Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi wamekuwa wanafikiri kwamba kufanya kitu kwa muda mrefu ndiyo wanapata uzoefu na kuwa bora zaidi. Na hata matangazo mbalimbali ya kazi huwa yanasisitiza kwenye hilo la uzoefu. Wataandika tunataka mtu lakini awe na uzoefu wa miaka kadhaa kwenye kazi hiyo.
Kadhalika watu wamekuwa wanajisifia kwamba wana uzoefu mkubwa kwa sababu wamefanya kitu kwa muda mrefu. Wengi utawasikia wakisema nina uzoefu wa miaka kumi kwenye kazi au biashara hii. Lakini unapochimba kwa ndani unagundua hawana uzoefu wa miaka kumi, bali wana uzoefu wa mwaka mmoja ambao umejirudia mara kumi.
Kwa kifupi watu wengi hawapati uzoefu kwa miaka wanayofanya kitu na badala ya kuwa bora kwa kadiri wanavyofanya kitu kwa muda mrefu, wanazidi kuwa hovyo.
Na hili sisemi mimi, bali tafiti za kisayansi na kijamii zinaonesha hivyo. Kwa mfano utafiti ambao umewahi kufanywa kwa madaktari unaonesha madaktari wengi waliofanya kazi kwa muda mrefu, uzoefu wao unakuwa mbaya kuliko wale ambao wametoka shuleni ndani ya miaka 2. Yaani pamoja na wengi kuweka imani kubwa kwa madaktari waliofanya kwa muda mrefu, uhalisia ni kwamba matokeo yao ni mabovu kuliko ya wale ambao wametosha shuleni siku siyo nyingi.
Mwanasaikolojia na mwandishi Anders Ericsson ametafiti kwa kina eneo hili, kutaka kujua nini kinajenga uzoefu kwa baadhi ya watu na wengine kushindwa kujijengea uzoefu licha ya kufanya kitu kwa muda mrefu.
Na katika tafiti zake, amegundua kuna aina tatu za ufanyaji wa kitu ambazo zinachangia sana kwenye uzoefu ambao mtu atautengeneza.
Aina ya kwanza ni kufanya kwa kawaida na mazoea, hapa mtu anafanya kitu jinsi alivyozoea kufanya na hakuna kipya anachojaribu. Hii ndiyo inazalisha uzoefu mbaya licha ya mtu kufanya kitu kwa muda mrefu.
Njia ya pili ni kufanya kwa malengo, hapa mtu unakuwa na malengo ya kufanya kitu na unajisukuma kufanya kwa ubora na kujaribu vitu vipya. Hii ndiyo inazalisha watu wanaokuwa na uzoefu mkubwa kwenye kile wanachofanya na kuwa bora zaidi kadiri muda unavyokwenda.
Njia ya tatu ni kufanya kwa makusudi, hapa unakuwa na malengo, lakini pia unakuwa na mtu wa kukusimamia, mwalimu au kocha ambaye ana uelewa mkubwa wa kule unakotaka kufika. Faida ya kufanya kwa makusudi ni unaepuka kufika ukomo ambao wengi wanafikia wanapojiwekea malengo. Pale unapokuwa na mtu anayekusimamia, atakusukuma zaidi ya unavyoweza kujisukuma zaidi.
Kwenye makala ya leo nakwenda kukushirikisha jinsi unavyoweza kutumia njia ya pili ya kufanya kwa malengo kujijengea uzoefu mkubwa na kuweza kufanikiwa sana kupitia kile unachofanya. Na kwenye uchambuzi wa kitabu cha juma, tutakwenda kujifunza kwa kina kuhusu njia ya tatu ambayo ni kufanya kwa makusudi. Kupitia kitabu cha PEAK, Anders ameeleza kwa kina sana jinsi tunavyoweza kufanya kwa makusudi.
Ili kuweza kufanya kitu kwa malengo na kujijengea uzoefu mkubwa na kufanikiwa, kuna mambo manne muhimu sana unayopaswa kuyazingatia.
MOJA; UNAPASWA KUWA NA MALENGO.
Hatua ya kwanza na muhimu katika kujijengea uzoefu mkubwa ni kufanya kitu kwa malengo. Lazima uwe na malengo ya muda mfupi na muda mrefu kwenye kile unachofanya. Malengo yanakufanya ujisukume zaidi na upige hatua zaidi kuliko kutokuwa na malengo.
Unapokuwa na malengo ni rahisi kuona kama unapiga hatua au umebaki pale pale. Bila ya malengo unaweza kujiona upo vizuri kumbe hakuna hatua unayopiga. Na kama hakuna hatua unayopiga, unarudi nyuma, kwa sababu maisha hayana kusimama, ni kwenda mbele au kurudi nyuma.
Jiwekee malengo kwenye kazi au biashara unayofanya, kila mwaka panga ni hatua zipi unataka kupiga, na pia kuwa na malengo ya miaka mingi unayoyafanyia kazi, labda baada ya miaka mitano na kumi uwe umepiga hatua ambazo ni kubwa. Kuwa na malengo kunakufanya upige hatua ambazo usingeweza kupiga bila ya malengo.
SOMA; Njia Tatu Za Kukulazimisha Kufanya Kile Unachojua Unapaswa Kufanya Lakini Hujisikii Kufanya.
MBILI; UNAPASWA KUWEKA UMAKINI WAKO KWENYE KILE UNACHOFANYA.
Tatizo kubwa ambalo watu wanalo ni kukosa umakini kwenye kile wanachofanya, hivyo wanajikuta wakifanya tu kwa mazoea. Hata unapowauliza kwa kina kuhusu wanachofanya, hawawezi kukueleza kwa nini wanafanya baadhi ya vitu wanavyofanya, wao wanajua tu kwamba wamezoea kufanya hivyo.
Ili kujijengea uzoefu mkubwa na kuweza kupiga hatua, unapaswa kuweka umakini wako kwenye kile unachofanya. Kwanza jua kwa nini unafanya kila unachofanya, hatua yoyote unayochukua jua umuhimu wake na ichukue kwa umakini mkubwa sana.
Unapokuwa unafanya kazi au biashara yako, mawazo yako yote yanapaswa kuwa kwenye kile unachofanya. Siyo unafanya kitu huku mawazo yako yapo sehemu nyingine tofauti na kile unachofanya. Kufanya kitu bila ya kuweka umakini ni kuruhusu mazoea yakutawale na hutaweza kupiga hatua kama mazoea yamekutawala.
Chochote unachoanza kufanya huwa unakuwa na umakini mkubwa mwanzoni, kwa sababu unakuwa hujui vitu vingi. Lakini baada ya muda unagundua mengi unayofanya ni yale yale, yanajirudia. Na hapa ndipo umakini unapoanza kupungua na kujikuta unafanya kwa mazoea. Usiruhusu kabia hali hii ikuingie. Endelea kuweka umakini mkubwa kwenye kile unachofanya kama ulivyokuwa unaweka wakati unaanza kufanya.
Unapoweka mawazo na fikra zako zote kwenye kile unachofanya unaona mambo mengi zaidi ya kuboresha na fursa za kupiga hatua zaidi kuliko yule ambaye anafanya kwa mazoea.
TATU; UNAPASWA KUPATA MREJESHO WA NAMNA UNAVYOFANYA.
Mrejesho ni muhimu sana kwa wewe kuweza kupiga hatua kubwa kwenye chochote unachofanya. Bila ya kuwa na mrejesho hutaweza kujua kama unapiga hatua au unarudi nyuma.
Mrejesho unaweza kutoka kwenye kile unachofanya au ukatoka kwa wengine. Unapokuwa na malengo na kuweka mipango unayoifanyia kazi, kadiri unavyotekeleza mipango hiyo ni mrejesho kwako kwamba unapiga hatua. Pia pale wengine wanapokuambia unapiga hatua, hasa wale wanaotegemea kile unachofanya, ni mrejesho kwamba unakwenda vizuri.
Bila ya mrejesho itakuwa vigumu kwako kujipima na huwezi kujijengea uzoefu mkubwa na utakaokuwezesha kufanikiwa zaidi. Kwa kila unachofanya, weka njia ya kupima hatua unazopiga, kuwa na njia inayokupa mrejesho kwenye kila unachofanya.
NNE; UNAPASWA KUTOKA NJE YA MAZOEA.
Sumu kubwa inayowazuia wengi kupata uzoefu na mafanikio ni mazoea. Wengi wanaosema wana uzoefu wa miaka mingi, wana uzoefu wa mwaka mmoja uliojirudia mara nyingi. Kufanya kitu kwa namna ile ile, hata ungefanya miaka 20 au 50, haikufanyi uwe na uzoefu mkubwa, badala yake kunakufanya uwe vibaya zaidi. Kwa sababu unapofanya kwa mazoea, mambo yanabadilika na wewe unabaki nyuma.
Unapaswa kutoka nje ya mazoea kwenye kile unachofanya, kila wakati jaribu vitu vipya, vitu ambavyo hujawahi kufanya na vinavyokupa hofu ya kufanya. Unapojaribu vitu hivi vipya vinakusukuma kukua zaidi ya pale ulipo sasa na hili linakuletea uzoefu mpya ambao unakuwezesha kupiga hatua zaidi.
Kila wakati jiulize kipi ambacho umeshazoea kufanya na toka nje ya mazoea. Unaweza kuanza kidogo kidogo kwa kujaribu njia mpya za kufanya kitu au kufanya kitu kipya kabisa ambacho hujawahi kufanya. Ukichagua kufanya kitu kipya, kitakutaka uweke umakini wako wote pale na hilo linakufanya uwe bora zaidi.
Hivyo kwa kifupi, ili kuweza kupata uzoefu mkubwa kwenye kile unachofanya, unapaswa kuwa na malengo unayofanyia kazi na yanayokusukuma, kujaribu vitu vipya na kutoka nje ya mazoea, kuweka umakini wako wote kwenye kile unachofanya na kuwa na njia ya kupima mwenendo wako, kwa kuwa na mrejesho unaoonesha hatua unazopiga.
Zingatia haya na utaweza kujijengea uzoefu mkubwa sana kwenye kile unachofanya na kuweza kupata mafanikio makubwa.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge