Moja ya changamoto kubwa kwenye zama tunazoishi sasa ni wingi wa maarifa na taarifa ambazo zinawafanya wengi washindwe kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha yao.
Kuna maarifa na taarifa nyingi ambazo zinakinzana na mtu anapofuatilia zote, anashindwa kujua afanye nini. Anaanza kubishana na yeye mwenyewe, anaanza kuwa na wasiwasi juu yake, anaanza kupokea upinzani kutoka kwa wengine na mwisho kujikuta hakuna hatua ambayo amepiga.
Ili uweze kufanya maamuzi bora kwenye maisha yako, na ili uweze kusimamia maamuzi hayo yaweze kukuletea matokeo bora, inabidi uwe mgumu kidogo, inabidi uwe umejipanga na ujue umesimama wapi. Lazima kwanza ujue nini hasa unachotaka, na uweze kuepuka vishawishi mbalimbali unavyotegwa navyo ili usiweze kufanya maamuzi na kuyasimamia.
Kuna mambo matatu ambayo ukiyafanya, yatakusaidia sana kwenye kufanya maamuzi bora. Mambo haya matatu yanaweza kuonekana ya ajabu kwako na yasiyohusiana na maamuzi, lakini ukiyafanyia kazi utaona jinsi ambavyo yanakuwezesha kufanya maamuzi bora na kuyasimamia pia.
Moja; usipokee ushauri ambao hujauomba.
Kuna wale watu ambao wanakuja kwako wakiwa na ushauri juu ya maisha yako, juu ya kile unachofanya na hata jinsi gani unaweza kufanya zaidi. Wanaweza kuwa na ushauri mzuri sana, lakini nikuambie kitu kimoja, kama hujamfuata mtu kumwomba ushauri, puuza ushauri wowote ambao unapewa.
Kama hujakwama na kuhitaji ushauri, huhitaji kuhangaika na kila ushauri wa kila anayetoa, badala yake unahitaji kufanyia kazi mipango ambayo tayari umeshajiwekea. Hivyo peleka nguvu zako kwenye mipango yako, na pale unapoona umekwama, pale unapohitaji ushauri, wewe ndiye uchague mtu gani anakufaa kwa ushauri na umsikilize na kufanyia kazi yale mliyoshauriana.
Hakuna kitu kimepoteza watu wengi kama ushauri wa bure, pale mtu anaposikiliza kila aina ya ushauri unaoletwa kwake, anajikuta anabadili kila anachofanya, mpaka anafika mahali anakuwa hajui tena ni nini anafanya au wapi anasimama.
Epuka ushauri wa bure, ushauri ambao watu wanakupa kabla hujawaomba, unaweza kuwa ushauri mzuri, lakini utakuchelewesha kama utaanza kuhangaika na kila ushauri.
Mbili; epuka vitu vyenye matangazo.
Kama kitu kinaambatana na tangazo, kiepuke kama ukoma, kwa sababu siyo kitu sahihi kwako, kinalazimishwa kufika kwako kwa kutumia matangazo yanayoambatana na kitu hicho.
Habari zinaambatana na matangazo, vipindi vya tv, matangazo, vipindi vya redio, matangazo, magazeti, matangazo na hata mitandao ya kijamii, yote inaendeshwa kwa matangazo.
Hii ina maana kwamba wale wanaokupa kile kinachokuja na matangazo, watafanya chochote ili wapate matangazo na hilo halitakuwa bora kwako.
Ukishaona kitu kinaambatana na matangazo, kimbia haraka sana, kuna namna watu wanataka kukutengeneza ili wapate wanachotaka, maana kuna vitu wanajaribu kukuuzia, ambavyo haviwezi kuwa bora sana kwako.
Ni furaha iliyoje kwamba angalau vitabu (mpaka sasa) havina matangazo, hivyo unaweza kujifunza kile unachotaka kujifunza bila ya kukatishwa na matangazo mbalimbali.
Tatu; unapoingia kwenye ubishi, chimba chanzo kikuu.
Kila unapojikuta kwenye ubishi, iwe ndani yako mwenyewe au ubishi na wengine, jiulize nini chanzo kikuu cha ubishi huo. Na usiangalie juu pekee, bali chimba ndani na ona chanzo kikuu.
Je ni imani gani zipo nyuma ya ubishi huo, kwa kila upande? Je ni maoni ya watu gani ambayo kila mtu anasimamia na kubishania? Je ukweli kamili ni upi? Ni hisia gani ambazo kila upande unaegemea kwenye ubishani huo?
Kwa kuchimba ndani, utagundua kwamba kile ambacho watu wanabishana, siyo kile halisi kinachowasukuma wawe kwenye ubishi, na ukishajua hilo, hutapoteza muda wako kubishana na yeyote hata na wewe binafsi. Kwa sababu utakijua chanzo na utakubaliana nacho au kukipuuza.
Rafiki, mambo haya matatu kama nilivyokuambia, unaweza usiyaelewe haraka, lakini yafanyie kazi na utaona ni jinsi gani utakavyookoa muda wako na nguvu zako na kuvipeleka kwenye mambo muhimu zaidi kwako. Pia yatakusaidia kuacha kuhangaika na vitu vingi ambavyo havina tija kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,