Kama unataka kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako, basi usifanye kazi. Hii ni kauli ambayo nimewahi kuitumia kama kicha cha habari cha makala huko nyuma, na mtu mmoja bila ya kusoma makala alinihukumu kwa kichwa hicho, akiniambia naanza kuwadanganya watu wasifanye kazi, kwamba najaribu kuwapa njia za mkato.
Kama unanijua vizuri unajua hicho siyo ninachoamini, na makala hiyo haikuwa inazungumzia chochote kuhusu njia za mkato za kufanikiwa, bali nilikuwa nazungumzia kuhusu kufanya kile ambacho mtu unapenda kufanya, kile ambacho upo tayari kukifanya hata kama hakuna anayekulipa. Hicho ndiyo kitakuwezesha kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Chochote ambacho tunafanya kwenye maisha yetu ili kuingiza kipato na pia kutoa mchango wetu kwa wengine, kimegawanyika katika makundi matatu;
Moja; ajira, hapa mtu unakuwa umeajiriwa na unapewa majukumu ya kufanya na kulipwa kama mlivyokubaliana.
Kazi; hapa mtu unatoa huduma, ujuzi au uzoefu fulani kwa wengine na unalipwa.
Tatu; wito, hapa mtu unafanya kitu kwa sababu kuna mchango mkubwa unaotoa kwa wengine bila ya kujali unalipwa nini.
Ukiviangalia vyote vitatu kwa nje utaona vinaingiliana na vyote vinaonekana ni kazi. Lakini vinatofautiana, ajira ni kitu ambacho unaomba wengine wakupe, kazi ni kitu ambacho unachagua kufanya na wito ni mchango ambao unachagua kutoa kwa wengine.
Sasa mafanikio makubwa sana kwenye maisha yanakuja pale ambapo vitu hivyo vitatu vinaoana, au viwili vinaoana. Kama utapata ajira ambayo unachagua kufanya kazi bora, ambayo ni wito wako, basi utafanikiwa sana. Au kama utachagua kufanya kazi ambayo inaendana na wito wako, utaweza kufanya makubwa.
Lengo langu hapa leo ni kukuonesha kama unaishi wito wako kwenye maisha au la. Na zipo dalili tano za kukuonesha hilo.
Moja; unaweza kusema bila ya kusita, napenda kitu hiki.
Kama unapenda kile unachofanya, kutoka ndani ya moyo wako na bila ya kusukumwa na yeyote basi unaishi wito wako. Na unapopenda kile unachofanya, unajiweka kwenye nafasi nzuri ya kuchukua hatua zaidi zitakazokuwezesha kufanikiwa zaidi.
Mbili; uko vizuri kwenye kile unachofanya.
Uzuri wa wito ni kwamba unakuwa vizuri kwenye unachofanya bila ya kulazimisha na yeyote. Unajikuta una msukumo wa kujifunza zaidi na hata kujaribu mambo mapya zaidi.
Tatu; huchoki.
Unapokuwa unaishi wito wako, huchoki kufanya kile unachofanya. Watu wengine watakuwa wanahesabu muda unaisha saa ngapi, wewe utashtuka kwamba muda umeisha haraka. Unaweza kumezwa na kazi zako mpaka ukasahau vitu kama kula au kupumzika. Kwa kuwa unapenda unachofanya, na uko vizuri kwenye kukifanya, huchoki kukifanya.
Nne; watu wanakuambia ni kitu chako.
Kama upo katikati ya wengine, na inapotokea kitu kinachoendana na unachofanya, watu wanakutafuta wewe, na kukuambia hicho ni kitu chako, ni dalili nzuri kwamba watu wanaona tofauti kubwa kwako na kwa wengine. Pale ambapo watu wanakuletea shida zinazoendana na unachofanya, wakiamini wewe pekee ndiye unayeweza kuzitatua kwa ubora, ni dalili nzuri kwamba unaishi wito wako na unaufanyia kazi vizuri.
Tano; unawanufaisha wengine.
Kinachofanya wito uwwe tofauti na kazi ni kipaumbele, kwenye wito, kipaumbele cha kwanza ni kuwasaidia wengine, kufanya maisha ya wengine yawe bora zaidi. Ndiyo maana wito unahusishwa na shughuli ambazo zina mchango wa moja kwa moja kwa wengine na siyo tu kuangalia fedha ambazo mtu anapata.
Rafiki, kila mtu ana wito ndani yake, lakini ni wachache sana wanaopata nafasi ya kujua wito wao. Hakikisha wewe unaujua wito wako, kisha geuza wito huo kuwa kazi yako na hutafanya tena kazi kwenye maisha yako. Badala yake utafanya kile unachopenda, ambacho kinawasaidia wengine na hivyo utaweza kupata chochote unachotaka kupata.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ujumbe mzuri sana Kocha.
Hakika umeniongezea kitu muhimu hapa
LikeLike
Karibu sana.
LikeLike