Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii mpya ya leo,
Ni siku nyingine nzuri sana kwetu, ambapo tumepata nafasi ya kipekee ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari WAKATI SAHIHI WA KUCHIMBA KISIMA…
Wakati sahihi wa kuchimba kisima ni kabla hujapatwa na kiu.
Wakati sahihi wa kununua mwavuli ni kabla mvua hazijaanza kunyesha.
Wakati sahihi wa kuwekeza ni wakati bado una nguvu za kufanya kazi,
Wakati sahihi wa kupanda mbegu ni wakati msimu unaanza.

Rafiki, kuna wakati sahihi wa kufanya kila kitu, na pia wakati sahihi ni kabla hujawa na uhitaji wa kile unachopaswa kufanyia kazi.
Lakini kwa kuwa hatuna uhitaji wa kitu hicho kwa sasa, huwa inakuwa rahisi kuahirisha. Na utaahirisha mpaka siku ambayo huwezi tena kuahirisha na pia huwezi tena kufanya, na hapo ndipo utayaona maisha ni magumu na hayana huruma.

Siku utakayokuwa una kiu kali, huna maji halafu ndiyo unataka uchimbe kisima, ndiyo utajua kwa nini ulipaswa kufanya hilo mapema.
Siku utakayokuwa huna tena nguvu za kufanya kazi zako kama unavyoweza kufanya sasa, huku ukiwa huna uhakika wa kipato, ndiyo utajua kwa nini ilikuwa muhimu kwako kuchukua hatua mapema.

Ninachotaka kukukumbusha asubuhi ya leo rafiki yangu ni hiki, fanya kile ambacho unajua unapaswa kufanya, kabla hujafikia wakati wa kukihitaji. Kwa kuchukua hatua sasa, unajiweka kwenye nafasi nzuri ya maisha yako kwenda vizuri.
Lakini kama utachukua njia rahisi, njia ya kuahirisha, jua huepuki ugumu wa sasa, bali unausogeza mbele, na huko mbele unakoupeleka patakuwa pagumu zaidi maana wewe hutakuwa na uwezo wa kufanya vizuri kama ulionao sasa.

Chukua hatua zote muhimu sasa rafiki yangu, usiahirishe chochote ambacho ni muhimu kwa maisha yako ya baadaye.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuchimba kisima kabla kiu haijakushika.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha