Hivi ni vitu viwili ambavyo ni tofauti sana, lakini watu wengi wamekuwa hawavielewi kwa undani, na hilo linawapelekea kuingia kwenye matatizo makubwa.

Watu wengi wanaponunua au kuuza vitu, huwa wanakazana kuangalia gharama na bei, na siyo kuangalia thamani. Wanapoangalia gharama, wanafanya maamuzi kwa namna ambavyo wanaona wanaweza kumudu gharama hizo, lakini wanasahau kitu muhimu zaidi ni thamani.

Gharama na thamani kwenye kununua.

Kwa upande wa kununua, watu wengi hupenda kununua vitu ambavyo gharama yake ni ya chini, yaani bei yake ni ndogo, bila ya kuangalia thamani halisi wanayoipata kwa kile wanacholipia.

Kwa uhalisia, vitu ambavyo bei yake ipo chini, huwa pia vina thamani ndogo. Hivyo mtu anayekazana kununua vitu kwa kuangalia gharama ndogo, anaishia kuwa na vitu ambavyo vina thamani ndogo, siyo imara na vinahitaji gharama zaidi ili mtu aweze kutumia.

Ukiona kitu kinauzwa kwa bei ndogo au gharama zake zipo chini, jua kuna namna wewe unayenunua utalipa gharama zaidi. Labda kitu hicho hakitakufaa sana kwa na namna ulivyotaka. Labda kitu hicho hakitadumu sana na hivyo utahitaji kuingia gharama tena kununua kingine.

Jaribu kufanya tathmini kwenye maisha yako, kama kuna kitu cha bei rahisi umewahi kununua na kikadumu kweli au kikakufaa kama ulivyotaka. Mara nyingi unaponunua kitu kwa sababu ni bei rahisi, unaishia kukuta unatumia gharama nyingi zaidi mpaka kitu hicho kikufae.

Gharama na thamani kwenye kuuza.

Upande mwingine wa kuangalia gharama na thamani ni kwenye kuuza.

Unapokuwa mfanyabiashara, kila unachouza kinakuwa na gharama zake. Mteja anapokuja kwenye biashara yako na ukamtajia bei, jibu la kwanza kabisa ambalo mteja atakupa ni bei yako ni ghali sana au gharama zako zipo juu sana.

Yaani kabla hata hujamaliza kueleza nini mteja atapata, yeye ameshakuambia kwamba bei yako ni juu.

Sasa kosa kubwa sana ambalo wewe kama mfanyabiashara unaweza kufanya ni kuanza kubishana na mteja kwamba bei haipo juu, au kukubaliana naye kwamba bei ipo juu na hivyo utampunguzia. Hayo yataharibu biashara yako, kwa sababu mteja anayekimbilia kukuambia bei ni juu, wala hata hajajua thamani anayokwenda kupata.

Cha kufanya, pale mteja anapokuambia bei yako ipo juu, mwambie ni kweli, halafu anza kumwonesha thamani ambayo ataipata kwa kulipa zaidi. Unaweza pia kumlinganishia na thamani ndogo atakayopata kwa kununua vitu vya bei ya chini. Mweleze mteja kwa kina thamani atakayoipata na namna atakavyonufaika kwa kununua kile unachouza.

Changamoto kubwa ni kwamba, bei inaonekana na kusikika haraka, lakini thamani imejificha, ni mpaka umweleweshe vizuri mteja wako ndiyo ataweza kuiona thamani ya kweli iliyopo ndani ya kitu.

Unapokuwa unafanya biashara, jipe muda wa kuwaeleza wateja wako thamani wanayoipata na hilo litawafanya waone kwa nini ni sahihi kwao kulipa zaidi, badala ya kukimbilia kupunguza bei au kuuza vitu vya bei ya chini.

Gharama na thamani ni vitu viwili muhimu sana kwenye maamuzi yetu ya kila siku. Tuvitumie vizuri ili kuweza kupata kile tunachotaka na kuyafanya maisha yetu kuwa bora zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha