Uko hapo ulipo sasa, kwa sababu ya maamuzi uliyofanya siku za nyuma, kwa kujua au kutokujua. Na maamuzi unayoyafanya leo, yatakugharimu kwa siku zijazo, iwe unajua au hujui.

Watu wengi wamekuwa wanafanya maamuzi mabaya, ambayo wakati wa kuyafanya hayaonekani kuwa mabaya, ila mpaka baadaye ndiyo madhara ya maamuzi hayo yanaonekana. Na huo unakuwa ni wakati ambao hawawezi kugeuza maamuzi ambayo waliyafanya mwanzo.

Leo tunakwenda kuangalia sababu mbili zinazopelekea wewe kufanya maamuzi mabaya, ili uweze kuepuka kufanya maamuzi mabaya leo yatakayokugharimu sana kesho.

Angalia kila changamoto unayopitia sasa, na utagundua siku za nyuma, kuna maamuzi uliyafanya, ambayo yamechangia wewe kuwa hapo. Iwe ni uchaguzi wa masomo au taaluma uliyosomea, uchaguzi wa kazi unayofanya, uchaguzi wa mwenza uliyenaye, kuna wakati ulifanya maamuzi, na sasa yanakusumbua.

Zipo sababu kuu mbili zinazowapelekea wengi kufanya maamuzi mabaya.

Sababu ya kwanza ni haraka.

Wakati wowote ambapo unakuwa na haraka ya kufanya maamuzi, inabidi ufanye sasa au hutaweza kufanya tena, unakuwa kwenye nafasi kubwa ya kufanya maamuzi mabaya. Kwa sababu unaposukumwa kufanya maamuzi kwa haraka, unakosa muda wa kufikiria kwa kina madhara ya maamuzi unayofanya, hasa kwa baadaye. Hivyo unajikuta unachagua chochote ambacho kitakusaidia kwa wakati ulionao. Sababu hii imewapelekea wengi kuingia kwenye maeneo ambayo walifikiri ni rahisi, lakini baadaye wakakuta ni magumu na wakati mwingine hawawezi kuondoka kirahisi.

Sababu ya pili ni madhara ya muda mrefu.

Sababu ya pili inayopelekea wengi kufanya maamuzi mabaya, ni pale madhara ya maamuzi hayo hayataonekana haraka, yaani itachukua muda mpaka madhara yaonekane. Hii ndiyo sababu kubwa sana, na ambayo imewaangusha wengi. Kwa sababu watu wamekuwa wanafanya maamuzi kwa kuangalia leo, hawajisumbui sana na kesho. Maamuzi mengi leo yanakuwa hayana shida, lakini siku zijazo, maamuzi hayo yanaleta madhara makubwa sana.

Chukulia mfano wa kutokuweka akiba kwa ajili ya baadaye, wakati una nguvu na kipato kinaingia hutaweza kuona madhara, lakini baadaye nguvu zinapoisha na kipato huna tena, ndiyo unakumbuka kama ungejiwekea akiba, mambo yasingekuwa magumu kama yanavyokua. Kadhalika maamuzi kama ya mahusiano na hata uchaguzi wa kazi na biashara, wengi huwa wanaangalia kile wanachopata sasa, lakini hawafikirii miaka mingi ijayo kile walichochagua kitawafanya wawe na maisha gani.

Ni rahisi kurubuniwa na kujisikia vizuri kwa muda mfupi, kuondokana na maumivu ya muda mfupi kwa kufanya maamuzi yanayokufaa kwa muda mfupi, lakini maamuzi ya aina hii huwa yana madhara makubwa sana kwa muda mrefu.

Kupunguza au kuondokana kabisa na kufanya maamuzi mabaya, kuwa makini na sababu hizo mbili.

Moja, usikimbilie kufanya maamuzi kwa haraka, hasa maamuzi makubwa na yanayobadili kabisa maisha yako. Jipe muda wa kutafakari maamuzi hayo, kuangalia maamuzi mbadala na kuona jinsi gani unaweza kufanya maamuzi bora zaidi.

Mbili, unapofanya maamuzi, angalia miaka mingi ijayo, usiangalie leo na kesho, angalia miaka 5, 10, 20 na hata 50 ijayo. Angalia madhara yote ya maamuzi unayofanya kwa sasa na hata kwa baadaye. Jione kwa miaka mingi inayokuja ukiwa kwenye maamuzi unayotaka kufanya leo, na jiulize kama hicho ndiyo unachotaka kufanya.

Haya ni muhimu sana kwa maamuzi makubwa, maamuzi ambayo yanabadili kabisa maisha yako na ukishayafanya ni vigumu kuyageuza. Yazingatie ili usiwe na maisha ya majuto na kufikiria kama ungejua mapema ungefanya maamuzi bora zaidi. Umeshajua leo, fanya maamuzi bora kuanzia leo ili siku zijazo usiwe kwenye wakati mgumu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha