Hakuna kitu cha hovyo, kinachopoteza muda na nguvu za watu kama mabishano.
Kwa sababu baada ya mabishano hakuna matokeo yoyote ya tofauti ambayo mtu unayapata.
Chukulia mfano wa mabishano ya kawaida kwenye mambo ambayo yana pande mbili, labda vyama vya siasa, dini, michezo na kadhalika, hata watu wabishaneje, kila mtu ataendelea kusimama upande aliokuwa. Hata kama mtu ataoneshwa ni jinsi gani upande aliopo siyo sahihi, bado ataendelea kusimama upande huo.
Sasa kama baada ya mabishano, kila mtu ataendelea kuamini kile alichokuwa anaamini, mabishano hayo yanakuwa yamesaidia nini? Ni upotevu wa muda pekee, hakuna zaidi ya hapo.
Hivyo mwanamafanikio, moja ya jambo muhimu unalopaswa kufanya kila siku kwenye maisha yako ni kuepuka mabishano kadiri uwezavyo.
Kama kuna kitu unataka kujifunza, mtafute mtu mwenye kukijua na kisha jifunze. Kama unavyoamini ni tofauti na wengine wanavyoamini, jua imani ipi unayoihitaji ili kufikia ndoto zako kubwa, kama ni ile uliyonayo endelea nayo na waache wengine waendelee na imani zao. Kama imani waliyonayo wengine ndiyo pia unayohitaji ili kuweza kufikia ndoto zako basi jifunze na ishi imani hiyo.
Mabishano mengi ambayo watu huwa wanaingia, ni kutaka kujionesha kwamba wao wapo sahihi kuliko watu wengine. Na hicho ni kitu ambacho hakipo, kila mtu yupo sahihi kulingana na imani yake na taarifa alizonazo. Hivyo kusema kwamba wewe upo sahihi zaidi ya wengine, na kutaka wengine wakubaliane na hilo, ni kutaka kusumbuana tu na wengine.
Kadhalika kama umekosea mtu, usitake kuingia kwenye malumbano kwamba nani amekosea na nani yupo sahihi, au kwa nini yeye alianzisha kitu fulani kilichopelekea umkosee. Kama umemkosea mtu, omba samahani na tatua kile ulichokosea kisha songa mbele. Hii itakuokolea muda wako, itaimarisha mahusiano yako na utaweza kuzingatia yale ambayo ni muhimu zaidi.
Usipoteze muda wako wa thamani kwa vitu ambavyo havitakubadili wewe wala wengine. Epuka mabishano ambayo watu tayari wana upande wao na wana imani kubwa juu ya ule upande waliopo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,