“If I do something that others don’t like but I feel good about, I’m happy. If others praise something I’ve done, but I’m not satisfied, I feel unhappy.” – Warren Buffett.
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KIPIMO CHA NDANI NA CHA NJE…
Rafiki, ni nini kinachokusukuma wewe kufanya kila unachofanya kwenye maisha yako.
Msukumo unaokupelekea kufanya maamuzi na hata kuchukua hatua unatoka wapi?
Kuna vipimo na misukumo miwili ambayo wengi wanaitumia.
Msukumo wa ndani, hapa mtu anafanya kitu kwa sababu ni muhimu na kina maana kwake, bila ya kujali wengine wanasema au kufanya nini.
Pia kuna msukumo wa nje, hapa mtu anafanya kitu kwa sababu wengine wanafanya au wengine wanasema afanye haya kama hakina maana wala umuhimu kwake.
Swalo ni je, wewe msukumo wako unatoka wapi?
Jiulize kazi unayofanya, mavazi unayovaa, biashara unayofanya, na kila kitu ulichonacho kwenye maisha yako, je unacho kwa sababu kina maana kwako au ni kwa sababu wengine nao wanavyo au umekuwa navyo ili wengine pia waone unavyo?
Kama msukumo unatoka ndani, unafanya kitu kwa sababu ni muhimu na kina maana kwako, maisha yako yatakuwa bora na ya furaha, bila ya kujali ni nini unacho au nini umekosa.
Kama msukumo unatoka nje, unafanya kwa sababu wengine wanafanya, au unataka kuwafurahisha wengine au wengine wanategemea ufanye, utafanya lakini maisha yako bado yatakuwa na utupu. Hata kama watu watakusifikia kwa nje, ndani yako utaujua ukweli na maisha yako hayatakuwa bora hata kama una vitu vingi kiasi gani.
Tumia msukumo wa ndani katika kufikiro, kufanya maamuzi na hata kuchukua hatua. Fanya kilicho muhimu kwako na chenye maana kwako, bila ya kujali wengine wanafanya nini au wanategemea ufanye nini.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutumia msukumo wa ndani kufanya makubwa zaidi kwenye maisha yako.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha