Rafiki yangu mpendwa,

Nilishakuambia ya kwamba hutafanikiwa kwa kukazana kuboresha madhaifu yako, badala yake utafanikiwa kwa kutumia vizuri uimara ambao tayari unao.

Ninachomaanisha ni kwamba, kama kuna eneo ambao una udhaifu, ukikazana kulifanya kuwa bora, utatumia nguvu nyingi na hutakuwa bora sana. Lakini kama utatumia nguvu hizo kwenye eneo ambalo tayari una uimara, utafanikiwa zaidi.

Lakini pia, haimaanishi unapaswa kuyapuuza kabisa maeneo ambayo una udhaifu, haimaanishi kwamba huhitaji kuyajua au unapaswa kujidanganya kwamba huna madhaifu.

Kila mtu ana madhaifu, na wale ambao wanayajua na kuyakubali madhaifu yao, inakuwa rahisi zaidi kwao kuweza kufanikiwa zaidi, kwa sababu hawatapoteza muda na nguvu nyingi kwenye madhaifu hayo, badala yake watawekeza kwenye yale maeneo ambayo tayari wapo imara.

Changamoto kubwa inayowazuia wengi wasiyajue madhaifu yao ni ile hali ya kuanguka kwenye mapenzi mazito kwa chochote ambacho mtu anakuwa anafanya au kwenye hali fulani.

Ulishawahi kusikia kauli ya waswahili kwamba mapenzi ni upofu? Kitu chochote ambacho unakuwa na mapenzi makubwa nacho, huwezi kamwe kuona madhaifu yake. Watu watakuambia wazi lakini mbona hapo pako hivi, wewe utakataa na kuwaambia watu hao hawaoni vizuri. Ni mpaka pale mapenzi hayo makali yanapotulia ndipo unaweza kuona kwa uhalisia.

NUFAIKA NA MABADILIKO

Mapenzi ya dhati au kwa lugha nyingine mahaba, ni kikwazo kikubwa kwa wengi kuyajua na kuyafanyia kazi madhaifu ambayo wanayo. Kwa sababu kwa kujipenda sana wao, au kupenda kile wanachofanya au hali waliyokuwa nayo, wanashindwa kuona kile ambacho kipo wazi kabisa.

Hapa siyo kwamba nakuambia usiwe na mapenzi ya dhati kwa chochote, lakini unapaswa kuwa makini, unapaswa kujipa nafasi ya kuweka mapenzi na mahaba yako pembeni na kuangalia kitu kwa jicho la uhalisia, jicho ambalo yeyote anaweza kulitumia.

Hili lina changamoto, kwa sababu linatutaka kwenda kinyume na asili yetu sisi binadamu. Kwa sababu sisi binadamu ni viumbe wa hisia, huwa tunafanya maamuzi mengi kwa kuendeshwa na hisia na siyo kwa kuendeshwa na fikra sahihi.

Lakini unahitaji kufanya hivyo, unahitaji kujua wakati gani wa kuweka hisia pembeni ili kuweza kuona kila unachopaswa kukiona. Siyo zoezi rahisi, lakini lina manufaa makubwa, litakuwezesha kuuona uhalisia, litakufanya uache kujidanganya na kuweza kuchukua hatua sahihi za kukuwezesha kupata chochote unachotaka.

SOMA; Njia Tatu Za Kukulazimisha Kufanya Kile Unachojua Unapaswa Kufanya Lakini Hujisikii Kufanya.

Ukishajua madhaifu yako, ukajua ukomo wako, ni rahisi kwako kuchukua hatua sahihi ili madhaifu hayo yasiwe kikwazo kwako.

Kwa mfano kama upo kwenye biashara, ukishajua ni eneo gani upo imara na lipi una udhaifu, unakazana kufanyia kazi lile eneo ambalo uko imara na kutafuta watu wa kukusaidia kwenye lile eneo ambalo una udhaifu.

Unapotafuta watu wa kushirikiana nao, angalia wale watu ambao wana uimara kwenye yale maeneo ambayo wewe una udhaifu na wewe una uimara kwenye yale maeneo ambayo wao wana udhaifu. Kwa njia hiyo mtatengeneza timu nzuri itakayoweza kufanya makubwa.

Lakini kama mtakutana watu ambao mna uimara eneo moja, na mna udhaifu maeneo yanayofanana, kitakachotokea ni majanga. Kwanza kwenye lile eneo ambalo wote mna uimara mtaanza kushindana, nani imara zaidi, hata kama haitakuwa wazi basi itakuwa kwa chini chini. Halafu yale maeneo ambayo mna udhaifu wote mtayaepuka. Hivyo hamtaweza kupiga hatua yoyote kwenye ushirikiano wetu huo.

Ni muhimu sana kujua udhaifu wako kwenye kila eneo la maisha yako, ili kuhakikisha unawekeza muda na nguvu zako kwenye lile eneo ambalo tayari una uimara kuweza kufanikiwa. Na hata inapokuja kwenye kushirikiana na wengine, kujua udhaifu na uimara wako, na kujua udhaifu na uimara wa wengine kutakusaidia sana.

KARIBU KWENYE SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018.

Rafiki, nakukumbusha kuhusu SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, ambayo itafanyika jumamosi ya tarehe 03/11/2018 jijini dar es salaam.

Kwenye semina hii tutajifunza na kuhamasika na kuweza kuweka mikakati ya mafanikio makubwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla.

Ada ya kushiriki semina hii ni tsh 100,000/= na mwisho wa kulipa ada hii ni tarehe 31/10/2018.

Malipo ya ada yanafanyika kwa namba 0755 953 887 au 0717 396 253 ukishalipa tuma ujumbe wenye majina yako na namba ya simu kwenye namba 0717396253 na utapewa maelekezo zaidi.

Karibu sana kwenye nafasi hii ya kipekee ya sisi kukutana pamoja kama wanamafanikio na kujifunza pamoja na kuhamasika ili kuweza kufanya makubwa zaidi.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu