Rafiki yangu mpendwa,

Inapokuja kwenye swala la kuongeza kipato, huwa wengi tunakimbilia kuangalia mbali na kusahau pale ambapo tupo sasa. Kama umeajiriwa unaanza kuangalia biashara gani zinazoweza kukulipa. Na kama upo kwenye biashara ila haikulipi sana, unaanza kuangalia biashara gani nyingine inayolipa zaidi.

Japokuwa ni rahisi kuona kitu kinacholipa zaidi kwenye eneo tofauti na pale ulipo sasa, sehemu nzuri ya kuanzia kuongeza kipato chako ni hapo ulipo sasa. Yaani kabla hujaanza kuangalia eneo jingine lolote, unaaswa kuanza kuangalia hapo ulipo sasa, maana hapo ulipo, umekalia mgodi mkubwa ambao ukiweza kuutumia vizuri, unaweza kuongeza kipato chako kadiri utakavyo.

Rafiki, ninachotaka kukuambia ni kwamba, hapo ulipo sasa, kwa kile unachofanya ndipo penye fursa nzuri kwako kuongeza kipato chako. Kwa sababu kama umeshafanya hicho unachofanya kwa muda sasa, umeshajijengea uzoefu mzuri, umeshajijengea mtandao wa watu na pia umeshajifunza kupitia kushinda na kushindwa. Yote hayo ni muhimu sana kwenye kuongeza kipato chako.

652d5-tangazo2bmasikini

Sasa wafiki, nimekuambia ipo njia moja ya uhakika ya kuongeza kipato chako kwa hapo ulipo sasa, na njia yenyewe ni hii; TOA THAMANI ZAIDI. Kama utaishia kusoma hapa na usiendelee tena, basi ondoka na hilo, toa thamani zaidi.

Kwa chochote unachofanya, iwe umeajiriwa, umejiajiri au unaendesha biashara, toa thamani zaidi na utaweza kuongeza kipato zaidi.

Kama ambavyo nimekuwa nakuambia, unalipwa kulingana na thamani unayotoa. Yaani kipato unachopata sasa, ndiyo kiasi cha thamani unayotoa kwa wengine. Hivyo kama unataka kupata zaidi, lazima uanze kutoa thamani zaidi.

Faida unayoipata kwenye biashara yako ni sawa na thamani unayoitoa kwa wateja wako. Mshahara unaopewa na mwajiri wako, ni sawa sawa na thamani unayompatia. Njia ya kwanza na ya uhakika ya kuongeza kipato chako, ni kutoa thamani zaidi.

Na kwa wale ambao wanasoma hapa na kujiambia mimi natoa thamani sana lakini silipwi vizuri, jaribu kujichunguza vizuri, angalia wale wanaolipwa zaidi na utaona kuna thamani zaidi wanayotoa. Labda wanafanya kitu ambacho hakuna wengine wanaoweza kufanya au wanaweka muda na nguvu zaidi kwenye kazi zao. Kwa vyovyote vile, ipo thamani ya ziada ambayo wanaitoa na inawapelekea walipwe zaidi.

Rafiki yangu, kumbuka hili kila unapofikiria kuongeza kipato chako, ni thamani ipi zaidi unayoweza kuitoa ili ulipwe zaidi?

Na hapa nakushirikisha njia tano za kutoa thamani zaidi kwa wale wanaotegemea kile unachofanya ili uweze kuongeza kipato chako zaidi.

Moja; toa huduma kwa wengi zaidi. Njia ya kwanza kabisa ni kutoa huduma kwa wengi zaidi, na hii ni nzuri kwa wale ambao wapo kwenye biashara. Haijalishi ni biashara gani unafanya, kuna watu wengi ambao wangeweza kuwa wateja wako wazuri, ila hawajui hata kama upo. Ni wajibu wako kuwafikia watu hao na kuwahudumia ili kuweza kuongeza kipato chako zaidi.

Mbili; toa huduma bora zaidi. Kwa chochote unachofanya, toa huduma bora zaidi ya ulivyozoea kutoa, au watu walivyozoea kupokea. Hii itawafanya watu wawe tayari kukulipa zaidi ya walivyozoea kulipa.

Tatu; weka muda zaidi. Hii ni nzuri kwa wale walioajiriwa, moja ya njia za kuongeza thamani zaidi ni kuweka muda zaidi kwenye kazi, kufanya kazi zaidi ya muda uliozoeleka, inakufanya wewe kutekeleza majukumu mengi zaidi na hivyo kutoa thamani zaidi. Unaweza kuweka muda zaidi kwa kuwahi kufika eneo la kazi na kuchelewa kuondoka, pia kwa kutokupoteza muda kwa mambo yasiyo muhimu na kuweka juhudi zaidi.

SOMA; Jinsi Ya Kuongeza Thamani Kwenye Kile Unachofanya Ili Uweze Kulipwa Zaidi.

Nne; fanya vitu vya ziada. Watu wengi huwa wanafanya kile ambacho wamezoea kufanya mara zote, lakini vipo vitu vya ziada wanavyoweza kufanya kwa pale walipo sasa, ila hawafanyi hivyo. Kwa chochote unachofanya, jiulize kipi cha ziada unachoweza kufanya na ukalipwa zaidi. Kama upo kwenye ajira, angalia ile huduma unayompa mwajiri wako, unawezaje kuitoa kwa wengine kwa muda ambao siyo wa kazi na ukalipwa pia.

Tano; fanya kile ambacho hakuna mwingine anaweza kufanya. Hii ndiyo njia kubwa ya kuongeza thamani, kwa kuangalia kile ambacho hakuna anayeweza au kupenda kufanya kisha ukakifanya wewe. hilo linakutofautisha na wengine wote na kukuweka kwenye nafasi ya kufanikiwa zaidi. Kama unafanya kile ambacho kila mtu anafanya, unajiweka kwenye nafasi ya kuweza kuondolewa na yeyote. Lakini ukifanya kile ambacho hakuna anayeweza kufanya, watu hawatakuwa na budi bali kuja kwako, na hapo unaweza kuamua kiasi gani unataka kulipwa.

Rafiki, mara zote angalia ni kwa namna gani unaweza kutoa thamani zaidi kwenye kile unachofanya sasa, kabla hujakimbilia kuangalia vitu vingine. Kwa sababu hapo ulipo sasa, umeshafanya uwekezaji mkubwa sana, utakaoweza kunufaika nao kama ukiutumia vizuri.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL

Usomaji