Upo usemi kwamba nyasi za jirani huwa zinaonekana ni za kijani kuliko nyasi zetu wenyewe. Yaani kama kwenye uwanja wako umepanda nyasi, na jirani yako naye amepanda nyasi, ukiangalia nyasi za jirani yako utaona zinaendelea vizuri kuliko zako. Unaweza kuona labda jirani huyo ana bahati na wewe huna bahati.

Lakini ni mpaka utakapoenda kwa jirani yako utashangaa kuona nyasi zake ni kama zako. Na ukiwa kwake, ukiangalia nyasi zako, utaona ni za kijani kuliko za jirani yako.

Huu ni mfano ambao unaelezea kile tunachofanya kwenye maisha yetu ya kila siku. Tukiangalia maisha ya wengine, tukiangalia kazi zao na biashara zao, tunaona mambo yao yako vizuri sana kuliko yetu. Tunaona wao wameshafanikiwa sana wakati sisi hatujui hata ni nini tunafanya.

Ni mpaka upate nafasi ya kujua kwa undani maisha ya watu hao, kazi zao na biashara zao ndiyo utagundua kwamba siyo kitu unachoweza kukionea wivu na kutamani kuwa nacho. Utakapogundua kwamba na wao wanapitia changamoto kama unazopitia wewe, wanakutana na magumu mengi, ndiyo utagundua kwamba haupo vibaya kama unavyojifikiria.

Kama nyasi za jirani yako zinaonekana ni za kijani kuliko zako, basi jua ni kwa sababu jirani yako ananyeshea nyasi zake na kuzihudumia vizuri kuliko unavyofanya kwenye nyasi zako.

Unachohitaji siyo kupata nyasi za jirani yako, bali kuhudumia nyasi zako vizuri. Na kama utatumia muda unaotumia kujilinganisha na wengine, ukaweka muda huo kwenye kufanya kilicho bora, utaweza kupiga hatua kubwa sana.

Hapo ulipo sasa, iwe ni kwenye mahusiano, kwenye kazi, kwenye biashara au kingine chochote unachofanya kwenye maisha yako, umekalia mgodi wa dhahabu, kuna fursa kubwa zinakuzunguka ambazo bado hujaziona kwa sababu huzitafuti. Kwa sababu unatumia muda mwingi kuangalia wengine wanafanya nini, unashindwa kuona vitu vya wazi vilivyo mbele yako.

Anza kuangalia kwa kina kila ulichonacho, kila ulichojifunza, kila uzoefu ulionao na kila unayemjua kwenye maisha yako na angalia vitu na watu hao wanawezaje kukusaidia kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.

Kitu unachosumbuka nacho sasa, kuna mtu unayemjua ambaye ana majibu mazuri sana, sasa hutaweza kumpata na kupata majibu hayo kama hutaanza kujiangalia wewe mwenyewe kwanza na kugundua mgodi wa dhahabu ambao tayari unao.

Kabla hujajiambia mambo yako ni magumu na ya wengine ni mazuri, anza kujikagua kwanza kwa kila kinachokuzunguka na utaona jinsi ambavyo una fursa nzuri ambazo hujazifanyia kazi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha