Ukiwa mbali na msitu, unachokiona ni msitu, unaona miti ambayo imefunga kila eneo na hutaweza kuiona ardhi kwa wazi wazi. Lakini unapoigia ndani ya msitu, huwezi tena kuuona msitu, badala yake unaona mti mmoja mmoja, unaona ardhi na vitu vingine vidogo vidogo ambavyo kwa mbali havionekani.

Hivi ndivyo maisha yetu yalivyo, tukiangalia kwa mbali tunayaona maisha yalivyo, labda mazuri au mabaya. Lakini tunapoishi siku moja moja, tunaona siku za kawaida, siku ambazo hazina cha tofauti sana.

Wakati unaziishi siku zako kwa ukawaida, ukipoteza muda hapa na pale, ukijaribu vitu mbalimbali na kutokuweka juhudi kubwa, siku zinapita na maisha yanaendelea. Inafika siku unaangalia maisha yako, unaona umri umekwenda, lakini hakuna kikubwa umefanya.

Na hapa ndipo unajiuliza swali kubwa na lenye uchungu sana, maisha yangu yamepotelea wapi? Nilikuwa nafanya nini kwa miaka 5, 10, 20, 30 na hata 50 iliyopita?

Hili ni swali ambalo ukisubiri uje kujiuliza baadaye, utakuwa umeshachelewa sana. Nakushauri ujiulize swali hili kila siku, kwa sababu maisha ya mafanikio ni mkusanyiko wa siku zenye mafanikio. Kadhalika maisha ya kushindwa ni mkusanyiko wa siku zenye kushindwa ndani yake.

Kama utajiuliza swali hili kila siku ya maisha yako, kwa kujiuliza wapi umeyapoteza maisha yako kwa siku husika, utaona kwa haraka yale unayofanya ambayo siyo muhimu kwako. Utaweza kuhukumu kila unachofanya na kuona kama ndiyo muhimu zaidi kufika kule unakotaka kufika.

Muhimu ni ujilazimishe kuuona msitu kama vile upo mbali na msitu, wakati upo ndani ya msitu. Hapa lazima uwe na maono ya juu, uwe kama mtu ambaye anayaangalia maisha yako kwa mbali na kuona kama ni bora au siyo bora.

Jinsi unavyochagua kuitumia dakika yako moja, kuna mchango mkubwa sana wa jinsi gani maisha yako yataishia. Ukiruhusu mazingira ya nje ndiyo yawe msukumo kwako wa hatua gani unazochukua na yapi unayofanya, utafika mwisho wa maisha yako na kujiuliza maisha yamepotelea wapi.

Lakini kama kila siku utajiuliza ni wapi unayapoteza maisha yako, itakuwa rahisi kwako kuchukua hatua mapema.

Njia nyingine bora ya kukumbuka unakokwenda na kuchukua hatua sahihi ni kujikumbusha malengo yako makubwa mara kwa mara. Tena ukifanya hivyo kwa kuandika, na ukafanya hivyo kila siku, itakuwa rahisi kujikamata pale unapofanya kitu ambacho hakiendani na malengo yako.

Usisubiri mpaka umri wako umeenda sana na uanze kujiuliza maisha yako yalipotelea wapi, badala yake jiulize kila siku unayapotezea wapi maisha yako na utaepuka sana kuyapoteza maisha yako kwa mambo yasiyo muhimu kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha