Ndege inapotaka kuruka hewani, kizuizi chake kikubwa ni hewa, hivyo ndege inahitaji kutumia nishati kubwa kuzidi ukinzani huo wa hewa ili iweze kuruka. Kwa akili za haraka haraka unaweza kusema kama kusingekuwa na hewa basi ndege ingeruka kwa urahisi, lakini ukweli ni kwamba, kama pasingekuwa na hewa kabisa, ndege isingeweza kuruka kabisa. Hivyo kinachozuia ndege isiruke, ndiyo kinachohitajika ili ndege iweze kuruka.

Boti inayosafiri kwenye maji, ukinzani wake mkubwa ni maji, hivyo nishati inabidi itumike ili kuvuka ukinzani huo wa maji. Nafikiri sihitaji tena kukukumbusha kwamba bila ya uwepo wa maji, boti haiwezi kusafiri.

Kwa asili, chochote ambacho kinaleta ukinzani kwenye kitu, ndiyo hicho hicho kinachohitajika ili kitu hicho kiweze kufanya kazi vizuri.

Kadhalika kwenye maisha yetu, kile kinachotuzuia, ndiyo tunachohitaji ili tuweze kufanikiwa. Vikwazo, magumu, changamoto na hata kushindwa, vyte hivi tunavihitaji ili tuweze kufanikiwa.

Kama vitu hivi vitaondolewa kabisa kwenye maisha yetu, yaani tukawa na maisha ambayo tunapata kila tunachotaka bila ya kukosa na bila ya kufanya kazi yoyote, kila kitu kinakosa maana.

Na hili linaonekana wazi kwa wale ambao wanapata kila kitu kwa urahisi, huwa wanaishia kuharibu maisha yao au kuishia kuwa na msongo wa mawazo na hata sonona.

Unahitaji sana kukutana na vikwazo ili uweze kutumia nguvu kubwa iliyopo ndani yako kuvuka vikwazo hivyo na hivyo pia kutumia nguvu hiyo kufanikiwa zaidi.

Unahitaji kukutana na changamoto ili kukua zaidi na kuweza kufanya makubwa zaidi ya yale uliyoyazoea.

Unahitaji kushindwa ili ujue thamani halisi ya ushindi, na uhamasike kuchukua hatua zaidi ili kufanikiwa zaidi.

Kila unachokutana nacho, ambacho kinakuzuia kupata unachotaka au kinakuchelewesha, jua hicho kimekuja kwako kama manufaa, kitumie vizuri na utaweza kupiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako.

Hilo ni kwenye maisha yetu binafsi, kazi zetu na hata biashara zetu, kila ugumu unaokutana nao usikate tamaa, bali angalia unawezaje kuwa bora zaidi kupitia ugumu huo na ukaweza kufanya makubwa zaidi.

Chochote unachofikiria ni kikwazo kwako, anza kukiangalia kwa jicho la pili na utaona manufaa makubwa ndani yake, ya kukuwezesha wewe kufanikiwa zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha