Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari TABIA YAKO HALISI…
Tabia yako halisi utaijua wakati ambapo unapitia magumu kwenye maisha yako.
Wakati unapitia mazuri, wakati ambapo huna changamoto na kila kitu kinaenda kama unavyopanga, ni rahisi sana kuigiza maisha na kuona mambo ni rahisi.

Ni pale ambapo mambo yanakuwa magumu sana, pale ambapo umekutana na changamoto kubwa na ngumu, pale ambapo unaona kila kitu hakiendi, hapo ndipo unapoijua tabia yako halisi.

Wakati wa magumu ndiyo wakati unaoweza kupima imani yako binafsi, misimamo yako na vipaumbele vyako. Pia ndiyo wakati unaoweza kupima mahusiano yako na wengine.

Wakati mwingine tunapitia magumu kwenye maisha yetu, ili tuweze kujifunza kuhusu sisi wenyewe.
Hivyo unapokuwa unapitia ugumu, usiishie tu kulalamika kwamba mambo yako hayaendi, bali angalia unajitengeneza kuwa mtu wa aina gani.

Utajijua vizuri sana wakati unapopitia ugumu kwenye maisha yako, hivyo unapokuwa kwenye ugumu, ambao lazima kila mtu apitie, tumia nafasi hiyo kujijua vizuri na pia kujitengeneza kuwa imara.

Kila mtu anaweza kujiita au kujiambia chochote pale mambo yanapokwenda vizuri. Pale kila kitu kinavyoenda kama unavyotaka unaweza kujioma tayari umeweza kila kitu. Ni rahisi kufanya kwa mazoea wakati kama huo. Na hapo ndipo mtu unapoyakaribisha magumu wewe mwenyewe.
Kwa sababu unakuwa umejisahau sana, magumu yanakuja kukumbusha tabia zako halisi na uweze kuyaona mambo kwa uhalisia wake na uache kujidanganya.

Kama ambavyo chuma kinapitisha kwenye moto ili kusafishwa na hata kufanya imara, wewe pia unapitia magumu ili kusafishwa na kuwa imara. Unapopitia magumu unajua kila ukweli kuhusu wewe, na ukifanyia kazi ukweli huo utaweza kupiga hatua sana.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujifunza, kujijua na kuimarika zaidi kwa kila ugumu unaopotia kwenye kila sikj yako.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha