Kila mchezo una sheria zake, ambazo lazima kila anayeshiriki azifuate ili mchezo uweze kwenda vizuri. Kwenye mchezo kama mpira wa miguu, ukishika mpira kwa mkono ni kosa kubwa litakalopelekea upate adhabu kali, wakati kwenye mpira wa mikono kushika mpira kwa mikono ni kitu cha kawaida.
Kwenye maisha yako pia, kila unachofanya kina sheria na taratibu zake, ambazo usipozijua utaishia kupata adhabu kwa njia ya kushindwa, kukutana na changamoto au kupoteza kile ulichokuwa unataka.
Usiingie kwenye mchezo wowote kabla hujajua sheria za mchezo huo. Kwa maneno mengine usiingie kwenye kitu chochote kipya kwenye maisha yako, kabla hujajua taratibu zake na jinsi kinavyokwenda. Unahitaji kujua kila unachoingia na kukifanya kwa undani, ili kuepuka makosa ya wazi ambayo yanawaangusha wengi.
Na hata kama unataka kuvunja sheria kwa sababu zinakuzuia kufanya yale unayotaka kufanya, labda ni mazoea ya watu ambayo yanawazuia wasikue, bado unahitaji kujua sheria hizo ili unapozivunja uwe upande salama wa kutokupoteza zaidi.
Chochote usichokijua kitakuumiza, usichokijua kitakuletea maumivu, usichokijua kitakufanya uteseke sana. Kuna wakati utajiona kama umekwama na hakuna njia, kumbe kuna vitu fulani ambavyo bado hujavijua. Kwa kujua vitu hivyo unaweza kupiga hatua kubwa.
Wanasema kutokujua sheria siyo kinga dhidi ya kuvunja sheria hiyo. Yaani ukivunja sheria, hata kama ulikuwa hujui, bado utaadhibiwa kwa sheria hiyo. Na hivyo ndivyo maisha yalivyo.
Usipozijua sheria za fedha, utaishia kufanya kazi na kutumia fedha zako bila ya kubaki na chochote mpaka siku inafika huna tena nguvu ya kufanya kazi na pia huna fedha za kuendesha maisha yako.
Usipozijua sheria za biashara, utaingia kwenye biashara na kushangaa wateja hawaonekani, au wakija hawarudi tena. Mbaya zaidi unaweza kuuza sana lakini fedha usione zinaenda wapi, mwishowe unajiambia kuna chuma ulete, kumbe tu hujazijua sheria za biashara.
Usipozijua sheria za mahusiano utasumbuka sana kwenye mahusiano yako na wengine. Kila wakati itakuwa ni ugomvi na kusuguana na wengine, vitu vidogo vitaleta mabishano makubwa na kila mtu atataka kuwa sahihi na kuona mwingine amekosea.
Usipojua sheria za maisha kwa ujumla, utaendesha maisha yako kama bendera ambayo inafuata upepo, utasumbuka na kila kitu, utachoka sana lakini hakuna kikubwa ambacho utaona umekamilisha.
Zijue sheria za mchezo wowote unaocheza, zijue sheria za chochote unachofanya kwenye maisha yako, jua wanakopita wale walioshindwa na wanakopita wale waliofanikiwa, kisha tengeneza njia yako ya ushindi, ambayo hairudii makosa ambayo yamewaangusha wengine.
Unapozijua sheria sahihi, ukatengeneza mkakati sahihi kwako na kuweka juhudi kubwa, hakuna kinachoweza kukuzuia kupata kile unachotaka kwenye maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,