Watu wengi wanapoianza safari ya mafanikio, na kupata mafanikio kiasi, mafanikio hayo hugeuka na kuwa sumu kwa mafanikio makubwa zaidi kwenye maisha yao.
Kinachotokea ni kwamba, kwa kuwa wamepata mafanikio kiasi, basi wanajisahau na kuona sasa wanaweza kufanya kila kitu. Hivyo pale inapojitokeza fursa yoyote ile, wanasema ndiyo haraka bila ya kusita.
Na watu wanaowazunguka ndiyo wanaikuza zaidi hatari hiyo, kwa sababu wanawasukumia fursa nyingi wakiamini zitawafaa. Na wakati huo huo pale watu hao wanapochelewa kuchukua hatua kwenye fursa fulani, wanawaambia kwamba wanapoteza.
Ili kufanikiwa kwenye maisha lazima uwe tayari kufunga milango ya fursa. Lazima uwe tayari kusema hapana kwa vitu vizuri ili uweze kupata vile vilivyo bora kabisa.
Chagua kutokufanya baadhi ya vitu, ili upeleke muda na nguvu zako kwenye yale ambayo ni muhimu zaidi kwako.
Njia bora ya kufunga milango ya fursa, kuchagua nini unafanya na nini hufanyi ni kuwa na orodha mbili.
Orodha ya kwanza ni vile vitu ambavyo ni muhimu sana kwako kufanya ili kuweza kufikia malengo yako makubwa. Hivyo andika malengo na maoni yako, na orodhesha vile unavyopaswa kufanya ambavyo vitakufikisha kwenye malengo hayo.
Orodha ya pili ni vile vitu ambavyo havina umuhimu kwako kufikia malengo yako, vinaweza kuwa vizuri kufanya, lakini havina mchango kwenye kufikia malengo na maono makubwa uliyonayo. Orodhesha vitu vyote ambavyo ni vizuri kufanya, ambavyo kila mtu anafanya, lakini havina mchango wowote kwenye kufikia malengo yako makubwa kwenye maisha yako. Hii ni orodha ya vitu ambavyo hupaswi kuvifanya kwenye maisha yako.
Sasa inapojitokeza fursa yoyote mpya, fursa ambayo unashawishika ni nzuri kufanya, fursa ambayo kila mtu anakuambia unaikosa, badala ya kupoteza muda kufikiria na kuhangaika na maamuzi, angalia inaangukia upande upi wa orodha yako. Kama inaangukia kwenye orodha ya vitu vya kufanya ifanye, kama inaangukia kwenye orodha ya vitu ambavyo hutafanya basi usiifanye.
Hii ni njia bora kwako kuepuka kuhangaika na kila aina ya fursa ambazo nyingi zinaishia kuchukua muda na nguvu zako na zisikufikishe kule unakotaka kufika.
Usikimbilie kila mlango unaofunguka, kila fursa inayojitokeza kwa sababu unaona ni nzuri kwako au utakosa, kwa sababu kila mtu anafanya. Lazima mpaka sasa uwe umeshajua kwamba hakuna njia ya mkato ya mafanikio, hakuna mafanikio ya haraka na lazima uweke kazi, ukutane na magumu na changamoto kabla hujafanikiwa. Hivyo unapoona fursa inayovutia kwa nje, jua ndani yake kuna ugumu na changamoto, hivyo swali kwako ni je upo tayari kukabiliana na magumu na changamoto utakazokwenda kukutana nazo, na je kwa kuvuka ugumu na changamoto hizo utafika unakotaka kufika na maisha yako?
Kama ukipima kila fursa kwa njia hii, utapunguza muda unaochukua mpaka kufanikiwa. Kwa sababu wengi wanachelewa kufanikiwa kwa sababu wanatumia muda mwingi kufanya mambo ambayo hayahusiani kabisa na kile wanachotaka kwenye maisha yako. Ni mpaka wanaposhindwa kwenye mengi ndiyo wanagundua kwamba hakuna njia ya mkato, hapo ndipo wanatulia na kile walichochagua na mwishowe wanafanikiwa sana.
Kadiri unavyojua hili haraka, na kuacha kuhangaika na kila fursa inayopita mbele ya macho yako, ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kufanikiwa.
Jifuze kufunga baadhi ya milango ya fursa, jifunze kusema hapana kwa mazuri kama kweli unataka kupata yale yaliyo bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,