Rafiki yangu mpendwa,

Nimewahi kukuambia kwa asili sisi binadamu ni viumbe wavivu sana, ambao tunapenda kupata zaidi kwa kutoa kidogo. Tunapenda kufanya kazi ndogo iwezekanavyo lakini tupate matokeo makubwa kuliko inavyowezekana. Tunapenda kulipa kidogo lakini kupata zaidi. Na hili siyo baya na wala siyo zuri.

Siyo baya kwa sababu ni kwa njia hii tumeweza kugundua vitu vingi vya kurahisisha maisha yetu. Uvumbuzi wa mashine mbalimbali ni matokeo ya uvivu wetu, kwa sababu hatutaki kufanya kazi zaidi, basi tunafikiria zaidi nini kinaweza kurahisisha kazi zetu na hapo ndipo watu walikuja na gunduzi mbalimbali.

Na pia hali hii siyo nzuri kwa sababu uvivu wetu wa asili unakuwa kikwazo kwetu kupiga hatua na kufanikiwa zaidi. Licha ya kuwepo kwa njia mbalimbali za kurahisisha kazi zetu, bado haituondoi sisi kwenye kuweka juhudi zaidi ili kupata kile tunachotaka.

Kwa mfano, watu wengi huwa tunapanga kufanya mambo makubwa ili kuweza kufikia malengo makubwa ya maisha yetu. Lakini inapofikia kwenye kuanza hatuanzi, au hata tukianza, tunaishia njiani, pale ambapo tunakutana na changamoto mbalimbali kwenye kile tunachofanya.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

Sasa kwa kuwa hakuna kinachokosa changamoto, wengi wamekuwa wanaishia njiani.

Sasa kwa kuwa udhaifu wetu ni kwenye kuweka kazi na juhudi kubwa, zipo njia tatu za kutuwezesha kuvuka changamoto hii na kufika tunakotaka kufika. Njia zote hizi zinahusisha kuwapa watu wengine jukumu la kutufuatilia kwa karibu kwenye yale tuliyopanga kufanya, ili isiwe rahisi kwetu kukata tamaa au kuacha.

Iko hivi rafiki, kama umeweka malengo yako mwenyewe, kama umejipangia vitu vyako mwenyewe, ukaanza kufanya na ukakutana na ugumu, ni rahisi kujiambia haina haja ya kuendelea na utaacha. Lakini kama utakuwa umemhusisha mtu mwingine kwenye mipango hiyo, itabidi uanze kufikiria utamwambiaje mtu huyo kwamba utaacha. Na kama ni mtu atakayekuhoji kwa kina, utalazimika kuendelea hata kama umekutana na ugumu.

Hivyo kwa chochote kikubwa unachotaka kufanya na maisha yako, hakikisha kuna mtu mwingine anayejua na siyo wewe pekee. Hii itakupa sababu ya kuendelea kwa sababu kuna watu wanakufuatilia kwa karibu.

Na zipo njia tatu za kupata watu wa kukufuatilia kwenye kile unachofanya.

Moja; mtu wa karibu unayemheshimu.

Njia ya kwanza ni kutumia mtu wa karibu yako, ambaye unamheshimu sana na kumwahidi kwamba unataka kufanya kitu fulani kwenye maisha yako na ungeomba akusimamie kwa karibu.

Hii ni njia rahisi kwa sababu mtu anayekujua anajua wapi madhaifu yako yalipo, na kwa heshima uliyonayo kwake, utajilazimisha kufanya hata kama mambo ni magumu kiasi gani.

Changamoto ya njia hii ni kwamba, mtu huyu atakusimamia tu kwa karibu, lakini hataweza kukusaidia kwa karibu pale unapokutana na changamoto. Hivyo ukimwendea na changamoto unayoona ni kubwa sana, itakuwa rahisi kwake kukubaliana na wewe kwamba haiwezekani hivyo acha tu.

Mbili; kutumia jamii nzima.

Siku hizi kuna mitandao ya kijamii, hivyo unaweza kutumia jamii nzima kukufuatilia kwa karibu kwenye kile unachofanya.

Kwa njia hii, unatangaza wazi kwamba ni kitu gani unataka kufanya na unawaomba watu wakufuatilie kwa karibu ukiwa unafanya. Hapa unakuwa umejitoa kweli kweli na umejiweka kwenye nafasi ya kukosolewa na kupingwa pia. Lakini kadiri unavyotaka kulinda heshima yako kwenye jamii, utajilazimisha kuhakikisha unakamilisha ulichopanga na kuwatangazia watu kwamba umemaliza.

Changamoto ya njia hii ni hakuna anayekufuatilia kwa karibu, hivyo wakati mwingine unaweza hata kudanganya na watu wasijue. Pia kwa kutangaza mipango yako mikubwa unajiweka kwenye hatari ya watu kukukosoa na kukupinga sana. Badala ya watu kuwa hamasa kwako, wanakuwa wakatishaji tamaa.

SOMA; Hii Ndiyo Sababu Moja Kwanini Unarudia Makosa Mengi Kila Siku Kwenye Maisha Yako

Tatu; kuwa na kocha anayekusimamia.

Njia ya tatu ya kukulazimisha wewe ufanye kile ambacho unajua unapaswa kufanya ni kuwa na kocha ambaye anakusimamia kwa karibu sana. Kocha huyu ni mtu mwenye ujuzi na uzoefu wa kuwawezesha watu kufanya yale wanayopaswa kufanya hata kama hawajisikii kufanya.

Njia hii ni nzuri kwa sababu kwanza unamlipa kocha, hivyo kama usipofanya unakuwa umepoteza fedha zako, na hakuna anayependa kupoteza fedha, hivyo unapolipia huduma hiyo, unakuwa umejipanga kweli kuifanyia kazi.

Pia kocha ana uzoefu na mbinu za kukuwezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali unazokutana nazo, hivyo unapokuwa na kocha, fikra kwamba umekutana na kitu kikubwa na haiwezekani tena haziwezi kukujia kwa namba yoyote ile.

Changamoto ya njia hii ni kwamba utahitaji kulipa gharama na pia itabidi ukubali kufuatiliwa kwa karibu mpaka ujisikie vibaya kwa nini mtu akufuatilie hivyo. Lakini hilo litakuwezesha kupata unachotaka.

Rafiki, kama kuna mipango ambayo umekuwa unaweka kila mwaka na hukamilishi, kama kuna kitu umekua unajiambia unafanya lakini unaahirisha au ukianza unaacha, chagua njia moja kati ya hizo tatu na anza kuitumia leo, utapata matokeo tofauti na ambavyo umekuwa unapata.

Na kama utahitaji kupata kocha wa kukusimamia na kukufuatilia kwa karibu, basi nipo hapa kwa ajili yako, jukumu langu ni kuhakikisha wewe unafika pale unapotaka kufika, kupata kile unachotaka kupata. Karibu sana.

MAREKEBISHO YA TAREHE YA MWISHO WA KULIPIA SEMINA.

Rafiki, kwenye moja ya email zilizopita, nilikuambia mwisho wa kulipia ili kushiriki SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018 ambayo itafanyika tarehe 03/11/2018 ni tarehe 31/12/2018, hiyo siyo tarehe sahihi, tarehe sahihi ni 31/10/2018.

Hivyo tarehe ya mwisho kwako kulipia ili tukutane pamoja tarehe 03/11/2018 kwa ajili ya kujifunza, kuhamasika na kuweka mkakati wa mwaka mzima ni tarehe 31/10/2018. Fanya malipo yako ya ada kabla ya tarehe hiyo, ili uweze kushiriki semina hii ya kipekee sana kwako kwa mwaka huu 2018.

Kiasi cha ada ya kushiriki ni tsh 100,000/= (laki moja) na unalipa kwa namba 0755 953 887 au 0717 396 253. Unaweza kulipa kidogo kidogo ili mpaka siku ya mwisho kulipia inapofikia uwe umeshalipa.

Karibu sana rafiki yangu kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu

Usomaji