Rafiki yangu mpendwa,
Mkulima yeyote anayeweka nguvu na rasilimali zake kulima shamba, anakuwa anaamini kwamba shamba hilo ni sahihi kwake na litaweza kumpatia mazao anayoyataka. Kwa kuamini hivyo, anakuwa tayari kuwekeza nguvu, muda na hata fedha kuhakikisha shamba linakuwa bora kwa ajili ya kutoa mazao mazuri.
Hii ndiyo tabia ya asili kwetu binadamu, huwa tunawekeza kwenye vile vitu ambavyo tunaviamini, vile vitu ambavyo tunajua havitatuangusha. Na chochote ambacho tunafanya uwekezaji ndani yake, kinakua na hata kufanikiwa sana. Kama wanavyosema kwenye kilimo, jembe huwa halimtupi mkulima.
Tunaweza kutumia vizuri dhana hiyo ya uwekezaji kwenye mafanikio yetu makubwa. Kama unataka kufanikiwa sana kwenye maisha yako, lazima ufanye uwekezaji mkubwa sana ndani yako. Na ili uweze kufanya uwekezaji mkubwa ndani yako, lazima kwanza uamini ndani yako, lazima uamini ndani yako upo uwezo wa kufanya makubwa. Kama ambavyo mkulima anavyoamini kwenye ardhi anayoilima.
Kama unaamini ndani yako, kama unaamini kesho yako inaweza kuwa bora zaidi ya leo yako, utafanya uwekezaji mkubwa ndani yako na kwenye uwezo wako. Utajifunza na kukazana kuwa bora sana kwa sababu unajua kuna kitu ndani yako kinachoweza kufanya makubwa zaidi.
Na kadiri unavyoendelea kuwekeza ndani yako, ndivyo unavyozidi kuamini ndani yako. Kwa hiyo vitu hivi viwili; kujiamini na kuwekeza ndani yako vinasukumana. Kadiri unavyojiamini ndivyo utakavyowekeza ndani yako, na kadiri unavyowekeza ndani yako ndivyo unavyozidi kujiamini.
Amini ndani yako rafiki, amini kwamba unao uwezo wa kufanya makubwa, amini kwamba unao uwezo mkubwa wa kipekee, na siyo tu unaamini ili kujiridhisha, bali ndiyo ukweli wenyewe kuhusu maisha yako.
Ukishaamini ndani yako, fanya uwekezaji mkubwa sana ndani yako. Fanya uwekezaji kwenye akili yako kwa kujifunza kila siku, fanya uwekezaji kwenye mwili wako kwa kuzingatia kanuni za afya bora, na pia fanya uwekezaji kwenye roho yako kwa kujijengea imani imara unayoishi nayo.
Kadiri unavyowekeza ndani yako, ndivyo unavyozidi kukua na kufanikiwa zaidi. Uwekezaji wa kwanza muhimu mno unaoweza kufanya kwenye maisha yako, ni uwekezaji wa ndani yako mwenyewe.
SOMA; Huu Ndiyo Uwekezaji Unaolipa Kwa Riba Kubwa Duniani
Hamisha uwekezaji unaofanya maeneo mengine kwenda uwekezaji wa ndani yako binafsi.
Watu wengi wanaposikia kuwekeza ndani yao wenyewe, huwa hawaelewi wanaanzaje uwekezaji huo. Na pale wanapogundua kwamba zipo gharama kwenye kuwekeza ndani yao binafsi, mfano kununua vitabu, kulipia gharama za kuwa na kocha na hata kuzingatia afya bora, huona hawana fedha za kuwekeza maeneo hayo.
Lakini kila mtu ana fedha za kuwekeza ndani yake binafsi, kwa sababu kila mtu tayari kuna maeneo anayowekeza.
Kwa mfano kama una gari, au chombo chochote cha usafiri, mara kwa mara utakuwa unakifanyia matengenezo na kukifanya kuwa bora zaidi. Jaribu kupiga mahesabu kwa mwaka mzima ni kiasi gani cha fedha unachotumia kutengeneza na kuboresha chombo chako cha usafiri, kisha wekeza kiasi kama hicho kwenye maendeleo yako binafsi. Utaweza kupiga hatua kubwa sana.
Chukua pia mfano wa nyumba, kama unamiliki nyumba, kila mwaka kuna matengenezo na marekebisho unayofanya ndani ya nyumba yako. Huo ni uwekezaji ambao unaufanya kwenye nyumba, kama utapeleka uwekezaji sawa na huo kwako binafsi, utaweza kupiga hatua kubwa sana.
Mwisho angalia mwili wako mwenyewe, kuna uwekezaji mkubwa sana unaofanya kwenye mwili wako ili uonekane kwa nje. Kuanzia mavazi unayonunua, usafi na urembo unaoweka kwenye mwili wako, ukitumia kiasi hicho hicho kuwekeza ndani yako, utapiga hatua sana. Kwa mfano ukajiwekea utaratibu kwamba kabla hujanunua nguo mpya basi inabidi kwanza ununue kitabu kipya cha kusoma na kujifunza, utaweza kununua vitabu vingi sana na kujifunza mengi. Angalia nguo zote ulizonazo halafu jiulize kama ungekuwa umenunua kitabu kwa kila nguo uliyonayo ungekuwa na vitabu vingapi?
Uwekezaji ambao tayari sasa unaufanya kwenye maeneo mengine ya maisha yako, ndiyo uwekezaji huo huo unapaswa kuufanya ndani yako binafsi ili uweze kufanikiwa sana.
Amini ndani yako na wekeza zaidi ndani yako, hakuna kitakachoweza kukuzuia wewe kufanikiwa ila wewe mwenyewe.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL