Haijalishi unafanya nini, kuna vitu vitatokea ambavyo hukutegemea kama vingetokea.

Sisi huwa tunapanga, lakini asili inaendesha mambo yake kwa namna inavyoendesha yenyewe, hivyo haitaenda kulingana na mipango yetu, bali kulingana na mipango yake.

Sasa kwa kuwa huwezi kuidhibiti asili, kwa kuwa huwezi kubadili mipango inayojiendesha kwa asili, hutaweza kuzuia vitu vinavyotokea kwa asili visitokee.

Na hapo ndipo wengi wanapokwama, wanakuwa na njia moja tu ya kufanya kitu, wanakuwa na mpango mmoja tu wa kufanyia kazi kiasi kwamba wanapokutana na changamoto au dharura basi wanashindwa kabisa kuendelea.

Ili kuzuia changamoto na dharura zisiwe kikwazo kwako, unahitaji kuwa na maandalizi bora sana tangu unapoanza. Unahitaji kuwa na njia mbadala za kufanya kile ulichopanga kufanya na uwe na mpango mbadala pale mpango mmoja unapokwama.

Hivyo kabla hujaanza, angalia njia zote ambazo zinaweza kukukwamisha, angalia changamoto zote unazoweza kukutana nazo, kisha kuwa na maandalizi kwa kila unachofikiria kinaweza kutokea.

Pia kuwa tayari kuchukua hatua za tofauti pale kinapotokea kitu ambacho hukufikiria kama kingeweza kutokea.

Kwa mfano kama kuna kitu unashirikiana na wengine kufanya, au unategemea wengine wakamilishe hatua fulani kabla ya wewe kuendelea, hakikisha una kitu mbadala cha kufanya kwa sababu mara nyingi sana mtu unayemtegemea afanye kitu fulani huwa hafanyi kwa namna ulivyokuwa unategemea. Labda atachelewa kukamilisha au atafanya kwa kiwango tofauti na ulivyotegemea.

Usikubali jambo lolote litokee kwenye maisha yako na likushangaze, kwamba kiwe ni kitu ambacho hukutegemea kabisa kitokee. Hiyo itaonesha hukuwa na maandalizi ya kutosha na hivyo kutoa nafasi kwa vitu vingine kukukwamisha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha