Huwezi kujua unaweza kwenda mbali kiasi gani, mpaka uende mbali zaidi ya ulivyozoea. Kadiri unavyokwenda mbali zaidi ya ulivyozoea, ndivyo unavyozidi kugundua kwamba unaweza kwenda mbali zaidi.
Kama umeacha kwenda mbali zaidi, utaamini kwamba pale ulipofika ndiyo kikomo, lakini uhitaji unapokuja, utagundua ya kwamba unaweza kwenda mbali zaidi.
Njia pekee ya kujua wewe ni imara kiasi gani, ya kujua kiasi chako cha uvumilivu na kujua namna gani unaweza kufanya zaidi, ni kukutana na magumu.
Magumu unayokutana nayo, mateso unayokutana nayo, japokuwa unaweza kuona ni mabaya na yanakurudisha nyuma, lakini yana kazi ya kukusukuma mbele zaidi, yana kazi ya kukuonesha wewe ni nani, yanakusaidia ujijue vizuri zaidi.
Kama hujawahi kukutana na ugumu, huwezi kujua una uwezo kiasi gani wa kupambana na magumu mbalimbali unayoweza kukutana nayo. Lakini unapokutana na ugumu na ukauvuka, hutaweza kusumbuliwa tena na ugumu wa aina hiyo.
Unapokutana na ugumu au mateso kwenye maisha yako, usiumie wala kukata tamaa, badala yake furahia kwamba unapata kitu cha kujipima umekuwa imara kiasi gani.
Kila ugumu na mateso unayokutana nayo, usilalamike kwamba yamekuja kukurudisha nyuma, badala yake shukuru kwa sababu yamekuja kukusaidia kwenda mbele zaidi
Unavyoweza kutatua kila ugumu na changamoto unayokutana nayo, ndivyo unavyozidi kuwa imara zaidi.
Unaweza kutamani sana maisha ambayo hayana changamoto wala mateso, lakini nakuhakikishia maisha hayo yatakuwa ya hovyo sana na yatakosa maana ya kuyaishi.
Kama kila wakati unapata kila unachotaka, hutajiona ukikua na hutaweza kuwa imara zaidi. Utaanza kufanya vitu kwa mazoea na mwishowe kukaribisha matatizo makubwa zaidi.
Sisi binadamu tumeumbwa kwa ajili ya changamoto na magumu, tusipokutana nayo kwenye maisha yetu, tunachagua kuyatengeneza sisi wenyewe.
Angalia maisha ya wale ambao wanapata kila wanachotaka, mwishowe huishia kutengeneza matatizo makubwa sana kwao, ambayo yanapelekea kuharibu maisha yao kabisa.
Kupata kila unachotaka kwenye maisha yako, kwa namna unavyotaka, ni hatari kubwa sana kwenye maisha yako. inakufanya uwe dhaifu kwa kuzoea vitu, na pia inakupa muda mwingi ambao utajikuta unautumia kutengeneza matatizo zaidi.
Kila gumu unalokutana nalo, hakikisha linakufanya uwe imara zaidi, hakikisha linakuwezesha kupiga hatua zaidi. Hii ndiyo njia bora kwako kunufaika na magumu unayokutana nayo kwenye maisha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Hakika naimami kuingia kwangu kisima haikuwa bahati mbaya pengine ilikuwa ni mpango wa Mungu, maana Elimu ninayoipata, ukilinganisha na matataizo ninayoyaptia, sijui ningekuwa wapi, hadi nakumbka maneno yasemayo “WATU WANGU WANAANGAMIA KWA KUKOSA MAARIFA. “asante kocha hebu nichomwe kama dhahabu katika tanuru la moto mkari, najua ipo siku nitang’ara japo hali inatisha, asante kwa Elimu ya ustoa.
LikeLike
Karibu sana Beatus
LikeLike