Rafiki yangu mpendwa,

Njia ya uhakika ya mtu kuweza kutengeneza kipato kisichokuwa na ukomo ni kuanzisha biashara. Na biashara nyingi zinazoanzishwa na wengi, huwa zinaanza kama biashara ndogo, lakini zenye ndoto ya kuwa biashara kubwa.

Ila zipo takwimu ambazo siyo za kufurahisha sana kuhusu biashara hizi ndogo. Katika biashara 10 zinazoanzishwa, biashara nane zinakuwa zimeshindwa kabla ya kufikia miaka miwili, yaani zinakuwa zimefungwa kabisa. Na zile zinazobaki, ndani ya miaka 5 itakuwa imebaki biashara moja tu.

Ukweli ni kwamba biashara nyingi ndogo zinakufa, kwa kasi ambayo ni kubwa na ya kukatisha tamaa kwa wale wanaoingia kwenye biashara hizi.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Zipo sababu nyingi zinazopelekea biashara nyingi ndogo kufa, lakini leo nimekuandalia zile tano ambazo zinagusa karibu kila biashara. Zijue sababu hizi saba na chukua hatua ili biashara yako isife.

Moja; wazo baya la biashara.

Kila wazo la biashara ni zuri, lakini siyo kila wazo la biashara ni zuri kwako, kwa wakati na mahali unapotaka kufanyia biashara yako. Watu wengi wamekuwa wanaingia kwenye biashara kwa sababu wameona watu wengine wanafanya biashara hiyo au kwa sababu wameambiwa ni kitu kinacholipa.

Hivyo wanaingia kwenye biashara ambayo hawajaielewa kwa undani na hawana hatua mbadala za kuchukua pale mambo yanapokwenda tofauti na walivyotarajia.

Hata uwe na mipango mizuri kiasi gani kabla hujaingia kwenye biashara, unapoingia ndiyo unagundua kwamba yanatokea mambo mengi ambayo hukuwa umeyapangilia.

Hivyo kama wazo halikuwa sahihi, unapokutana na ugumu na changamoto hutaweza kuendelea.

Mbili; mtaji mdogo na matumizi mabaya ya mtaji.

Wafanyabiashara wengi wadogo wanaanza biashara zao na mtaji mdogo, kitu ambacho kinawaweka kwenye hatari ya biashara hizo kushindwa pale zinapokutana na changamoto kubwa inayohitaji fedha lakini wao hawana.

Matumizi mabaya ya mtaji pia ni tatizo, hasa pale mfanyabiashara anapotumia mtaji wote kwenye manunuzi mbalimbali na kubaki bila ya fedha yoyote. Inapotokea changamoto inayohitaji fedha kwa haraka, mfanyabiashara anakuwa hana cha kufanya.

Hata kama unaanza biashara na mtaji kidogo, unahitaji kuhifadhi sehemu ya mtaji wako kama akiba kwa lolote litakalotokea.

Tatu; wafanyakazi wabovu au kukosa wafanyakazi kabisa.

Hapa kuna changamoto mbili, ya kwanza ni biashara kutokuwa na wafanyakazi kabisa, ambapo mmiliki wa biashara ndiye anayefanya kila kitu. Hilo linamchosha na kadiri biashara inavyokua anashindwa kuisimamia vizuri na hivyo inashindwa.

Changamoto ya pili ni kuwa na wafanyakazi wabovu, wafanyakazi wasiojali kuhusu mafanikio ya biashara hiyo, wasiojituma na wasiokuwa waaminifu. Wanachoangalia wao ni nini wanapata na wapo tayari hata kuiba ili kupata fedha zaidi.

Ukiwa na wafanyakazi wabovu kwenye biashara yako, upo kwenye hatari kubwa ya kushindwa. Kazana kuajiri wafanyakazi bora, wanaojituma, waaminifu na waadilifu.

SOMA; Sababu Kumi (10) Kwa Nini Unapaswa Kuwa Na Biashara Mwaka Huu 2018.

Nne; udhibiti mdogo wa mzunguko wa fedha.

Fedha yote ya biashara inapaswa kukaa kwenye biashara. Hili ni somo ambalo wafanyabiashara wengi wadogo wamekuwa hawalielewi. Hawaelewi kama biashara yao na wao ni watu wawili tofauti. Wanaamini kwa sababu biashara ni yao, basi wanaweza kuchukua fedha kwenye biashara na kwenda kufanyia mambo mengine.

Na hapo ndipo utaona watu wanafanya mambo ya ajabu kweli, mtu anachukua fedha kwenye biashara na kwenda kujenga nyumba ya kuishi, wakati bado biashara haijaweza kujitegemea, au anatoa fedha na kwenda kununua gari ya kutembelea, wakati bado biashara haijasimama. Hapo bado wale wanaotoa fedha kwa ajili ya matumizi ya kila siku.

Dhibiti mzunguko wa fedha kwenye biashara yako, hakikisha fedha yote ya biashara ipo kwenye biashara na kama unategemea biashara hiyo kuishi, basi jilipe sehemu ya faida ya biashara, na siyo kutoa tu fedha kwenye biashara bila ya mahesabu.

Tano; mfanyabiashara kutokuwa tayari kujitoa na kuweka kazi.

Sijui nani anawashauri wengi kuhusu mafanikio ya biashara, hasa biashara ndogo, lakini wafanyabiashara wengi wanaingia kwenye biashara kwa mtazamo kwamba ni kitu rahisi na cha haraka. Hivyo wanaendesha biashara kwa kufanya kazi kama wanavyojisikia wenyewe. Tena wengine wana anasa ya kulewa baada ya muda wa biashara, kuamka muda wanaotaka wenyewe na hata siku nyingine kufunga biashara ili kwenda kuangalia mpira au burudani nyingine.

Unapoingia kwenye biashara ndogo huna tofauti na mtu anayeingia kwenye vita. Maisha yako ni mapambano masaa 24 kwa siku kila siku. Muda wote unapaswa kuwa unaifikiria biashara yako, unahitaji kuachana na starehe na anasa mbalimbali, unahitaji kuachana na baadhi ya watu ambao hawana pakubwa wanapoenda na unahitaji kuweka muda na nguvu za ziada kwenye biashara yako. Bila ya hivyo, biashara yako itashindwa.

Rafiki, sababu hizi kubwa tano zimeua biashara nyingi sana, angalia jinsi ambavyo zinahusika kwenye biashara yako na chukua hatua sahihi ili kuzuia biashara yako isife kutokana na sababu hizo tano. Ingia kwenye biashara sahihi, tumia vizuri mtaji wako, ajiri watu sahihi, dhibiti mzunguko wako wa fedha na simamia biashara yako vizuri. Mambo hayo matano ukiyafanya vizuri, utakuwa na biashara yenye mafanikio makubwa.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL

Usomaji