Rafiki yangu mpendwa,
Inapokuja kwenye kujifunza, huwa zipo njia mbili;
Njia ya kwanza ni ya moja kwa moja (active) ambapo unahusika moja kwa moja kwenye kujifunza na unachukua hatua fulani wakati wa kujifunza.
Njia ya pili ni isiyo ya moja kwa moja (passive) ambapo unajifunza ila siyo moja kwa moja, na mara nyingi unakuwa huna hatua ya kuchukua wakati huo wa kujifunza.
Sasa katika njia hizi mbili, njia ya kwanza ndiyo ina nguvu kubwa sana kwenye kujifunza. Kwa sababu inajulikana kabisa kwamba watu huwa wanakumbuka zaidi kile walichofanya kuliko walichosoma au kusikia.
Hivyo inapokuja kwenye kujifunza, njia kubwa tunayotumia ni isiyo ya moja kwa moja, yaani kujisomea na kuangalia au kusikiliza masomo. Njia hii unaifanya kwa urahisi, lakini mara nyingi unakuwa huna hatua za kuchukua wakati wa kujifunza huko.
Kwa kujifunza kwa njia ya moja kwa moja, unahusika moja kwa moja kwenye mafunzo yanayotolewa, unauliza maswali moja kwa moja, unakuwa na mazoezi ya kufanya na unaondoka ukiwa umejifunza zaidi.
Tarehe 03/11/2018 tutakuwa na SEMINA YETU YA KISIMA CHA MAARIFA 2018 ambayo itafanyika kwa kukutana ana kwa ana jijini dar es salaam.
Wapo watu ambao wamekuwa sambamba na mimi tangu naanza huduma hii, na wamekuwa wanajifunza kila ninachofundisha, wamesoma kila kitabu ambacho nimeandika na wamehudhuria kila semina ya mtandaoni ninayotoa. Na wanachojiuliza kwa sasa ni je kuna kipya watakachojifunza kwa kushiriki semina hii ya kukutana ana kwa ana?
Kabla sijatoa majibu ya swali hilo, ambalo huenda na wewe unajiuliza, kwanza soma maoni ya mwanamafanikio mwenzetu, aliyetuandikia kuhusu hili;
Habari kocha, ni matumaini yangu kwamba hujambo na unaendelea vema na maandalizi ya Semina.
Baada ya kukaa chini kutathimini gharama ya Semina hii kwa upande wangu binafsi Nimeona ni ya gharama sana. Itanigharimu 350000/ tshs, hii yote ni kutokana na umbali wa dar na ninapokaa.
Lakini Pamoja na hivyo Nimeamua na nimejitoa kulipa gharama yote na nitahudhuria Semina hii.
Dukuduku Langu,
Najua tumekuwa pamoja kwa muda mrefu sasa, nimeshajifunza mengi uliotufundisha kuhusu maisha, biashara na hata Mafanikio. Nimeshahudhuria Semina zako mingi, na zimenisaidia sana kupiga hatua zaidi kwenye maisha yangu. Nashukuru sana katika hili.
Lakini sasa, je Semina hii ya leo ya gharama kubwa namna hii itakuwa ya mambo mapya tofauti na yale unayotufundisha kila siku kwa miaka mitano sasa?
#kitu gani kikubwa utashauri na kupendekeza tutegemee na hata tutarajie kunufaika nayo kupitia Semina hii?
*PENDEKEZO LANGU*
Kwa jinsi mfumo wa Semina hii unavyoonekana itakuwa ni Semina yenye mambo mengi mazuri ya kujifunza kwa Masaa machache. Ni Masaa 12 ya kuwa makini kusikiliza (yaani kuwa serious) bila utani.
Sasa kwa sababu tunataka kutengeneza jamii moja, na sisi ni watu tofauti tofauti, kwa maana kada tofauti, tumetoka Mazingira tofauti, n.k
Kwa maoni yangu ni muhimu kama tutapata muda wa kutambulishana na kujuana zaidi kupitia mkutano huu.
Sio mara zote wote tutapata fursa kama hii, hivyo inapotokea tuitumie vizuri.
Asante. N. M.
Na hivi ndivyo nilivyomjibu mwanamafanikio mwenzetu aliyeuliza kuhusu hili;
Salama N. M,
Hongera sana kwa kujitoa kufanya uwekezaji huo mkubwa ili kuweza kushiriki SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA.
Kuhusu vitu vya tofauti vya kujifunza, ndiyo vipo vingi sana. Kwanza kabisa kitendo cha kukutana pamoja kwenye semina ya live ni manufaa makubwa sana. Unaweza kujifunza vitu vingi sana kwa kusoma, kusikiliza na kuangalia, lakini uwepo wa moja kwa moja unakuwa na nguvu ya kipekee kabisa.
Pia kwenye semina hizi huwa naandaa mkakati wa kila mmoja wetu kwenda kufanyia kazi kwa mwaka mzima, kitu ambacho ni tofauti na semina za kawaida za mtandaoni.
Kuhusu nafasi ya kujuana, kwenye kila semina huwa naweka muda mwingi wa watu kujuana kwa kuanza na utambulisho wa kila mmoja na pia kuna mapumziko mengi, ya chai, chakula na mapumziko ya jioni, yote hayo huwa nasisitiza watu waongee na watu tofauti.
Na dhumuni langu kuu kwenye kila semina ni kupata nafasi ya kuongea na kila aliyeshiriki, ana kwa ana na kuongea maneno machache.
Karibu sana kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, itakuwa na manufaa bora kabisa kwako.
Kocha Makirita.

Hilo ni jibu kwa kifupi, lakini leo nimekuandalia jibu refu, jibu linalozama ndani zaidi na kukuonesha kwa nini ni muhimu mno kuhudhuria semina ya moja kwa moja.
Hizi hapa ni faida tano za kuhudhuria semina ya kushiriki moja kwa moja, kama SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018.
- Kujuana na watu wapya.
Kwenye mafanikio ipo kauli inayosema utajiri wako ni sawa na mtandao wako (YOUR NETWORTH IS EQUAL TO YOUR NETWORK). Kadiri unavyokuwa na mtandao mkubwa wa wanaokujua na unaowajua, ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kufanikiwa. Kwa sababu ni kupitia watu wapya ndiyo utapata mawazo mapya, utapata hamasa mpya na huenda ukapata watu wa kushirikiana nao kwenye mambo mbalimbali.
Hivyo kushiriki semina za moja kwa moja, unapata fursa ya kujuana na watu wapya na kukuza mtandao wako, kitu ambacho siyo rahisi kama hukutani na watu wapya. Pia watu wengi huwa wanakutana na watu wale wale ambao wamezoeana nao na hawana kipya cha kuongeza kwenye maisha yao.
- Kukutana na watu wenye fikra zinazoendana na zako.
Faida nyingine kubwa ya kushiriki semina za moja kwa moja ni kukutana na watu ambao wana fikra zinazoendana na zako, watu wenye mtazamo sawa na wako na ambao mnaongea lugha moja.
Kwenye semina kama ya KISIMA CHA MAARIFA, unakutana na watu ambao wana kiu ya mafanikio makubwa, watu ambao wanajua wanaweza kufanya zaidi na wapo tayari kufanya, watu wasiokata tamaa wala kuwasikiliza wakatishaji tamaa.
Ni vigumu sana kuwapata watu wa aina hii kwenye maisha yako ya kawaida, na huenda wengi wanakushangaa na kukuona wa ajabu. Unapohudhuria semina za aina hii, unakutana na watu wanaoendana na wewe na hili linakufanya uone upo kwenye njia sahihi kwako kufikia mafanikio makubwa.
- Unanyonga nguvu chanya inayokuwepo kwenye semina.
Tofauti kubwa ya semina ya kushiriki moja kwa moja na semina ya mtandaoni ni namna gani unapata ile nguvu inayoambatana na mafunzo unayopata. Unaposhiriki semina ya moja kwa moja, ile nguvu inayokuwepo kwenye eneo la semina, yote inakuingia ndani yako na inakuwa na msukumo mkubwa sana kwako.
Fikiria kitu chochote ambacho umewahi kuangalia au kuhadithiwa na kushiriki moja kwa moja, tofauti ni kubwa. Fikiria msiba ambao ulihadithiwa na msiba ambao ulihudhuria, upi ulipata majonzi makubwa?
Kila unachoshiriki moja kwa moja, kuna nguvu kubwa sana unayoondoka nayo. Unaposhiriki semina ya mafanikio kama ya KISIMA CHA MAARIFA, unaondoka na nguvu kubwa itakayokupa hamasa ya kufanya makubwa zaidi.
- Kupata mafunzo mfululizo bila ya kukatisha katisha.
Unapohudhuria semina ya moja kwa moja, unakuwa umetenga muda wako wote kujifunza, huna cha kukukatisha na kukuondoa kwenye mfululizo wako wa mafunzo. Kama ni masaa 10 utajifunza kwa masaa hayo kumi.
Lakini semina ambazo siyo za moja kwa moja, kama ya mtandaoni, ni rahisi sana kubaki nyuma kwa kushindwa kwenda na mfululizo. Labda kinatokea kitu kinakukatisha kwenye mafunzo na unajiambia utakuja kuendelea. Mwisho unajikuta umerundika masomo mengi ambayo unajiambia utayapitia lakini hupati muda wa kufanya hivyo.
Kwa kutenga siku moja ambayo utajifunza vitu vingi na kupanga kwenda kuvifanyia kazi, utajifunza mengi na kuweza kuchukua hatua bila ya kubaki nyuma.
- Unaondoka ukiwa umeelewa vizuri.
Faida nyingine kubwa ya kushiriki semina ya moja kwa moja ni kuondoka ukia umeelewa vizuri. Mara nyingi kuna vitu unaweza usielewe pale unapokuwa unasoma mwenyewe, lakini unapokutana na anayefundisha, unaelewa vizuri. Na pia usipoelewa, una nafasi ya kuuliza swali na ukajibiwa. Na hata usipopata nafasi ya kuuliza swali basi utaweza kupata hata dakika moja ya kukutana na anayefundisha na kuuliza chochote ulichonacho.
Kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018 utapata nafasi kubwa ya kuuliza chochote ambacho umekuwa huelewi kwenye masomo ya mwaka mzima. Utaweza kupata mifano halisi ya jinsi ya kutumia yale unayojifunza ili kuweza kupiga hatua zaidi.
NYONGEZA; FAIDA YA ZIADA YA KUSHIRIKI SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA.
Sehemu kubwa ya watua ambao wananufaika na huduma ninazotoa za maarifa, hatujawahi kukutana ana kwa ana. Wengi wapo mikoa mbalimbali na hata kwa wale waliopo karibu, bado changamoto ya muda inazuia tusiweze kuonana.
Kushiriki SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA tunapata nafasi nzuri ya kukutana ana kwa ana. Na hili ni jambo ambalo kwa mazingira ya kawaida ni gumu, lakini kwenye semina tunakuwa pamoja kwa siku nzima, na tunaweza kuzungumza mengi kuhusu maisha na mafanikio kwa ujumla.
Rafiki, kuna thamani kubwa sana kwenye kushiriki semina ya moja kwa moja, hata kama unayokwenda kujifunza ni yale yale. Kama ambavyo ilivyo muhimu kwenda kwenye nyumba za ibada hata kama una vitabu vya dini nyumbani au hata unaweza kufuatilia mafundisho kwa tv au redio.
KARIBU KWENYE SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018.
Rafiki, tarehe 03/11/2018 ndiyo siku ya SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, semina hii itafanyika kwenye moja ya hoteli zilizopo jijini dar es salaam.
Itakuwa ni semina ya siku nzima, kuanzia saa moja asubuhi mpaka saa moja jioni. Yatakuwa ni masaa 12 ya kujifunza, kujuana na wengine, kuhamasika na kuweka mkakati wa kwenda kufanyia kazi kwa mwaka mzima.
Ada ya kushiriki semina hii ni tshs 100,000/= (laki moja) ada ambayo itajumuisha huduma zote za siku ya semina, kuanzia chai, chakula cha mchana, vitafunwa vya jioni, vijitabu vya kuandikia na kalamu.
Ili kupata nafasi ya kushiriki semina hii, unapaswa kulipa ada yako kabla ya tarehe 31/10/2018, ambayo ndiyo tarehe ya mwisho ya kulipia ada.
Pia nafasi za kushiriki semina hii ni 100 pekee, na zilizobaki ni chache sana. hivyo kama hutaki kukosa nafasi hii, lipa ada yako mapema ili tuweze kuwa pamoja kwenye semina hii.
Nakusubiri kwa hamu sana rafiki yangu kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, kwa sababu yapo mengi mazuri nimekuandalia kwa mafanikio yako kwa mwaka 2018/2019.
Namba za kufanya malipo ili kushiriki semina hii ni MPESA- 0755 953 887 au TIGO PESA/AIRTEL MONEY – 0717 396 253. Majina ya namba hizo ni AMANI MAKIRITA. Ukituma fedha tuma na ujumbe wa kueleza umefanya malipo ya semina, ukiambatana na jina lako na namba yako ya simu kwa ajili ya kupewa taarifa zaidi za semina.
Ni mimi rafiki na kocha wako,
Dr. Makirita Amani,