawafanya wakukumbuke kwa maisha yao yote.

Kama wewe ni daktari toa huduma bora kabisa za utabibu kwa wagonjwa wako. Yafanye maisha yao kuwa bora kiasi kwamba hawatasahau kukutana na wewe kwenye maisha yao.

Kama wewe ni kiongozi waongoze watu wako kwa namna bora kabisa, namba ambayo hawajawahi kuongozwa kwenye maisha yao yote. Wafanye wakukumbuke mara zote kwa jinsi ulivyoweza kuwatoa eneo moja kwenda eneo jingine.

Kama wewe ni mwandishi, andika vitu ambavyo vitayafanya maisha ya wasomaji wako kuwa bora. Waandikie kile wanachopaswa kujua lakini hakuna anayewaambia. Wape maarifa na taarifa ambazo wakitumia kwenye maisha yao, wanaona mabadiliko makubwa na wanakukumbuka kwa maisha yako yote.

Unajionea wewe mwenyewe rafiki, huhitaji kuwa na akili nyingi sana, mtaji mkubwa au uvumbuzi wa kipekee ndiyo uache alama kuwa hapa duniani. Bali unachopaswa kufanya ni kuwahudumia watu, kuwapa kile ambacho kitayafanya maisha yao kuwa bora zaidi. Na hilo lipo ndani ya uwezo wako kwa chochote kile unachofanya.

Weka watu kuwa kipaumbele cha kwanza kwako, weka jukumu lako kuu kuwa kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi na kwa njia hii utaishi kwenye maisha yao kwa muda mrefu. Hii ndiyo njia unayoweza kuitumia kuacha alama kwenye hii dunia, na huenda jina lako likaendelea kutajwa hata baada ya wewe kuwa umekufa, hivyo ukaweza kuishi kwa muda mrefu hata baada ya kuwa umekufa.

Ifanye kazi yako rafiki, na yaguse maisha ya wengine kwa namna ambayo hawatakusahau.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL

Usomaji