#TANO ZA JUMA #8 2019; Siyo Kipaji Ni Juhudi, Siri Za Kufika Kilele Cha Ubobezi, Hatua Nne Za Kujijengea Uzoefu Bora, Ubobezi Katika Fedha Na Umuhimu Wa Kuwa Na Mwalimu Au Kocha.
Rafiki yangu mpendwa,
Karibu kwenye tano za juma la 8 la mwaka huu 2018 ambapo juma hili tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kwenye kitabu kinachoitwa PEAK; Secrets from the New Science of Expertise kilichoandikwa na mwanasaikolojia Anders Ericsson.
Kitabu hiki kinatupa siri za kisayansi za kuweza kufikia ubobezi mkubwa kwenye kitu chochote tunachochagua kufanya kwenye maisha yetu. Kitabu hiki kimetokana na tafiti mbalimbali ambazo zimefanywa kwenye eneo la ubobezi na hivyo kimekuja na majibu sahihi ya hatua unazopaswa kuchukua ili kufikia ubobezi.
Katika tano za juma hili, tutaona kwa nini siyo kipaji kinachowafikisha watu kwenye ubobezi bali juhudi, tutajifunza hatua za kufikia ubobezi. Pia tutajifunza ubobezi kwenye eneo la fedha na umuhimu wa kuwa na kocha au mwalimu katika safari ya ubobezi.
Karibu ujifunze na uchukue hatua ili uweze kufikia ubobezi kwenye maisha yako.
#1 NENO LA JUMA; SIYO KIPAJI NI JUHUDI.
Rafiki, kwa miaka mingi watu wamekuwa wakiamini kwamba kuna watu ambao wamezaliwa na vipaji ambavyo vimewawezesha kufikia kwenye ubobezi mkubwa ana katika maeneo waliyobobea.
Na mifano ipo mingi sana, kwenye utunzi wa nyimbo na upigaji wa vyombo, Morzat anaonekana kuwa mmoja wa watu wenye kipaji kikubwa. Kadhalika kwenye mchezo wa golf, Tiger Woods anaonekana kuwa mchezaji ambao ana kipaji kikubwa kwenye mchezo huo. Na hata michezo mingine na hata kwenye taaluma mbalimbali, wale ambao wamefanikiwa sana wanaonekana kuwa na kipaji kikubwa.
Lakini unapokwenda kuchimba ndani, na kuangalia kwa undani maisha ya wale wanaosemekana wana vipaji, huoni kipaji bali unaona juhudi kubwa na za muda mrefu. Katika mifano niliyotoa hapa, Morzat ambaye anaonena alikuwa na kipaji, alianza kufundishwa kupiga vyombo vya muziki akiwa na miaka minne, ana akawa anafanya hivyo kila siku. Huyu ni mtoto ambaye alikuwa akijua kufanya kitu kimoja tu, muziki. Je utamlinganisha na mtu mwingine anayekuja kujifunza muziki ukubwani?
Ukiangalia kwa Tiger Woods pia, wazazi wake wanakiri kumpa michezo ya kitoto inayoendana na mchezo wa golf tangu akiwa na miezi tisa, huyu ni mtu ambaye tangu anapata utambuzi wake, anajua kitu kimoja tu, golf, je utaweza kumshindanisha na mtu mwingine ambaye amejua mchezo huo baadaye?
Chagua mtu yeyote unayeamini ana kipaji, iwe ni mchezaji, mwanasayansi na hata kiongozi, na angalia maisha yake tangu utotoni, utagundua kuna mazingira ambayo yalimweka kwenye juhudi ambazo zilimwandaa kufikia ubobezi huo. Hata wachezaji wenye ubobezi mkubwa kama Christiano Ronaldo na Messi, ukiangalia utoto wao, wametumia sehemu kubwa kwenye kujifunza mchezo wa mpira. Angalia maisha ya wanasayansi kama Eistein, Newton na wengineo, wote waliweka muda na juhudi kubwa kabla hawajafikia ubobezi ambao wengi wanakuja kuamini ni vipaji vimewafikisha pale walipo.
Hivyo ujumbe kwako rafiki yangu ni huu, unaweza kubobea kwenye jambo lolote lile, kama tu utaweka juhudi ambazo zinapaswa kuwekwa ili kufikia ubobezi. Na kwenye kitabu cha juma hili cha PEAK, tunakwenda kujifunza juhudi sahihi unazopaswa kuweka ili kufikia ubobezi.
Usijiambie tena kwamba huwezi kufikia ubobezi kwa sababu huna kipaji au uwezo. Tafiti zote ambazo zimefanywa kwenye ubobezi zimekuja na jibu moja, wale wanaofikia ubobezi wana uwezo mkubwa sana, lakini ni uwezo ambao upo ndani ya kila mmoja wetu. Kinachotutofautisha sisi na wale waliobobea sana ni kiasi ambacho tumeendeleza uwezo ambao upo ndani yetu.
Uwezo tayari unao, unachohitaji ni juhudi ili kubobea, aina gani ya juhudi utakwenda kujifunza kwenye kitabu cha juma.
#2 KITABU CHA JUMA; SIRI ZA KUFIKA KILELE CHA UBOBEZI.
Juma hili tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kwenye kitabu kinachoitwa PEAK; Secrets from the New Science of Expertise. Na hapa nimekushirikisha yale muhimu sana kuzingatia ili kuweza kufikia ubobezi wa hali ya juu sana kwenye kitu chochote ambacho umechagua kufanya kwenye maisha yako.
MOJA; NGUVU YA KUFANYA KWA MALENGO.
Kinachowatofautisha wale wanaofikia ubobezi na wale wanaoishia kuwa kawaida siyo wanachofanya, bali namna wanavyofanya kile wanachofanya. Watu wawili wanaweza kuwa wanafanya kitu kimoja, lakini mmoja akabobea na mwingine asibobee.
Mwandishi anatuambia zipo aina tatu za ufanyaji ambazo zinawatofautisha wanaobobea na wanaokuwa kawaida.
Aina ya kwanza ni kufanya kwa kawaida, hapa mtu anafanya kile ambacho amezoea kufanya kila wakati, hakuna kipya anachofanya na hivyo hawezi kubobea. Hivi ndivyo wengi wanavyoendesha maisha yao, wanaonekana kufanya sana lakini hakuna hatua wanapiga. Hii ni kwa sababu wanafanya kwa mazoea.
Aina ya pili ni kufanya kwa malengo, hapa mtu anafanya kitu kwa malengo, na hivyo anakuwa na hatua anazopanga kupiga zinazomsukuma kufanya zaidi. Katika kufanya kwa malengo mtu anapiga hatua zaidi kwa sababu malengo anayojiwekea yanamsukuma zaidi. Kwenye kufanya kwa malengo mtu anakuwa na sifa nne; moja anakuwa na lengo la wapi anataka kufika, mbili anaweka umakini wake wote kwenye kile anachofanya. Tatu anakuwa na njia ya kujipima na kupata mrejesho wa hatua anazochukua na nne anajisukuma kutoka nje ya mazoea, kufanya vitu vipya ambavyo vinamwezesha kupiga hatua zaidi.
Aina ya tatu ni kufanya kwa makusudi, kama mwandishi anavyoita DELIRATE PRACTICE, hapa mtu anakuwa na kusudi kubwa linalomsukuma kufanya kitu. Hii ndiyo aina ya ufanyaji ambayo inazalisha watu wenye ubobezi wa hali ya juu. Kufanya kwa makusudi kuna sifa kama za kufanya kwa malengo, lakini ina sifa nyingine mbili za nyongeza. Ya kwanza ni eneo ambalo mtu anakuwa amechagua kubobea linapaswa kuwa na wabobezi ambao wanaweza kuangaliwa na mtu akajifunza kwao. Mtu anapoweza kuwaangalia wabobezi na kujifunza kile wanachofanya na namna wanavyofanya, inakuwa rahisi kwake naye kufanya. Sifa ya pili ni kuwa na mwalimu au kocha ambaye anamfundisha na kumsimamia mtu kwenye hatua anazochukua. Kwa kuwa na mtu wa nje anayetoa maelekezo au kupima hatua mtu anazochukua na kutoa mrejesho, kunamfanya mtu apige hatua kubwa zaidi.
Hizo ndizo aina tatu za ufanyaji na aina ya tatu ndiyo mwandishi ameijadili kwa kina sana kwenye kitabu cha PEAK. Kwenye uchambuzi huu tutajifunza kwa kina jinsi ambavyo tunaweza kutumia aina ya tatu ya ufanyaji na kufikia ubobezi kwenye kitu chochote ambacho tumechagua kufanya.
MBILI; KUTUMIA NGUVU YA MABADILIKO YA MWILI NA UBONGO.
Kinachofanya iwe rahisi kwa watu kubobea, ni mabadiliko ambayo miili na ubongo wetu inaweza kuyapokea.
Kujifunza kitu kipya ni rahisi kwa watoto kuliko watu wazima kwa sababu miili yao bado inakuwa na ubongo wao bado unakuwa unajiendeleza. Ndivyo maana mtu anapoanza kufanya kitu utotoni, anaonekana kuwa na kipaji kikubwa baadaye. Hii ni kwa sababu miili na ubongo wao unabadilika na kuendana na kile ambacho wanakuwa wanafanya.
Lakini kadiri mtu anavyokua, mwili unakomaa na ubongo unakuwa umekamilika kujiendeleza, na hivyo kujifunza kitu kipya kunakuwa kugumu na kwa taratibu.
Lakini siyo kwamba ukishakuwa mtu mzima huwezi tena kujifunza kitu kipya. Mwandishi ametushirikisha tafiti nyingi zinazoonesha watu wazima ambao wamejifunza michezo mipya na miili yao ikaweza kuzoea. Na kwa upande wa ubongo, pia zipo tafiti zinazoonesha ubongo kuweza kubadilika hata kwa watu wazima. Na udhibitisho wa hilo unatoka kwa madereva teksi wa jiji la London. Ili kupewa leseni ya kuendesha teksi kwenye jiji la London, dereva lazima afaulu mtihani ambao unamtaka kuwa amekariri mitaa na majengo yote yanayozunguka Charing Cross. Hivyo madereva hao wanaotaka kupata leseni inawabidi wakariri kwa kichwa mitaa yote, nyumba zote, vituo vyote, majengo ya serikali, hospitali, nyumba za ibada, kwa kifupi mpaka alama za barabarani wawe wamekariri. Kipimo cha ubongo kwa madereva waliofaulu mtihani huo na kupata leseni kinaonesha sehemu za ubongo wao kuwa kubwa kuliko watu wa kawaida.
Mfano huo na mingine mingi inaonesha kwamba mtu yeyote, bila ya kujali umri anaweza kujiendeleza na kufikia ubobezi kama atachukua hatua sahihi. Inasaidia sana kama mtu akianza akiwa mtoto kwa sababu hatapoteza muda mwingi. Lakini kama ulikosa nafasi utotoni usiumie, sasa unaweza kuanza na ukapiga hatua kubwa.
TATU; KUTENGENEZA TASWIRA KWENYE AKILI YAKO.
Katika kufikia ubobezi, unapaswa kutengeneza taswira kwenye akili yako juu ya kile unachofanya. Wale waliobobea huwa wanakuwa na taswira ya kiakili juu ya kile wanachofanya, hivyo wanajua hatua zote za ufanyaji na kuwa na mategemeo nini kitatokea kwenye hatua ipi.
Mfano mzuri wa taswira ya kiakili ni kwenye michezo mbalimbali. Kama hujawahi kuangalia kabisa mpira wa miguu na hujui unachezwaje, ukiona watu 22 wanakimbizana na mpira mmoja unaweza kusema wamechanganyikiwa, kwa nini kila mtu asipewe mpira wake na akakimbia nao, kwa nini wote wakimbilie mpira mmoja? Lakini kwa shabiki ambaye anaujua mchezo huo, anajua kwa nini wachezaji wanakimbiza mpira mmoja. Na hata akute mchezo katikati, anajua nini kinaendelea na kuweza kuelewa vizuri. Na kwa mchezaji wa mpira wa miguu, ndiyo kabisa anaweza mpaka kusema nini kitatokea kwenye mchezo huo, kwa kuangalia kwa muda mfupi.
Unapaswa kujijengea taswira za kiakili kwa kile unachofanya, taswira ambazo zitakusaidia kubeba taarifa nyingi kwa wakati mmoja.
Kikwazo kikubwa kwetu kubeba taarifa nyingi juu ya kitu fulani ni ukomo wetu wa kumbukumbu za muda mfupi. Akili yetu inaweza kukumbuka vitu saba pekee kwa wakati mmoja. Ndiyo maana unaweza kukariri namba yako ya simu kwa urahisi kuliko kukariri namba yako ya akaunti. Lakini ukifikiria namba hiyo ya akaunti kwa muda mrefu, unaikariri, kwa sababu hapo inaingia kwenye kumbukumbu za muda mrefu.
Wakati unajifunza kitu na kuchukua hatua, unatumia zaidi kumbukumbu za muda mrefu, hivyo njia pekee ya kupokea na kutunza taarifa nyingi unazopata wakati huo ni kuwa na taswira za kiakili ambazo zinakuwezesha kubeba taarifa nyingi kwa wakati mmoja. Mfano kwenye kukariri namba nyingi, unazikusanya pamoja kwa mafungu yenye maana kwako, ambayo unayapa picha fulani utakayoikumbuka kirahisi.
Katika kujijengea taswira ya kiakili, inakuwa rahisi pale mtu anapochagua eneo ambalo anataka kubobea na kuweka juhudi zake hapo. Ni vigumu kuweza kuwa na taswira za kiakili kwenye maeneo mengi, lakini unapochagua eneo moja unabobea vizuri. Mfano kwa madereva teksi wa London, licha ya kuweza kukariri mitaa yote ya London, kwenye majaribio ya kumbukumbu nyingine hawaoneshi kuwa na kumbukumbu kuliko watu wa kawaida. Hivyo kinachowawezesha kukariri mitaa hiyo siyo uwezo mkubwa wa kumbukumbu walionao, bali uwezo wa kutengeneza taswira ya mitaa yote na vilivyopo kwenye akili zao.
TATU; KIWANGO CHA JUU CHA UFANYAJI.
Hakuna mtu yeyote ambaye amefikia ubobezi wa hali ya juu sana kwenye kile anachofanya bila ya kuweka juhudi kubwa na kwa muda mrefu. Hivyo ndivyo tafiti zote zinavyoonesha. Na tafiti hizi zinaonesha pia kwamba wale wanaofikia ubobezi wa hali ya juu, wanafanya kwa makusudi. Haitokei kama ajali kwamba mtu amefikia ubobezi, bali mtu anautafuta kweli ubobezi huo, kwa kuweka juhudi kubwa mno. Wakati mwingine anakuwa hata hafurahii, lakini kwa kuwa ana kusudi kubwa na msukumo wa kufanya, anafanya.
Hivyo tunaweza kusema kwamba kiwango cha juu kabia cha ufanyaji, ambacho kinazalisha wabobezi wa hali ya juu ni kufanya kwa makusudi (deliberate practice).
Kama ambavyo tumeona, kufanya kwa makusudi ni aina ya kipekee ya ufanyaji ambapo eneo unalotaka kubobea lazima liwe lina wabobezi ambao mtu unaweza kujifunza kwao. Na pia unahitaji kuwa na mwalimu au kocha ambaye atakufundisha na kukusimamia kwa karibu.
Maeneo ambayo yanaweza kuwa na sifa hizo mbili na ambayo mtu unaweza kufanya kwa makusudi ni michezo ambayo ni rahisi kupimika kwa nje kama muziki (upigaji wa vyombo), chess, tenesi, golf na hata riadha.
Pamoja na kwamba maeneo machache ndiyo yanakidhi ufanyaji kwa makusudi, bado unaweza kutumia misingi hii kwenye chochote ambacho mtu unafanya, iwe ni kazi, biashara au hata maisha kwa ujumla na ukaweza kupiga hatua kubwa.
Na njia ya wewe kuweza kutumia njia hii ya ufanyaji iko wazi, angalia wale ambao wamefanikiwa sana kwenye kile unachotaka kufanikiwa pia, jua ni vitu gani wanafanya tofauti, ambavyo wengine hawafanyi, jua ni taswira zipi wamejijengea kiakili na kisha fanya kama wao, jijengee taswira kama walizonazo wao. Baada ya kujua kile cha tofauti na jinsi ya kukifanya, unapaswa kuwa na mtu wa nje wa kukusimamia na kukusukuma zaidi. Na hapa unahitaji kuwa na mwalimu, kocha au hata mshauri ambaye ana uelewa juu ya kile unachotaka kubobea, ambaye anaweza kukufuatilia kwa karibu.
Hatua hizi mbili kila mtu anaweza kuzichukua kwenye lolote analotaka kubobea kwenye maisha yake, kazi ni kwako kuchukua hatua.
TANO; KUFANYA KWA MAKUSUDI KWENYE KAZI.
Kumekuwa na makosa makubwa sana yanayofanyika kwenye mfumo wa elimu, ambao unapaswa kuwaandaa watu kuwa wafanyaji wa kazi, lakini mpaka mtu anahitimu, anakuwa hajapata ujuzi atakaotumia kwenye kazi. Badala yake anamaliza akiwa na maarifa mengi sana kuhusu kazi anayopaswa kufanya, lakini ujuzi hakuna.
Mfumo wa elimu unaegemea zaidi kwenye kutoa maarifa, kwa kuwa maarifa ni rahisi kufundisha kwa watu wengi na kwa pamoja. Lakini unasahau eneo la ujuzi ambalo ndiyo muhimu zaidi. Kufundisha ujuzi ni kugumu kwa sababu inahitaji anayefundisha na anayefundishwa wafanye kazi kwa pamoja. Ndiyo maana zamani watu walikuwa wakijifunza kutoka kwa wabobezi na walipata ujuzi bora. Lakini wale wanaohitimu, wanakuwa na maarifa mengi, lakini ujuzi kidogo.
Hivyo kama unataka kubobea kwenye kazi yoyote unayofanya, jukumu lako ni moja, kujijengea ujuzi zaidi. Angalia wale waliofanikiwa kwenye kazi hiyo ni vitu gani wanafanya na namna wanavyovifanya kwa utofauti, kisha jifunze kufanya vitu hivyo na fanya kwa ubora zaidi. Itasaidia sana pale unapokuwa na menta au msimamizi kwenye kazi ambaye ana ubobezi mkubwa na yeye atakuwezesha wewe kubobea pia.
Na kwa kila hatua unayotaka kuchukua ya kukuwezesha kubobea zaidi, jiulize maswali haya muhimu;
Je inakusukuma kuondoka kwenye mazoea? Kufanya ulichozoea hakuwezi kukupa ubebozi.
Je unapata mrejesho wa haraka kwa hatua unazopiga? Mrejesho ndiyo unakuonesha ni wapi unapatia na wapi unakosea.
Je wapo watu ambao wameweza kufanya kwa ubora wa hali ya juu na kubobea? Hawa ndiyo utakaojifunza kwao.
Je kuna ujuzi ambao utajifunza kupitia kile unachofanya? Ujuzi ndiyo unaleta ubobezi, na siyo maarifa pekee.
SITA; KUFANYA KWA MAKUSUDI KWENYE MAISHA YA KILA SIKU.
Kufanya kwa makusudi hakujatengwa kwa wale wanaotaka kubobea kwenye michezo au sayansi pekee, bali ni kitu ambacho kila mtu anaweza kukitumia kwenye maisha yake ya kawaida. Iwe unataka kuwa mzazi bora, mwenza bora, mwandishi, muuzaji na mambo mengine kwenye maisha, kufanya kwa makusudi kutakuwezesha kupiga hatua zaidi.
Hatua ya kwanza na muhimu ni kuchagua eneo ambalo unataka kubobea, huwezi kubobea kwenye kila eneo, hivyo chagua moja au machache.
Baada ya hapo waangalie wale ambao wamebobea kwenye eneo hilo, wanafanyaje na ni taswira zipi za kiakili wanazo, jifunze namna wanavyofanya na jijengee taswira za kiakili utakazotumia kwenye ufanyaji wake.
Unahitaji kutafuta mwalimu au kocha ambaye atakusimamia, ambaye analielewa eneo hilo na hivyo anaweza kukupa mrejesho wa haraka na kukurekebisha pale unapokosea.
Katika ufanyaji, unapaswa kuweka akili na mawazo yako yote pale. Kama akili yako inazurura, kwa mawazo kuwa sehemu nyingine wakati unafanya, huwezi kutengeneza ubobezi. Hivyo unapaswa kutenga muda ambao hakuna usumbufu mwingine wowote na kuweka akili na nguvu zako zote kwenye kile unachofanya. Kufanya kitu kwa umakini huu kwa saa moja pekee kutakuwezesha kupiga hatua kuliko kufanya kwa masaa matatu huku ukiwa na usumbufu.
Kama huwezi kupata mwalimu au kocha wa kukuongoza, basi vipo vitu vitatu ambavyo unapaswa kuvizingatia. Kitu cha kwanza ni kujilazimisha kuweka umakini wako kwenye kile unachofanya (FOCUS), kitu cha pili ni kuweka mfumo ambao utakupa mtejesho wa haraka, ili kujua kama unapiga hatua au la (FEEDBACK) na kitu cha tatu ni kujirekebisha haraka pale unapogundua umetoka nje ya lengo au umekosea (FIX IT). Ukizingatia vitu hivi vitatu, utaweza kufikia ubobezi kwenye chochote ulichochagua kufanya.
Ili kujisukuma kufanya nje ya mazoea yako na kutokuishia njiani, unapaswa kuwa na sababu za kufanya na sababu za kuacha. Sababu za kufanya ni zile zinazokusukuma wewe kufanya na sababu za kuacha ni zile zinazokuvutia kuacha. Ili kutokuacha, unapaswa kuimarisha sababu za kuendelea kufanya na kudhoofisha sababu za kuacha. Bila ya kufanya hili, hutaweza kupiga hatua. Angalia mwanzo wa mwaka jinsi watu wengi wanavyoweka malengo makubwa lakini haichukui muda wanaachana nayo. Hii ni kwa kuwa wanaruhusu sababu za kuacha ziwe na nguvu kuliko sababu za kuendelea kufanya.
SABA; NJIA YA KUELEKEA KWENYE KILELE CHA UBOBEZI.
Zipo hatua nne ambazo watu wanapitia katika kuelekea kwenye kilele cha ubobezi kwenye chochote ambacho wanakifanya. Njia hii inafanana kwa wote hivyo ni muhimu kuijua na kujua upo kwenye hatua ipi na wapi unapaswa kupita ili kufika kwenye ubobezi huo wa hali ya juu.
Hatua ya kwanza ni KUKUTANA NA KITU. Hapa ni pale mtu anapokutana na kitu ambacho kinamvutia na anapenda kukifanya. Hapa mtu anavutiwa na kitu kuliko wengine wanavyovutiwa nacho, na kutaka kukifuatilia kwa undani zaidi. Hapa mtu anaonesha dalili za kutaka kuwa bora kwenye kitu hicho na kufanikiwa zaidi. Atatumia muda mwingi kufuatilia na kuzungumzia kitu hicho kuliko wengine wanavyotumia muda kwenye kitu hicho.
Hatua ya pili ni KUWEKA UMAKINI. Hapa mtu anaanza kuweka umakini katika ufanyaji wa kitu hicho. Kwa bahati anakuwa amekutana na ufanyaji wa makusudi, labda amejifunza kuhusu mtu aliyefanikiwa sana kwenye kitu hicho na jinsi alivyofanya kwa tofauti na yeye akaanza kufanya. Wengine wanatafuta kabisa mwalimu au kocha na kuanza kujifunza kutoka kwao. Hii ni hatua ambayo wale anaobobea wanajitofautisha na wale wanaoishia kuwa washabiki wa kitu husika.
Hatua ya tatu ni KUJITOA KWELI. Hapa mtu anajitoa kweli na kuweka dhamira ya kuwa mbobezi kwenye kile anachofanya. Hapa mtu anakuwa ameanza kupata mafanikio kwa kuweka umakini, na mafanikio hayo yanamfanya aone anaweza kufanya zaidi. Katika kujitoa kweli, mtu anawekeza kila alichonacho kwenye kile anachofanya. Anatafuta mwalimu bora zaidi na anaweza kuondoka eneo moja na kwenda jingine ili aweze kupata nafasi ya kuwa bora zaidi. Hatua ya kujitoa ndiyo inawasukuma zaidi wale wanaofikia kilele cha juu kabisa cha ubobezi.
Hatua ya nne ni WATENGENEZA NJIA. Hapa mtu anakuwa amefikia viwango vya juu sana kwenye ufanyaji, anatengeneza viwango vipya ambavyo vinabadili kabisa kile ambacho anafanya. Hapa ni kama mtu anatengeneza njia mpya, anakuja na ufanyaji mpya, ambao haukuwepo kabisa. Kwa yeye kufikia ubobezi huo na kufanya kwa utofauti mkubwa, inawalazimu wengine wote kufanya kama yeye. Hapa ndipo mtu anapoweka rekodi mpya ambayo wengine wote wanakazana kuivunja. Au mtu anakuja na njia mpya ya ufanyaji wa kitu ambayo inakuwa ndiyo njia wengine wanaitumia kufanya. Hatua hii ya utengenezaji wa njia inamtaka mtu kwenda juu zaidi ya mazoea, kwenda tofauti na walimu wake na kuja na kitu kipya.
Angalizo, hatua hizi nne zinafuatana, ni vigumu sana kuanza na kitu na moja kwa moja ukafikia hatua ya kutengeneza njia. Lazima kwanza ubobee kwenye njia walizotengeneza wengine kabla hujatengeneza njia yako mwenyewe. Na hata wanasayansi ambao wameonekana kuja na kanuni mpya za kisayansi, walibobea kwanza kwenye kanuni za kisayansi za wanasayansi wengine kabla hawajatengeneza kanuni zao. Hivyo usitafute njia ya mkato, badala yake fuata hatua na weka juhudi na muda na utaweza kufikia ubobezi mkubwa kwenye kile unachofanya.
NANE; VIPI KUHUSU VIPAJI ASILI?
Kama tulivyojifunza kwenye utangulizi, katika neno la juma, kinachowafikisha watu kwenye ubobezi siyo kipaji bali juhudi. Wale waliobobea wameweka kazi na juhudi kubwa kwa miaka mingi kabla hawajafika pale walipo sasa. Hakuna yeyote ambaye ameweza kupita njia ya mkato kufikia ubobezi.
Watu wanapenda kuamini kwamba kuna miujiza katika maisha, kwamba wapo watu waliozaliwa na uwezo mkubwa wa kukariri vitu au uwezo mkubwa wa mwili kuweka juhudi kubwa. Lakini tafiti zinaonesha hicho kitu hakipo. Hata wale wanaoonekana kuwa na kipaji au uwezo wa kipekee, kinachoonekana ni walipata nafasi au tuseme bahati ya kuanza wakiwa wadogo ukilinganisha na wengine.
Mfano mzuri ambao mwandishi anatupa ni wazazi ambao tangu wanachumbiana, mwanaume alimwambia mwanamke kwamba lengo lake ni kuwa na watoto waliobobea na kushika nafasi za juu duniani. Na walipata watoto watatu, na wote walianza kuwafundisha wakiwa wadogo sana mchezo wa chess, na watoto wote watatu waliweza kufikia viwango vya juu sana kwenye mchezo wa chess. Kinachofanya hili liwe la tofauti ni kwamba watoto wao wote watatu walikuwa wa kike, na kwa kipindi hicho, chess ulionekana kuwa mchezo wa wanaume. Lakini kwa kuanza kuwafundisha wakiwa wadogo, kati ya miaka miwili mpaka minne, walipokuja kufika miaka 16 mpaka 20 walikuwa wamevunja rekodi nyingi duniani.
Hivyo kile tunachoita uwezo au kipaji, ni muendelezo wa kile ambacho kipo ndani ya kila mtu, ila unakuwa umeanza mapema. Na kama hukupata nafasi ya kuanza mapema, unaweza kuanza sasa, lakini jipe vitu viwili, kuwa tayari kuweka juhudi kubwa na kuwa na subira kwa kuwa itakuchukua muda mrefu mpaka kufikia ubobezi.
TISA; HATUA ZA KUCHUKUA BAADA YA HAPA.
Kama tulivyojifunza, kufanya kwa makusudi (deliberate practice) ndiyo msingi mkuu wa ubobezi kwenye chochote ambacho tunachagua kufanya, tunapaswa kuuchagua kufanya kwa makusudi yale yote ambayo tunataka kubobea. Tunapaswa kuachana na mazoea na kutengeneza msukumo ambao utatuwezesha kupiga hatua zaidi. Hatua zote muhimu tumeshajifunza, kazi kwetu ni kuchukua hatua.
Wote tunajua ya kwamba dunia inabadilika kwa kasi sana, sayansi na teknolojia zinabadili kila kitu. Kuna kazi ambazo miaka kumi iliyopita zilikuwa zinalipa sana, lakini kwa sasa hazipo kabisa. Na zipo kazi ambazo kwa sasa zinaonekana kulipa mno, lakini miaka kumi ijayo hazitakuwepo kabisa.
Njia pekee ya kuvuka salama kwenye nyakati hizi za mabadiliko ni kuchagua kuwa mbobezi kwenye chochote unachofanya. ubobee kwa namna ambayo hakuna mwingine anayeweza kufanya kama wewe, ubobee kiasi kwamba hakuna kompyuta inayoweza kufanya kama wewe.
Na hilo linawezekana kama mtu utachagua eneo unalotaka kubobea na kuweka kazi na muda. Lakini pia kwa kuwa mambo yanabadilika, ukishabobea eneo moja usikubali mazoea yaingie, badala yake endelea kujiboresha zaidi kiasi kwamba mambo yanapobadilika, wewe unakuwa mbele ya mabadiliko.
Pia kwa watoto wetu, tunapaswa kuwajengea msingi wa ubobezi mapema, tafiti zinaonesha watoto wanaoanza kufanya kitu wakiwa na umri chini ya miaka 6, baada ya miaka kumi wanakuwa na ubobezi mkubwa sana. Hivyo kama una watoto wadogo na unataka kuwasaidia kufanya makubwa hapa duniani, anza kuwajenga msingi wa ubobezi wakiwa bado ni wadogo. Chini ya miaka 6 ni bora, lakini kama wamezidi hapo pia ni bora kuanza mapema kabla hawajafikia utu uzima.
Rafiki, hivi ndivyo tunavyoweza kubobea kwenye chochote ambacho mtu unakuwa umechagua kufanya. Misingi na hatua zote muhimu umejifunza kwenye kitabu hiki, kazi ni kwako kuchukua hatua ili kubobea. Pia wasaidie watoto wako na wengine wanaoweza kujifunza kwako kubobea zaidi.
#3 MAKALA YA JUMA; HATUA NNE ZA KUJIJENGEA UZOEFU BORA.
Kwenye kila eneo la maisha, iwe ni kazi, biashara, elimu na hata michezo, kuna watu wawili ambao wanaweza kuonekana wameanzia hatua sawa ya chini na wanafanya kila kitu kwa kufanana, lakini kuna mmoja akapiga hatua sana huku mwingine akabaki chini.
Ni tofauti hii ya matokeo ambayo hupelekea watu kuamini kwamba wale wanaopiga hatua wana kipaji ambacho wale wanaoshindwa kupiga hatua hawana. Kwa sababu utaelezeaje hali hiyo, watu wawili, wanafanya kitu kimoja, wanaweka juhudi ambazo zinaonekana kufanana, lakini mmoja anabobea na mwingine anabaki kuwa kawaida?
Kwenye kitabu chetu cha juma, mwandishi anatuambia haitoshi tu kuweka juhudi, bali ni aina gani ya juhudi ambazo mtu anaweka ndiyo inaamua kama mtu atabobea au la. Kwamba hata kama kwa nje watu wanaonekana kuweka juhudi sawa, kuna tofauti kubwa kwa ndani kwenye aina hiyo ya juhudi wanazoweka.
Mwandishi ameanisha aina tatu za juhudi, aina moja iliyozoeleka na wengi ambayo inawafanya waishie kuwa kawaida, na aina nyingine mbili ambazo zinawawezesha watu kupiga hatua zaidi na kubobea.
Kwenye makala ya juma hili, nimekuchambulia aina ya pili ya juhudi, ambayo ndiyo inawatofautisha sana wanaopiga hatua na wanaobaki pale pale. Kama hukusoma makala hii nzuri, yenye hatua nne unazopaswa kuchukua kwenye juhudi unazoweka ili ufanikiwe sana, fungua hapa kuisoma; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kujijengea Uzoefu Mkubwa Kwenye Kile Unachofanya Na Kuweza Kufanikiwa Sana.
Endelea kutembelea www.amkamtanzania.com kila siku na www.kisimachamaarifa.co.tz kila siku kuendelea kupata makala nzuri za kukuwezesha kupiga hatua zaidi.
#4 TUONGEE PESA; UBOBEZI KATIKA FEDHA.
Rafiki, kwenye eneo la fedha unaweza kufikia ubobezi kama unavyoweza kufikia kwenye maeneo mengine. Na kwa kuwa fedha ni eneo muhimu sana kwenye maisha yetu, nashauri kila mmoja wetu ajijengee ubobezi kwenye eneo hili la fedha.
Na hatua za ubobezi kwenye fedha hazina tofauti na hatua za ubobezi tulizojifunza.
Kwanza kabisa lazima ujue wapi unataka kufika kifedha, na uwe na lengo la uhakika la kifedha. Lengo lisiwe tu kuwa na fedha nyingi, au kuwa bilionea, badala yake unapaswa kuwa na namba kamili ya kiasi cha fedha unachotaka kufikia.
Hatua ya pili ni kuwaangalia wale ambao wameshafikia lengo hilo la kifedha, kama lengo ni kuwa na bilioni tano, angalia wale wenye bilioni tano na kuendelea. Angalia vitu gani vya tofauti wanafanya, angalia na jifunze mtazamo na taswira za kifedha walizojijengea kwenye akili zao. Uzuri ni kwamba vitabu vingi sana vimeshaandikwa kwenye eneo hili, hivyo ni wewe kujifunza.
Hatua ya tatu kuwa na mwalimu, menta, kocha au mashauri wa karibu ambaye ataendelea kukusukuma pale unapotaka kukata tamaa na kurudi nyuma. Safari haitakuwa rahisi, bila ya kuwa na mtu wa nje wa kukusukuma, hutaweza kufikia lengo lako hilo kubwa la kifedha.
Hatua ya nne ni kuwa na mpango na kuanza kuufanyia kazi. Baada ya hatua zote tatu za juu kukamilika, weka mpango wako wa kufika kwenye ubobezi wa kifedha na fanyia kazi mpango huo. Mpango huo uwe na njia ya kujipima na kupata mrejesho wa namna unavyokwenda. Pia shirikiana kwa karibu na mwalimu, menta au kocha uliyemchagua ili aweze kukupa mbinu za kuvuka changamoto mbalimbali unazokutana nazo.
Hatua ya tano ni kuwa na uvumilivu na subira, mambo hayatatokea haraka, itakuchukua muda na safari itakuwa ndefu. Kama unafikiria kulala masikini na kuamka tajiri, kama unafikiria ipo siri au njia za mkato ambazo ukitumia utafikia lengo haraka unajidanganya. Ukishachagua mpango unaofanyia kazi, weka umakini wako wote hapo, sahau vitu vingine vyote. Watu wakija kwako na fursa wanazokuambia ni za haraka za kutajirika usihangaike nazo, wewe kazana na mpango wako.
Rafiki, fuata hatua hizo tano na utaweza kufikia ubobezi wa kifedha na kuwa na utajiri na uhuru wa kifedha kwenye maisha yako.
#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; UMUHIMU WA KUWA NA MWALIMU AU KOCHA.
“The best way to get past any barrier is to come at it from a different direction, which is one reason it is useful to work with a teacher or coach.” ― Anders Ericsson
Wachezaji wote wakubwa na wenye mafanikio makubwa, wana makocha ambao wanawasimamia kwa karibu. Wajasiriamali wote wenye mafanikio makubwa wana makocha na washauri wa karibu wanaowategemea sana. Na hata viongozi wa nchi na mashirika makubwa duniani, wana washauri na makocha ambao wanawategemea sana.
Unapokutana na changamoto kwenye maisha, ni vigumu kuivuka kwa kutumia fikra na mbinu zako mwenyewe. Kwa sababu mara nyingi unajikuta ukifanya kile ambacho umezoa kufanya mara zote, na hilo linapelekea kupata matokeo yale yale.
Kama ambavyo Anders Ericsson anatuambia kwenye tafakari hiyo hapo juu, njia bora ya kuvuka kikwazo unachokutana nacho, ni kukiendea kwa njia ya tofauti, na ndiyo sababu ni muhimu sana kuwa na mwalimu au kocha. Kwa sababu kwa kutumia uzoefu na mbinu zako mwenyewe, ni vigumu kuona njia ya tofauti ya kuliendea jambo. Lakini unapokuwa na kocha au mwalimu, inakuwa rahisi kwake kukuonesha ipi njia ya tofauti unayoweza kuitumia.
Je wewe una kocha au mwalimu unayemtegemea kwenye maamuzi mbalimbali unayofanya kwenye kazi zako, biashara na maisha yako? Kama huna unajikwamisha wewe mwenyewe kufanikiwa, kwa sababu kuna mambo unayafanya vile vile kila mara na hupati matokeo ya tofuati.
Kama hujaanza kutumia huduma zangu za ukocha, anza kuzitumia sasa ili uweze kufanya maamuzi bora na kupiga hatua kwenye maisha yako. Huduma zote za ukocha ninazotoa zinapatikana hapa; www.amkamtanzania.com/kocha
#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.
Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.
Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.
Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.
Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.
Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.
Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.
Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)
Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha
Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu